Sisi binadamu ni viumbe wa kuhukumu.

Tuna majibu ya kila kitu.

Na majibu haya tunajitengenezea ndani ya vichwa vyetu.

Tukiamini kwamba kwa namna moja au nyingine sisi ni bora zaidi ya wengine kwenye mambo fulani.

Au tukiamini sisi tuko hovyo zaidi ya wengine katika maeneo fulani.

KILA MTU UNAYEKUTANA NAYE AMEBEBA MATATIZO YAKE, USIHUKUMU.
KILA MTU UNAYEKUTANA NAYE AMEBEBA MATATIZO YAKE, USIHUKUMU.

Ni kweli binadamu tunatofautiana, lakini wote tunapitia changamoto ambazo hazitofautiani sana.

Kila mtu ana matatizo yake, ambayo sio mabaya au hovyo kuliko ambayo unayo wewe.

SOMA; Matatizo Yote Ya Mahusiano Yanaanzia Hapa… Sehemu Ya Pili(2)

Hii inatukumbusha nini sasa?

Inatukumbusha tusihukumu. Haijalishi mtu amefanya maamuzi gani, hatuna haki ya kuhukumu.

Kwa sababu maamuzi mengi ambayo watu wanafanya ni kulingana na matatizo waliyonayo.

Watu wengi wanafanya maamuzi kutokana na hisia zinazowatawala katika wakati huo wa maamuzi. Na hisia kubwa mbili zinazoendesha watu ni hofu na upendo.

Maamuzi yoyote ambayo mtu anafanya, jua anaendeshwa na hisia za hofu, kwamba kuna kitu anapoteza, au hisia za upendo kwamba kuna kitu anapata. Inategemea ni hisia zipi zimemtawala mtu.

Kama utataka kufanya maamuzi bora kwako na kwa wengine, jitahidi mara zote utawaliwe na hisia za upendo. Maisha yatakuwa rahisi na bora sana kwako.

Unaweza kufanya kazi au biashara kwa sababu unaogopa kama utakosa fedha maisha yako yatakuwa magumu sana. Na hivyo kufanya kazi ile ili tu usifukuzwe au ili tu mteja asiache kufanya biashara na wewe. Na pia unaweza kufanya kazi au biashara kwa sababu ndio kitu unachopenda kufanya, ndio mchango mkubwa ambao unapenda kutoa kwa watu wanaokuja kwenye kazi au biashara yako. Kuna tofauti kubwa sana kati ya hali hizi mbili, moja inajenga hofu zaidi na uhaba na nyingine inaleta furaha na mafanikio.

Jitahidi mara zote uendeshwe na hisia za upendo, pale hofu inapokuingia usipigane nayo, bali fikiria ni kitu gani ungependa kutoa kwa watu zaidi. Usijiangalie wewe tu, angalia wengine wanaweza kunufaikaje, na mwisho wa siku hofu itajijali yenyewe huku wewe ukiendelea kufanya kilicho bora.

TAMKO LA LEO;

Nimejua ya kwamba kila binadamu anapitia matatizo ambayo hayatofautiani sana na wengine. Na pia kila mtu anafanya maamuzi kwa kuongozwa na hisia mbili kubwa, hisia ya hofu na hisia ya upendo. Hisia za hofu zinaleta uhaba na hofu zaidi na hisia za upendo zinaleta furaha na mafanikio. Licha ya matatizo ninayopitia kwenye maisha yangu, nitajitahidi nifanye maamuzi yangu kwa kuongozwa na hisia za upendo.

Tukutane kwenye ukurasa wa kesho, Like page yangu ya Coach Makirita Amani uendelee kupata mambo mazuri ya kuboresha kazi yako, biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Pia usiache kutembelea mtandao huu kila siku kujifunza mambo mapya na mazuri. Kusoma makala zilizopita za KURASA 365 ZA MWAKA 2015 bonyeza hayo maandishi.

Pia washirikishe wengine makala hii kwa kubonyeza vitufe vya facebook au twitter hapo chini. Pia watumie makala hii nzuri kwa njia ya email.

Kwa lolote andika email kwenda makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kujifunza zaidi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa jiunge na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi kupata utaratibu.

TUPO PAMOJA.