Kila siku mpya inapoanza, kuna zawadi kubwa na nzuri sana ambayo kila mmoja wetu anapewa. Zawadi hii ina thamani kuliko kitu chochote kuwahi kutokea kwenye maisha yetu.

Zawadi hii tunapewa kwa usawa wote hapa duniani na hakuna anayepunjwa au kusimangwa.

POKEA ZAWADI HII NZURI NA ITUMIE VIZURI.
POKEA ZAWADI HII NZURI NA ITUMIE VIZURI.

Pamoja na zawadi hii kuwa kubwa, ya muhimu na ya thamani bado sio wote tunaipokea kwa usawa, sio wote tunaitumia vizuri, watu wengi wamekuwa wakiitumia vibaya na kuipoteza kabisa.

Pamoja na wengi kuitumia vibaya, bado wanaendelea kupewa zawadi hii. Yaani hata kama unatumia vibaya hii unayopewa leo kesho utapewa zawadi hiyo tena.

Maumivu ya matumizi mabaya ya zawadi unayopewa kila siku hutayaona sasa, bali utayaona baadae ambapo utajiuliza ni nani alikuwa anaiba zawadi zangu?

Leo nataka nikuambie kwamba pokea zawadi hii nzuri kwa moyo mmoja na itumie vizuri. Lakini je umeshaijua zawadi yenyewe? Bado hujajua ni zawadi gani ambayo tunapewa sawa haijalishi ni tajiri au masikini, na hata ukitumia vibaya bado kesho utapewa nyingine na vizuri zaidi huwezi kuichukua zawadi hii kabla, yaani kuikopa?

SOMA; Acha Kujiua Mapema Kabla Ya Muda Wako.

Zawadi tunayozungumzia hapa ni MUDA. Muda ni zawadi ya kipekee kwetu wanadamu. Ni zawadi ambayo tunapewa sawa wote, kila mmoja wetu ana masaa 24 tu kwa siku. Ni zawadi ambayo hata ukipoteza muda leo, bado kesho utapewa tena masaa mengine 24. Na uzuri ni kwamba huwezi kukopa muda, kwamba kwa sababu wa leo haukutoshi, basi unakopa masaa mawili ya kesho umalize mipango ya leo halafu siku yako ya kesho iwe na masaa 22. Haiwezi kutokea hivyo kamwe.

Unapewa zawadi hii kwa kipimo kile kile kila siku na hakuna anayekunyanyasa au kukusimanga kwamba nimekuwa nakupa muda lakini huutumii vizuri. Kila siku unapewa zawadi hii bila ya kujali umekuwa unaitumiaje. Mpaka inafika siku kwamba zawadi hii inafutwa kabisa. Na baada ya hapo inabaki historia utakayokuwa umeandika kwa matumizi yako ya zawadi hii wakati ambapo ulikuwa unaipokea.

Kama kuna jambo moja na la muhimu sana kila mmoja wetu kufanya, basi ni kutumia muda huu tunaopewa vizuri. Tumia muda huu katika kufanya yale mambo ambayo yataboresha maisha yako na ya wanaokuzunguka. Kwa kufanya hivi utaona muda unatosha. Lakini kama utatumia muda huu kwa mambo yasiyo ya msingi, kila siku utaona muda haukutoshi.

TAMKO LA LEO;

Nimejua ya kwamba masaa 24 ninayopewa kila siku ni zawadi kubwa na nzuri sana. Lakini natumiaje masaa haya ni juu yangu mwenyewe. Najua hata kama nitatumia vibaya masaa ya leo, kesho nitapewa mengine tena. Na nitaendelea kupewa zawadi hii mpaka itakapofika siku na ikaondolewa moja kwa moja, ambapo sitaipata tena. Katika wakati huu ndio historia yangu kutokana na nilivyotumia muda wangu itabaki. Nitakuwa makini sana kwenye matumizi yangu ya zawadi hii ambayo ni muhimu sana. Sitaiacha ipotee bure.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.

TUPO PAMOJA.