Zama hizi tunazoishi kila mtu ana maoni.

Na kila mtu ana maoni kuhusu jambo lolote.

Na kila mtu anaweza kutoa maoni yake juu ya jambo lolote bila ya kujali maoni yake ni mazuri au mabaya.

Na kusema ni rahisi sana, hasa kama huhusiki kwenye utendaji.

Ni kitu kizuri kwa watu kuwa na maoni, ila pia kunakuja na gharama kubwa.

MAONI

Watu wengi wameshindwa kufanya mambo makubwa kwenye maisha yao kutokana na maoni ya wengine.

Labda ulipanga kufungua biashara fulani, ukawauliza watu wako wa karibu, na wakakupa maoni yao. Ukaacha hukufungua.

Tatizo kubwa ni kwamba maoni sio ukweli, maoni sio uhalisia, maoni ni hisia za mtu tu anavyoamua kusema kuhusiana na kitu fulani na mara nyingi yanaendeshwa na hofu zake.

Watu sio kwamba wanafanya utafiti wa kina halafu ndio wanatoa maoni, wao wanaangalia hisia zao kisha wanatoa maoni yao, na kulingana na hisia walizonazo, maoni yanaweza kuwa mazuri au mabaya.

SOMA; Sikiliza Hawa Watu Wanaokupa Mawazo Ya Biashara Kila Siku.

Sasa haijalishi maoni wengine wametoa ni mazuri au mabaya, yasikuzuie wewe kuiendea ndoto zako.

Leo nakutangazia kwamba maoni yoyote ambayo mtu yeyote atayatoa kwenye ndoto yako kubwa kwenye maisha ni kelele, usisikilize hata kidogo. Tumia muda huo kupambana kufikia ndoto yako kubwa na sio kuanza kufikiria watu wanasemaje kuhusiana na ndoto hiyo.

Usikubali ndoto yako izimwe na maoni ya mtu anayeendeshwa na hisia za hofu au upendo. Weka juhudi kwenye ndoto yako, na utapata unachotafuta.

TAMKO LA LEO;

Najua kitu chochote ambacho ninafanya, lazima kuna watu watakuja na maoni yao. Kwenye ndoto yangu kubwa ya maisha, sitaruhusu maoni ya mtu yeyote yaingilie ndoto yangu hii. Nitaendelea kufanyia kazi ndoto yangu kwa sababu najua maoni ya wengine hayana nafasi yoyote, ni kelele tu.

NENO LA LEO.

“If someone isn’t what others want them to be, the others become angry. Everyone seems to have a clear idea of how other people should lead their lives, but none about his or her own.”
― Paulo Coelho

Kama mtu hayupo kama vile watu wengine wanavyotaka awe, watu wanachukia. Kila mtu anaonekana kuwa na mawazo mazuri sana ni jinsi gani watu wengine waishi maisha yao lakini hawana mawazo ya jinsi gani ya wao wenyewe kuishi maisha yao.

 

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.