Wafanyabiashara wengi wadogo wamekuwa wanafanya kosa moja kubwa sana linalogharimu ukuaji wa biashara zao. Kwa kufanya kosa hili wamekuwa wakishindwa kukuza biashara zao na hivyo biashara kufa au kubaki kwenye kiwango kilekile. Kosa kubwa ambalo wafanyabiashara wengi wadogo wamekuwa wanafanya ni kufikiri kwamba biashara ndogo ni aina ndogo ya biashara kubwa. Yaani kufikiri kwamba biashara ndogo ni kama mdogo wa biashara kubwa na hivyo wakitumia mbinu zilezile ambazo biashara kubwa zinatumia basi wataweza kufikia ngazi hizo za biashara kubwa.
Hili ni kosa kubwa sana, biashara ndogo na biashara kubwa sio vitu viwili ambavyo vipo kwenye kundi moja ila ngazi mbili tofauti. Biashara ndogo na biashara kubwa ni vitu viwili tofauti kabisa na vinavyohitaji mbinu tofauti. Ukitumia mbinu za biashara kubwa kwenye biashara ndogo, unajihakikishia kushindwa kwenye biashara yako hiyo ndogo.
Ni ipi tofauti ya biashara ndogo na biashara kubwa?
Ukilinganisha biashara hizo mbili, ndogo na kubwa kuna tofauti kubwa sana. Na tofauti hii inaletwa na ukubwa na udogo. Biashara kubwa ina mtaji mkubwa, ina wafanyakazi wengi, inaweza kuwafikia wateja wengi, ina mtandao mkubwa na vitu vingine muhimu. Kwa upande wa pili biashara ndogo ina mtaji mdogo, ina wafanyakazi wachache, inaweza kufikia wateja wachache na pia inaweza kuwa na mtandao mdogo. Kwa tofauti hii biashara kubwa inakuwa kwenye kundi lake na biashara ndogo inakuwa kwenye kundi lake. Na ili kuondoka kwenye kundi la biashara ndogo kwenda kwenye biashara kubwa unahitaji kuwa na mbinu tofauti na zinazotumika na biashara kubwa.
Ukijaribu kutumia mbinu zinazotumiwa na biashara kubwa kwenye kukuza biashara yako ndogo utajikuta kwenye matatizo makubwa kibiashara. Kwa mfano biashara kubwa ina mtaji mkubwa na hivyo kuweza kuwekeza kwenye matangazo ambayo ni gharama lakini yanawafikia wengi. Wewe kama una biashara ndogo kujaribu kufanya hivi unaweza kumaliza mtaji wako wote na bado usipate majibu unayotarajia. Badala ya wewe kufikiria kuwekeza kwenye matangazo ya gharama kubwa, unahitaji kuwa na njia ambayo itawavutia wateja kuja kwenye biashara yako. Unahitaji kujenga ukaribu na wateja wako ili waendelee kukuletea wateja wengi zaidi.
Mambo muhimu ya kufanya ili kukuza biashara yako kutoka ndogo na kuwa kubwa.
Tumeshaona biashara ndogo na biashara kubwa ni vitu viwili tofauti. Na kama unataka kukuza biashara yako kutoka ndogo na kwenda kubwa unahitaji mbinu za pekee ili kuweza kufikia hatua hiyo. Hapa nakushirikisha baadhi ya mbinu unazoweza kutumia kukuza biashara yako ndogo.
1. Angalia ni jinsi gani unaweza kushirikiana na biashara kubwa. Katika kila biashara unayofanya, kuna biashara kubwa ambazo zinaweza kuwa na uhusiano na biashara unayofanya. Zijue biashara hizi na jua ni jinsi gani unaweza kushirikiana nazo. Angalia ni jinsi gani biashara hizo zinaweza kunufaika na biashara yako ili na wewe uweze kunufaika nao kwa sababu tayari wana wateja wengi. Kwa mfano kama una bidhaa au huduma ambayo itawanufaisha wateja wa biashara kubwa ila kwa sasa hawaipati, unaweza kukaa na biashara hiyo kubwa na kuwaonesha ni jinsi gani ushirikiano wenu utamnufaisha kila mmoja wenu. Wao wanaongeza thamani kwa wateja wao na wewe unaongeza wateja wengi zaidi.
2. Angalia jinsi ambavyo unaweza kupata matangazo ya bure. Kama unahitaji kutumia vyombo vya habari ili kuwafikia watu wengi zaidi na biashara yako kujulikana, basi angalia jinsi ambavyo unaweza kupata nafasi hii bila ya kulipia gharama kubwa. Kupitia biashara yako unaweza kufanya tukio lolote la kijamii ambalo litaonekana kama habari inayofaa kuripotiwa na hivyo wewe kupata nafasi ya kufikisha ujumbe wa tukio ulilofanya na biashara yako pia. Kwa mfano unaweza kuhamasisha usafi wa mazingira na ukachagua siku ambayo utawashawishi watu wengi kujitokeza, au kutoa misaada mbalimbali. Hufanyi hivi kwa sababu tu unataka utangazwe, ila unafanya kusaidia jamii na wakati huo huo kukuza biashara yako zaidi.
3. Kuwa karibu na wateja wako na wapatie huduma bora sana. Biashara kubwa iko mbali sana na wateja wake. Kuna ngazi nyingi sana kwenye biashara kubwa kiasi kwamba wenye nafasi za maamuzi kwenye biashara hizo hawawezi kukutana na mteja moja kwa moja. Ila wewe kwenye biashara yako ndogo unaweza kukutana na mteja moja kwa moja, ukajua matatizo yake na changamoto anazopitia. Tumia ukaribu wako huu na wateja kujenga uaminifu na kuwapa huduma bora ambazo zitawafanya waitangaze biashara yako kwa watu wao wa karibu.
Kama upo kwenye biashara ndogo, una nafasi kubwa sana ya kuweza kukuza biashara yako kama utakuwa na mipango mizuri na kuacha kuichukulia biashara yako kama sehemu ndogo ya biashara kubwa. Ifanye biashara yako kuwa ya tofauti na utaweza kuikuza na kuwa kubwa.
TUPO PAMOJA.