Wamiliki wengi wa biashara huwa wanapenda kuweka matatizo ya biashara zao kuwa siri yao wenyewe. Hata watu ambao wanahusika na biashara hiyo kwa karibu sana hawapati nafasi ya kujua kama biashara ipo kwenye matatizo. Watu kama wafanyakazi wa biashara hiyo wanakuwa hawajui kama biashara ipo kwenye matatizo na hivyo kuendelea na kazi zao kama walivyozoea.
Mmiliki wa biashara unaweza kuwa na sababu ya msingi kabisa ya kutowaambia watu hawa kwamba biashara ipo kwenye matatizo kwa kuogopa kuwavunja moyo. Labda biashara imepata hasara kubwa, labda kuna manunuzi ulifanya na yamekwenda vibaya, labda biashara inapoteza mteja muhimu na hivyo kuwa hatarini. Kuna matatizo mengi ambayo mmiliki wa biashara anaweza kuona ni makubwa sana kwa watu wengine kuweza kuhangaika nayo.
SOMA; Sema HAPANA, Hapa Ndio Uhuru Wako Ulipo.
Lakini ukweli ni kwamba unahitaji kuwashirikisha watu wote wanaohusika na biashara yako jambo lolote baya linaloweza kutokea. Kwa nini ni muhimu kufanya hivi?
1. Kadiri tatizo linavyofikiriwa na watu wengi ndivyo nafasi ya kulitatua inakuwa kubwa.
2. Kama tatizo litatokea na kuwa na uhitaji w akufanya mabadiliko kwenye biashara yako, kila mtu ataelewa. Kwa mfano ukahitaji kupunguza wafanyakazi kwa sababu biashara imepata hasara kubwa. Ni rahisi watu kukuelewa kama walikuwa wanajua tatizo tangu awali.
3. Inakupunguzia wewe msongo wa mawazo. Wewe kama mmiliki una mambo mengi ya kufikiria kuhusu biashara yako. Unapotumia muda mwingi kufikiria kuhusu matatizo, utasahau kufikiria njia za kukuza biashara hiyo na hivyo kuongeza matatizo zaidi.
Weka uwazi kwenye biashara yako. Hakikisha kila anayehusika anajua ni nini kinaendelea. Usitake kuja kuwashtukiza watu pale jambo baya linapotokea. Ni heri watu wakajua mapema na hivyo kujiandaa kwa lolote litakalotokea.
Nakutakia kila la kheri kwenye biashara yako.
Kipengele hiki cha BIASHARA LEO kinakupa mbinu muhimu za kutatua changamoto za kibiashara zinazokuzuia kufikia mafanikio makubwa. Pia unajifunza kuepuka makosa unayofanya kwenye biashara yako na yanakuzuia kufanikiwa. Kujifunza mengi zaidi kuhusu mafanikio kwenye maisha jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa kubonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA. Kwa ushauri zaidi wa kibiashara, ikiwepo jinsi ya kupata wazo bora la biashara, jinsi ya kuanza na kukuza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto za biashara piga simu 0717396253.
Jiunge na COACHING/MENTORSHIP PROGRAM ambapo utapata muongozo wa hatua kwa hatua mpaka ufikie mafanikio kwenye kazi au biashara unayofanya. Bonyeza haya maandishi kupata maelekezo ya programu hii.