Biashara yako ina ukomo wake wa kukua, yaani biashara inaweza kukua mpaka itakapofikia ukomo huo utakaoujua leo. Bila ya kujua ukomo hii ni vigumu sana kwa biashara yako kuweza kukua zaidi.

Wafanyabiashara wengi ambao biashara zao zimedumaa hawajui kwamba tayari zimefikia ukomo. Hivyo hukazana kufanya mambo mengi ambayo bado hayasaidii ukuaji wa biashara hiyo. Leo nitakushirikisha kikomo cha biashara yako na jinsi unavyoweza kukiepuka.

Kabla hatujakiangalia kikomo hiko, tuiangalie biashara kama chupa ya soda au ya bia kama utapenda kufikiria hivyo. Chupa ina nafasi kubwa sana ndani yake, ila kwenye mdomo wa chupa ni nafasi ndogo sana (nyembamba). Kimiminika kinaweza kuingia kwenye chupa hiyo ila kikomo chake ni mdomo wa chupa. Kikishafika pale hakuna jinsi unaweza kuweka zaidi. Sasa kila biashara ina mdomo wake wa chupa, na hapa ndipo kwenye kikomo cha ukuaji wa biashara yoyote.

Kikomo cha ukuaji wa biashara yako ni kikomo chako cha kujifunza. Yaani pale ambapo utaacha kujifunza kuhusu biashara unayofanya na biashara kwa ujumla hapo ndipo biashara inapoacha kukua. Hapo inakuwa imefikia kikomo na hata ukiweka juhudi kiasi gani hakuna ukuaji utakaoongezeka. Kwa kifupi wewe mwenyewe na kujifunza kwako ndio mdomo wa chupa kwenye biashara yako.

Biashara yako haiwezi kukua kukuzidi wewe mmiliki wa biashara. Biashara yako haiwezi kukua kama wewe mmiliki hukui. Kama unataka biashara yako ikue, anza kukua wewe kwanza.

Unawezaje kukua wewe ili na biashara yako ikue?

1. Soma makala za biashara na ujasiriamali, soma kipengele hiki cha biashara leo na jiunge na KISIMA CHA MAARIFA ili upate nafasi ya kujifunza zaidi.

2. Soma vitabu vinavyohusiana na biashara na ujasiriamali, soma vingi uwezavyo, kwenye kila kitabu utajifunza mbinu tofauti tofauti.

3. Hudhuria semina mbalimbali zinazohusiana na biashara na ujasiriamali, huku utajifunza mengi kupitia kwa watu waliofanikiwa zaidi.

4. Jifunze kutokana na makosa yako na ya wengine pia. Jifunze kwa yale unayofanikiwa na wengine wanavyofanikiwa.

Ni rahisi kama hivyo, unataka biashara yako ikue, anza kukua wewe kwanza.

Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.

Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa. Kujifunza mengi zaidi kuhusu mafanikio kwenye maisha jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.