Moja ya sababu kubwa nakusisitiza sana sana na tena sana kuwa bora ni kwa sababu maisha hayasimami. Chochote unachofanya kwenye maisha yako, hakikuachi hapo ulipo, kinakufanya kuwa bora zaidi au kuwa hovyo zaidi.

Hata kama hufanyi chochote, bado hubaki hivyo ulivyo, bali maisha yako yanakuwa hovyo zaidi.

Unakua au unakufa, na hakuna hali ya katikati.

UMECHAGUA KUKUA AU UMECHAGUA KUFA?
UMECHAGUA KUKUA AU UMECHAGUA KUFA?

Ukiamua kuyapeleka maisha yaende tu kadiri mambo yanavyokwenda, unayafanya kuwa hovyo na hatimaye kufa.

Ukiamua kutengeneza maisha ya tofauti, yanayoendana na wewe ambapo unatoa mchango mkubwa kwa wengine unaendelea kukua na kuwa bora zaidi. Na hata utakapoondoka hapa duniani, kazi zako zitainufaisha dunia.

Hakuna kusimama, hakuna katikati, ni unakuwa bora au unakuwa hovyo.

SOMA; Ishi kwa misingi hii nane na maisha yako yatakuwa bora sana.

Na sababu kubwa inayofanya kusiwe na kusimama ni kwamba dunia inaendelea kwenda. Dunia haijali wewe unafanya nini, dunia haijali wewe unasubiri nini. Dunia inazidi kusonga mbele, dunia inazidi kubadilika. Hivyo kama wewe huwezi kwenda na dunia ninavyokwenda, unaachwa nyuma, unakuwa hovyo.

Kila siku unapoamka asubuhi una nafasi ya kuchagua, leo naenda kuwa bora au leo naenda kuwa hovyo. Kuweka msisitizo zaidi kila unapoamka jiambie kwa sauti kabisa, LEO NAENDA KUWA BORA ZAIDI, au LEO NAENDA KUWA HOVYO ZAIDI. Halafu usidanganye, maana utakuwa unajidanganya mwenyewe.

TAMKO LANGU;

Najua maisha yangu hayana hali ya kati kati, ni kwamba nakuwa bora au nakua hovyo, ni kwamba naenda mbele au narudi nyuma. Kuanzia sasa nachagua kuwa bora, nachagua kusonga mbele. Kila siku nitakapoamka nitafanya uchaguzi huu muhimu sana wa kwenda kuwa bora zaidi siku hiyo zaidi ya ambavyo nimewahi kuwa kwenye maisha yangu.

NENO LA LEO.

“In this world you’re either growing or you’re dying so get in motion and grow.”

― Lou Holtz

Kwenye dunia hii ni labda unakua au unakufa, hivyo fanya mambo yatakayokufanya ukue.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.