Mapinduzi ya viwanda yaliyotokea takribani karne mbili zilizopita yalileta mabadiliko makubwa sana kwenye ufanyaji wa kazi. Kabla ya hapo hakukuwa na ajira rasmi na hivyo watu wengi walizalisha kwa kiwango kidogo na kubadilishana. Viwanda vilipokuja viliweza kuzalisha kwa kiwango kikubwa sana na hivyo kuhitaji wafanyakazi wengi. Na kwa kuwa wafanyakazi wengi hawakuwa na ujuzi basi viwanda viligawa majukumu yake katika sehemu ndogo ndogo sana ambapo mtu anafanya kitu kimoja tu.

Kwa mfanyakazi kuajiriwa kufanya kitu kimoja tu ilikuwa faida kwa viwanda kwa sababu kama akiondoka ni rahisi kupata mtu mwingine wa kuziba nafasi yake. Kwa kifupi wafanyakazi walikuwa wanapatikana kirahisi na hivyo gharama zao hazikuwa kubwa. Na hapa ndipo ulipozaliwa utamaduni wa kuwa na wafanyakazi wengi wanaofanya kazi kwa kulipwa mshahara kidogo.

Sasa ni muda umepita tangu mapinduzi ya viwanda kutokea na sasa viwanda havifanyi vizuri kama ilivyokuwa awali. Lakini bado watu wanaendelea kutumia utaratibu ule wa viwanda wa kutafuta wafanyakazi wanaowalipa mshahara kidogo ili wafanye kazi.

Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanaingia kwenye mtego huu pia. Mtu anapotafuta mfanyakazi anaangalia ni mfanyakazi gani ambaye atamlipa mshahara kidogo akiamini kwamba atatengeneza faida kubwa. Unaweza kuamini hivyo ila ukweli ni kinyume na unavyoamini. Kwa kuajiri wafanyakazi ambao unawalipa mshahara kidogo huongezi faida bali unapoteza faida kubwa sana. Leo hapa utaona ni kwa nini na jinsi gani ya kuepuka jambo hili kutokea kwenye biashara yako.

Unapoajiri mfanyakazi ambaye unaweza kumlipa mshahara kidogo na yeye akakubali, kwanza kabisa jua kwamba unaajiri mfanyakazi ambaye hana sifa. Maana kama angekuwa na sifa angeajiriwa sehemu nyingine ambazo zinalipa vizuri. Ila kwa kuwa haajiriki na wewe umeamua kuajiri yeyote anayekubali kuchukua mshahara kidogo basi ndio unakutana naye. Kwa kuajiri mfanyakazi ambaye hana sifa za utendaji mzuri wa kazi ni chanzo kikubwa cha kushindwa kwa biashara yako. Hataweza kutoa huduma bora ambazo unahitaji kutoa ili uweze kuwaridhisha wateja na waendelee kuja kwenye biashara yako.

Tatizo jingine kubwa linalotokana na wewe kulipa mshahara kidogo ni kuwaondolea morali wa kazi wafanyakazi wako. Tuseme labda umepata mfanyakazi ambaye ana sifa nzuri ila imembidi akubali kazi yako ya mshahara kidogo kwa sababu bado hajapata kazi nyingine. Mfanyakazi huyu atafanya kazi ila sio kwa ule ubora wake. Atafanya kazi chini ya kiwango chako na hatojali kama biashara yako inakua au inakufa. Kwa sababu anaona wewe humjali basi na yeye hana haja ya kukujali au kuijali biashara yako.

Kwa njia hizi mbili unajikuta biashara yako inaathirika kwa kiasi kikubwa sana. Unapata wafanyakazi ambao hawana sifa na hivyo unashindwa kutoa bidhaa na huduma nzuri na pia ukipata wenye sifa hawajali biashara yako kwa sababu hata wewe huwajali wao. Wakati wewe unafikiria kwa kulipa mshahara kidogo unaokoa gharama kumbe unazidi kupoteza fedha nyingi kwa sababu unashindwa kutoa huduma bora na hivyo wateja kukukimbia.

Ufanye nini ili usirudishwe nyuma na hili la wafanyakazi?

Kwanza kabisa ajiri wafanyakazi ambao ni bora na wana sifa nzuri. Hakikisha mfanyakazi anaweza kufanya kazi unayompa na pia anaipenda na yupo tayari kuweka juhudi za ziada.

Pili mlipe mfanyakazi huyu bora kipato kizuri ambacho kitamfanya aifurahie kazi yake na awe tayari kuweka juhudi za ziada kwenye kazi hiyo. Hii itamfanya ajali nakuona biashara kama ni yake. Kwa sababu anajua asipofanya hivyo wewe hutopata faida na hivyo utashindwa kumlipa. Na malipo mazuri sio lazima yawe makubwa sana, ila hata kujali kwako kunaleta tofauti kubwa sana kwa maisha ya wafanyakazi wako.

Mara zote huwa nasema mfanyakazi wako ndio mteja wako namba moja, kama utashindwa kumhudumia vizuri atakuwa wa kwanza kufukuza wateja wote wanaokuja kwenye biashara yako. Ajiri wafanyakazi wenye uwezo na jali uwezo wao na wao wenyewe ili nao waweze kukujali wewe na biashara yako.

Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.

TUPO PAMOJA.