Ni hali iliyowazi kwamba maisha yanakuwa magumu kadiri siku zinavyokwenda. Na gharama za maisha zinaongezeka huku vipato vya Ajira vikibaki pale pale au kuongezeka kidogo sana. Hali hii imewafanya waajiriwa wengi kujiingiza kwenye ujasiriamali. Hivyo licha ya kipato cha ajira wanapata kipato kingine cha ziada kupitia ujasiriamali wanaofanya. Waajiriwa wanakuwa na mipango mizuri sana ya kibiashara na kutafuta mtaji wa kuwafanya waweze kuingia kwenye biashara hizo. Ila wanapokuwa kwenye biashara wanakutana na changamoto nyingi zinazosababisha biashara ishindwe kuku ana wakati mwingine kufa kabisa.
Ukiangalia biashara nyingi ambazo zinafanywa au kusimamiwa na waajiriwa, zinakuwa na matatizo mengi, hazikui na mbaya zaidi pale mwajiriwa anapokuwa ameondoka kwenye kazi, iwe kwa kuacha au kustaafu biashara hizi hazichukui muda nazo zinakufa. Ni kitu gani kinasababisha matatizo haya kwenye biashara za watu ambao bado wapo kwneye ajira? Leo tutaangalia hili kwa undani.
Watu wengi ambao nimewashauri kwenye biashara zao na ambao ni waajiriwa, nimekuwa nakutana na kitu kimoja ambacho kinajirudia kwa kila mwajiriwa mwenye changamoto ya kibiashara. Leo tutajadili kitu hiko ili na wewe usiendelee kukutana na changamoto kwenye biashara zako kwa kufanya kitu hiki iwe ni kwa kujua au kwa kutokujua.
Watu wengi ambao wameajiriwa na wanafanyabiashara pia wamekuwa wanashindwa kutenganisha kipato cha biashara na kipato cha ajira zao. Hivyo wanakuwa ni kama wana kapu moja na humo ndani wanaweka fedha yoyote wanayoipata, mshahara humo humo na faida ya biashara humo humo. Hatari kubwa wanayokutana nayo ni pale ambapo kipato kimoja hasa mshahara hakiingii tena wakati huo wanaendelea kutoa kile kipato kinachotokana na biashara. Na hapa ndio mwanzo wa biashara kufa.
Wafanyabiashara hawa ambao pia ni waajiriwa, wanapokuwa na changamoto ya fedha hutoa fedha kwenye biashara kwa ajili ya matumizi. Na wanapopata mshahara hurudisha fedha hizo. Unaweza usione madhara yake kwa haraka kwa sababu utafikiria hata hivyo zote si ni fedha zangu? Lakini ukweli ni kwamba unailemaza biashara, unairudisha biashara nyuma na unaiofanya biashara ishindwe kujiendedha yenyewe. Biashara inayotolewa fedha na kurudishwa kila mara ni biashara ambayo haiwezi kujitegemea yenyewe. Na ikitokea mmiliki wa biashara hana tena kipato cha ziada biashara inakufa.
Ufanye nini ili kuondokana na changamoto hii?
Jambo kubwa unalotakiwa kufanya haraka sana ili kuondokana na changamoto hii na kuokoa biashara yako na hatari ya kufa ni kujenga nidhamu ya fedha zako binafsi na fedha za biashara. Jua mtaji wa biashara yako ni kiasi gani na weka mtaji huo kwenye biashara. Ukishaweka mtaji huo acha biashara ijiendeshe yenyewe, usitoe wala kuweka fedha kila mara. Na kwa kusisitiza usitoe fedha kabisa, ila kama kuna kitu muhimu cha kuongeza ongeza fedha. Hata kama una shida ya fedha kiasi gani angalia kwanza njia nyingine unayoweza kutatua tatizo lako la fedha na sio kufikiria kutoa fedha kwneye biashara. Unahitaji nidhamu kubwa sana ili kuweza kulisimamia hili, lakini inawezekana.
Hakikisha biashara inawezakujiendesha yenyewe kwa faida bila yaw ewe kuingilia kila mara. Kama kuna changamoto yoyote jua kwanza ni kitu gani kinasababisha changamoto hiyo kabla hujaweka fedha zaidi. Hii ni muhimu sana kwenye ukuaji wa biashara yako. Kuendesha biashara isiyokua kwa muda mrefu halafu ikaja kufa pale ambapo ndio ulitaka kuitegemea ni jambo linaloweza kukuumiza sana. Anza kulifanyia kazi sasa kabla mambo hayajawa mabaya zaidi.
Wafanyabiashara wengine huwa na mawazo kwamba acha biashara hii iende ilivyo ila nikishastaafu na kupata fedha zangu za mafao nitaikuza vizuri zaidi. Huu ni uongo unaokufanya uendelee kuharibu biashara yako kwa sasa. Ni lazima uweze kuisimamisha biashara inayojiendesha kwa faida hata kwa mtaji kidogo kabla hujaweka mtaji mkubwa. Kama biashara ina mtaji wa milioni kumi lakini inajiendesha kwa hasara, unafikiri ni kitu gani kitatokea utakapoweka milioni 50? Utaongeza hasara uliyokuwa unapata awali.
Kama umeajiriwa na pia una biashara yako pembeni nakupa hongera sana, na zingatia kuijenga biashara inayoweza kujiendesha yenyewe bila ya kutegemea mshahara wako. Kama unapata changamoto zaidi kwenye uendeshaji wako wa biashara tuwasiliane kwa mawasiliano yangu yaliyopo hapo chini. Nakutakia kila la kheri.
TUPO PAMOJA.