Kila mmoja wetu yupo kwenye jukumu kubwa la kutatua matatizo ya dunia. Kila mmoja wetu kupitia kazi au biashara anayofanya napenda kuona dunia ikiwa sehemu nzuri ya watu kuishi.

Lakini kuna watu ambao wanafanikiwa kwenye hili na kuna wengine hawafanikiwi. Kuna ambao kweli wanaweza kutatua matatizo haya ya dunia hata kama ni kwa kidogo. Na kuna wengi ambao wanashindwa kabisa kutatua matatizo hayo ya dunia.
Kuna kitu kimoja muhimu sana unachohitaji kufanya kabla hata hujafikiria kwenda kutatua matatizo ya dunia. Kitu hiki ni wewe kutatua kwanza matatizo yako na nafsi yako.
Kila mmoja wetu katika kipindi fulani anapitia wakati ambao anakuwa na mgogoro na nafsi yake. Unafanya kitu lakini unakuwa unajiuliza je hiki ndio muhimu kwangu kufanya, je kitanifikisha wapi, mbona wengine wanafanya vizuri kuliko mimi? Na mengine mengi.
SOMA; Ni Lipi Dhumuni Lako Kwenye Maisha? Langu Ni Hili Hapa.
Mgogoro kama huu ni mkubwa sana na usiuchukulie kirahisi. Bila kumaliza mgogoro huu hutaweza kufanya jambo lolote kubwa. Unahitaji kutatua mgogoro huu, kuwa na amani na nafsi yako, kwa kujua dhumuni lako hapa duniani ni nini na kukubali kulifanya bila ya kuangalia nyuma au kuangalia wengine wanafanya au kusema nini.
Ukishalijua dhumuni lako, na kukubaliana na nafsi yako kwamba hiki ndio utakachofanya, utakuwa umeshinda mtihani mkubwa sana na hapo unakuwa tayari kutatua matatizo ya dunia. Utafanya chochote unachofanya kwa kujiamini na watu watakuamini pia.
Hakikisha unafanya makubaliano na nafsi yako, hakikisha una amani nafsi yako na kile unachofanya kinatoka kweli ndani yako.
TAMKO LANGU;
Najua ya kwamba kabla sijaweza kutatua matatizo ya dunia, ninahitaji kutatua matatizo yangu kwanza. Nahitaji kukubaliana na nafsi yangu juu ya kile ambacho ninafanya. Nahitaji kuwa na imani kwamba hiki ndio kitu nimechagua kufanya na sitarudi nyuma kwa sababu yoyote ile.
NENO LA LEO.
“Your purpose in life is to find your purpose and give your whole heart and soul to it”
― Gautama Buddha
Jukumu lako kubwa kwenye maisha ni kujua dhumuni la maisha yako na kuweka moyo wako wote na nafsi yako kwenye kufikia dhumuni hilo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.