Kama kuna kazi ngumu duniani basi ni kufikiri, na sio kufikiri tu, bali kufikiri kwa kina.
Binadamu yuko radhi afanye jambo lolote ili tu akwepe zoezi hili la kufikiria.
Lakini utaniambia, mbona mimi muda wote ninafikiria? Mbona mimi muda wote nina mawazo?
Na mimi nitakujibu, ndio unamawazo lakini hufikirii na mawazo hayo ndio unayoyatumia kukwepa kufikiria.

Kwa mfano tuseme labda unapitia matatizo kwenye kazi yako, labda kazi ni nyingi na kipato ni kidogo. Na hivyo unakuwa na mawazo mengi. Na mawazo yenyewe ni kama; hii kazi kwa nini inanitesa, kwa nini mwajiri wangu ananinyonya, hivi kama kipato kitaendelea kuwa kidogo hivi maisha yataendaje, kwa nini nisiandamane kudai kipato zaidi, vipi nikiandamana halafu nikafukuzwa maisha yataendaje na mawazo mengine mengi.
Yote hayo ni mawazo, na yanaweza kuwa yanakuumiza sana, lakini rafiki yangu bado hujafikiri kuhusu tatizo unalopitia. Kufikiri ungeanza kuangalia hali unayopitia na kile unachotaka, kisha unapanga unawezaje kutoka hapo na kwenda pale unapotaka kufika. Kwa mfano utajiuliza kwa nini kazi zangu ni nyingi lakini kipato ni kidogo, ni thamani gani ninayotoa kwenye kazi ninayofanya, nawezaje kuongeza thamani hii sana ili mwajiri wangu anione ni mtu muhimu na hivyo kuniongezea kipato. Haya ni maswali ambayo yataleta fikra zitakazokupelekea wewe kuboresha hali unayopitia.
SOMA; Hawa Ndio Watu Unaotakiwa Kuwafikiria Zaidi.
Huu ni mfano mmoja tu kwenye eneo moja. Lakini hivi ndivyo ilivyo kwenye biashara, na hata maisha kwa ujumla/ labda una changamoto za kifamilia, badala ya kuwa na mawazo kwamba unateswa na kunyanyaswa, fikiria ni jinsi gani unaweza kuboresha hali hiyo ya kifamilia.
Maisha bora yanaanza na fikra sahihi, usijiumize na mawazo na fikiria kile unachofikiria. Je kinakupeleka kwenye kutatua tatizo au kinakuongezea msongo ulionao kwenye tatizo? Kila mara fikiria hivi ili ujikamate pale unapojaribu kutoroka kazi ngumu ya kufikiri.
TAMKO LA LEO;
Nimejua ya kwamba kuwa na mawazo ni tofauti kabisa na kufikiri. Najua kufikiri ni kazi ngumu na ambayo inalipa vizuri. Pia nimejua ya kwamba mara nyingi nimekuwa natoroka kazi hii ya kufikiri kwa kujiingiza kwenye mawazo ambayo hayawezi kunisaidia. Kuanzia sasa nitakuwa nafikiri kile ambacho nafikiri ili kuhakikisha mara zote natengeneza suluhisho la changamoto mbalimbali ninazopitia.
Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.
Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.
Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.
Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.
TUPO PAMOJA.