Inapokuja kwenye tabia halisi za binadamu huwa napenda kuweka unafiki pembeni. Ni kawaida yangu kuweka unafiki pembeni kwenye mambo yote ya kimaisha, wanafiki hawafanikiwi, hivyo na wewe usijiingize kwenye unafiki.

goodVsEvil

Sawa, sasa tabia ya asili ya binadamu ni ubinafsi, na kupenda kupata zaidi ya wengine. Unahitaji kujitambua kwa kiasi cha juu sana ili uweze kuvuka hilo. La sivyo utaishia kuendeshwa na tabia hizi za asili na mwishowe unaishia kuwa mwizi, au fisadi au kudhulumu wengine. Na wizi ninazozungumzia hapa sio wa fedha tu, bali hata wa muda, wizi wa mapenzi na kadhalika.

Hivi unajua unaweza kuwa fisadi wa mapenzi, kuna watu ambao unatakiwa uwape mapenzi ya dhati lakini unawanyima? (hili ndio nimelifikiria wakati huu naandika hapa, nitaliandikia vizuri siku nyingine)

SOMA; Kutoka Kwenye Kuajiriwa Mpaka Kujiajiri, Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Ili Kununua Uhuru Wako.

Leo nataka nikukumbushe uache kutengeneza maadui wewe mwenyewe. Na maadui hawa wanatokana na tabia za asili za binadamu.

Ukweli ni kwamba utakapofanikiwa, na lazima ufanikiwe kama unasoma hapa na kuyafanyia kazi, kuna watu wengi sana watakaokuchukia. Na wengi wa hao watakao kuchukia wengi watakuwa ni watu wako wa karibu, ndugu zako au marafiki zako. Ndio utaona wakikuchekea na ndio watakusifia sana ila kwa ndani watakuchukia japo hujawafanyia lolote baya.

Kwa nini wakuchukie wakati wewe huna tatizo nao?

Hakuna kitu kinauma kama watu kukuona wewe ulikuwa nao ngazi moja halafu umewacha na kwenda ngazi ya mbali. Hujawahi kusikia huyu tulikuwa tunashinda nae hapa ila siku hizi amepata pesa anaringa. Au siku hizi anajiona yupo matawi ya juu. Nafikiri unanielewa vizuri sana na huenda kuna mtu wako wa karibu ulishamwona amebadilika na kuanza kumwazia hivyo.

Lengo la mimi kuandika kwenye ukurasa wa leo sio kukuambia hayo ambayo tayari unayafahamu, bali kukupa mbinu ya kuepuka kutengeneza maadui wa baadae.

Na mbinu hiyo ni rahisi sana, kila unachofanya kwenye maisha yako, kila unachojifunza washirikishe marafiki zako wa karibu. Kama umesoma makala nzuri kama hii na kuna mazuri uliyojifunza, itume kwa watu wako wa karibu wote, na waambie waisome, waambie kuna mambo umejifunza na ungependa wajifunze pia. Kuna mbinu nzuri unaitumia kufanikiwa kwenye kazi washirikishe, kuna biashara nzuri unaijua washirikishe.

Lakini nawatumia hawasomi, nawapa mbinu hawazifanyi. Sawa usichoke endelea kuwaumia makala nzuri endelea kuwapa mbinu nzuri. Baadae wewe utakapobadilika na kuwa na mafanikio na wao wakabaki pale walipo, hata wakitaka kutengeneza ubaya na wewe nafsi zao sitawasuta na watajikuta wakijisikia vibaya zaidi kwao binafsi.

SOMA; Ushauri; Ni Jinsi Gani Unaweza Kufikia Malengo Yako Kama Una Idadi Kubwa Ya Wategemezi?

Kila siku, naweka maarifa mazuri ya kuboresha maisha kwenye kurasa hizi, soma na watumie wale wa karibu yako, wale ambao mnataka mfanikiwe pamoja, wale ambao unataka mpande nao ngazi kwenye madaraja ya juu zaidi. Usipowatumia na wakaja kukuona mbaya pale utakapokuwa juu zaidi yao, usiwalaumu, kwa sababu hawajui na hawataendelea kujua, kwa sababu wewe unayejua hujataka kuwajulisha.

TAMKO LA LEO;

Nimegundua kwamba nimekuwa najitengenezea maadui wangu wenyewe. Najua kiu yangu ya mabadiliko sio sawa na ya wale walionizunguka. Kuanzia sasa nitawashirikisha watu hawa wa karibu vitu vyote ninavyojifunza na mbinu zote ninazotumia. Watakaofanya sawa na kama hawatafanya sitaacha kuwatumia. Nawapenda watu wangu wa karibu, sitaki mafanikio yangu yanitenge na wao.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.

TUPO PAMOJA.