Linapokuja swala la kutangaza biashara, watu hufikiria matangazo kwenye vyombo vikubwa vya habari, kupata tangazo wakati wa taarifa ya habari, ambapo watu wengi wanaangalia. Au kudhamini michezo inayofuatiliwa na wengi. Au kuweka bango kubwa kwenye eneo ambalo watu wengi wanapita. Hizi zote ni njia nzuri za kutangaza biashara yako, ila pia zina gharama kubwa. Kama wewe ni mfanyabiashara mdogo au wa kati ni vigumu sana kuweza kutumia njia hizi kukuza biashara yako.
Je kama wewe ni mfanyabiashara ambaye huwezi kuwekeza fedha nyingi kwenye matangazo ndio umeshindwa kwenye biashara? Jibu ni hapana, kuna njia moja unayoweza kuitumia kutangaza biashara yako ambayo ina nguvu kubwa kuliko hata matangazo yanayolipiwa fedha nyingi. Kwa njia hii unakuwa na uhakika wa kupata mteja kwa kila tangazo unalotoa. Tofauti na matangazo ya kwenye vyombo vya habari ambapo watu hufanya mambo yao mengine wakati wa matangazo.
Njia ninayotaka kukushirikisha leo ni kuwatumia wateja wako kama sehemu ya kutangaza biashara yako. Wateja ambao unao sasa na wameridhishwa na husuma unayowapatia kupitia biashara yako, ni sehemu nzuri sana ya kutangaza biashara yako na ukawa na uhakika wa kupata wateja wengi zaidi. Ili uweze kuwatumia wateja wako kama sehemu ya kutangaza biashara yako, kuna mambo muhimu unayopaswa kuyajua na kuyafanyia kazi.
Jambo la kwanza ni kuwahamasisha wateja wako kuwaambia watu wengine kuhusiana na biashara yako. Kama unamuuzia mtu kitu unaweza kumwambia kama kuna watu wengine anaowafahamu na wanaweza kunufaika na biashara hiyo asisite kuwaambia ili nao wanufaike kama anavyonufaika wewe. Pia tambua juhudi za wateja wako wanaowaambia wengine ili waone kile wanachofanya kinathaminika na kuheshimika. Hapa unaweza kuwapa punguzo la bei au hata kuwapa zawadi nzuri na wakawa watu wazuri wa kukutangazia biashara yako.
Kitu kingine cha kufanya ni kuomba ridhaa ya mteja wako kutumia taarifa za mtu wake wa karibu ili kutangaza biashara yako. Kama umemuuzia mtu bidhaa au huduma unaweza kumuuliza ni mtu gani wa karibu kwake anayemfahamu na anaweza kunufaika na bidhaa au huduma unayotoa na ana uhakika wakijua watanunua. Baada ya mteja kukupatia mtu au watu hawa, muombe ruhusa ya kuwasiliana na hao watu kupitia jina lake. Yaani utawasiliana na hao watu na kuwaambia mtu fulani alinunua kitu hiki kutoka kwenye biashara yetu na anafikiri kitakufaa pia, na hapa unampa sifa za bidhaa au huduma mnayotoa. Kwa kutumia njia hii unakuwa unatangaza kwa mteja ambaye kwa kiasi kikubwa atanunua na kuwa mteja wako. Njia hii ya kuongea na mteja mpya wewe mwenyewe badala ya mteja anayempendekeza inahakikisha unampatia mteja mpya taarifa za kutosha na za kumshawishi achukue hatua.
Kitu cha mwisho unachotakiwa kufanya ni waombe wateja wako walioridhishwa na huduma zako kutoa ushahidi wa jinsi walivyonufaika na huduma au bidhaa unazotoa. Hakuna kitu chenye nguvu kama ushuhuda wa mteja. Mteja ambaye alikuwa na matatizo fulani ila alipofika kwenye biashara yako akapata suluhisho ambalo limeboresha maisha yake. Kwa kutumia ushuhuda huu kwa watu wengine kuna ambao watakuwa na matatizo kama aliyokuwa nayo mteja aliyetoa ushuhuda na hivyo kuchukua hatua. Njia ya ushuhuda ina nguvu sana na imekuwa inatumika kwa miaka mingi na kwenye huduma nyingi. Itumie na wewe kwenye biashara yako lakini kuwa mkweli, usijaribu kudanganya. Ushuhuda huu unaweza kuwa nao kwa maandishi ambayo ameandika mteja aliyeridhika au kurekodi sauti au picha za mteja akizungumza jinsi maisha yake yamekuwa bora.
Wateja ulionao sasa kwenye biashara yako ni sehemu nzuri sana ya kuanza kuitangaza biashara yako na ambayo haihitaji gharama kubwa. Watumie wateja hawa vizuri kukuza biashara yako na kuweza kuwafikia wengi zaidi. Nakutakia kila la kheri kwenye maboresho ya biashara yako.
TUPO PAMOJA.