Kuna biashara nyingi ambazo zinaanzishwa lakini hazifiki mbali. Kuna biashara ambazo zimekuwepo kwa kitambo kirefu lakini hazina mabadiliko yoyote kwenye ukuaji, na baada ya muda zinakufa kabisa. Sio kwamba wanaoanzisha biashara hizi hawana mawazo mazuri, wengi wana mawazo mazuri ya biashara. Wengi wanakuwa wamefanya biashara yenye mafanikio lakini baada ya muda fulani mambo yanaonekana kubadilika na mtu kushindwa kwenye biashara.

Changamoto inayozikumba biashara nyingi ni kukosa misingi muhimu ya kibiashara. biashara inapokuwa ndogo haikutani na changamoto zinazotokana na kukosa misingi ya kibiashara. Ila inapokua ndio changamoto zinazotokana na kukosa misingi zinaibuka na kuifanya biashara kushindwa na kufa haraka sana.

Leo tutajadili misingi mitatu muhimu ya kuijenga biashara yako. Kwa kusimamia misingi hii na ukaweka juhudi biashara yako itaendelea kukua siku hadi siku.

Msingi wa kwanza; Wasaidie watu wengi.

Msingi wa kwanza wa kujenga biashara yako ni kusaidia watu wengi. Usiingie kwenye biashara au kuendelea kuwa kwenye biashara kama hujui biashara yako inamsadia mtu gani. Kwa chochote unachofanya kwenye biashara yako kilenge kwenye kuwasaidia watu wengi. Watu wana matatizo, watu wana changamoto na wangependa kuondokana nazo. Ifanye biashara yako iwe suluhisho la changamoto na matatizo ambayo watu wanakuwa nayo. Na katika kuwasaidia kutatua matatizo yao wanakupa fedha na unatengeneza faida kupitia biashara yako. Bidhaa au huduma unayouza iwe imelenga kuwasaidia watu wengi kuwa na maisha ambayo ni bora kuliko yalivyo sasa. Japokuwa mafanikio ya biashara yako yanategemea faida, lengo lako lisiwe kutengeneza faida tu, bali liwe kuwasaidia watu na wao wakulipe, katika hali hii utatengeneza faida kubwa sana, hasa unapotatua tatizo linalosumbua watu wengi.

Msingi wa pili; Fanya kilicho sahihi.

Katika wakati wowote kwenye biashara yako, fanya kile ambacho ni sahihi. Usijiingize kwenye shughuli zozote ambazo zitaharibu sifa yako ya kibiashara. unahitaji kuwa mwaminifu ili wateja waweze kukuamini na kuendele akufanya biashara na wewe. Ukianza kufanya vitendo ambavyo sio vya kiaminifu haitakuchukua muda watu watajua na wataacha kufanya biashara na wewe. Tumekuwa tunaona watu wengi wanafanikiwa haraka kwenye biashara ambazo sio halali, lakini ni kitu gani ambacho kinatokea baada ya hapo? Wnaporomoka haraka kuliko hata walivyopanda. Usikubali tamaa ya muda mfupi ikufanye uchukue maamuzi ambayo baadae yataharibu sura ya biashara yako. Usijidanganye kwamba ukifanya mara moja tu hakuna atakayejua, utajenga tabia na baada ya muda kila kitu kitakuwa wazi. Timiza kile ambacho unaahidi na boresha biashara yako kila siku. Mteja atakuwa na amani ya kufanya biashara na wewe kama atakuwa na uhakika wewe ni mtu wa kuaminika na unayefanya kile unachosema.

Msingi wa tatu; Ilipe jamii inayokuzunguka.

Hakuna biashara ambayo inajitegemea yenyewe kama yenyewe. Biashara zipo kwenye jamii na jamii hizi ndio zinafanya biashara ikue na kupata mafanikio. Hata kama sio kila mtu kwneye jamii ni mteja wako, kuna wengi ambao wamechangia wateja wako kuendelea kuwepo. Biashara yako inatakiwa kujali jamii inayozunguka biashara hiyo. Kushiriki kwenye shughuli mbalimbali zinazolenga kuboresha jamii husika na hata kusaidia baadhi ya jitihada zinazofanywa na wanajamii katika kuboresha jamii husika. Biashara yako inatakiwa kuw ana sura ya kijamii na sio kuonekana kama watu ambao mpo pale kuchuma fedha tu. Unahitaji kuwa mmoja wa wanajamii na kusaidia katika ustawi wa jamii nzima.

Kwa misingi hii mitatu biashara yoyote itaweza kusimama na kuwa na mafanikio kw akipindi kirefu. Biashara inapoanza kwenda kinyume na misingi hii, kama kutaka kupata faida kwa kunyonya wengine na kutoa huduma ambazo zipo chini ya kiwango ndio zinaanza kushindwa na hatimaye kufa kabisa. Jenga biashara yako kwenye misingi hii mitatu na furahia matunda mazuri utakayoyavuna kupitia biashara yako. Kila la kheri.

TUPO PAMOJA.