Nafikiri kama umekuwa unanisoma kwa muda mrefu utakuwa unajiua kabisa ya kwamba mimi ni mwinjilisti mzuri sana wa mafanikio.
Yaani kila ninachozungumza, kila ninachoandika ni kuhusu mafanikio, kuhusu kuwa bora leo zaidi ya ulivyokuwa jana, kuhusu kwenda hatua ya ziada, kuhusu kutoa zaidi ya ulivyotegemewa kutoa.
Huu ndio wimbo ambao nimekuwa nakuimbia na nitaendelea kukuimbia kwa sababu najua haijalishi umefikia hatua gani sasa au hata siku zijazo, bado unaweza kuwa bora zaidi, bado unahitaji kwenda mbali zaidi. Wale ambao wanafikia hatua fulani na kuridhika kwamba wao ndio wao hao hawajui wanakokwenda.
Leo nataka nikushirikishe kwa nini nahubiri sana mafanikio na sio fedha. Kwa sababu kuna watu wanakuambia kama tatizo ni kuwa na maisha bora si niwe na fedha tu, maana fedha ndio dawa ya kila kitu? Ni kweli kabisa kwamba fedha ni dawa ya kila kitu kasoro kimoja tu, nafsi yako wewe.
Iko hivi kama unaanza na huna fedha, utaona fedha ndio kila kitu. Ila kadiri unavyopata fedha, kuna kiwango utafikia na hata fedha ziongezeke kiasi gani huoni tena tofauti. Yaani kwa sasa kama ndio unakazana kupata fedha, kadiri unavyopata fedha nyingi utakuwa na furaha, ila kuna kiwango ukifikia hata fedha iongezeke kiasi gani, furaha haiongezeki tena, inakuwa ni kitu cha kawaida kwako sasa. Na hapa ndipo utakapoteseka sana kama kilichokuwa kinakusukuma ni fedha tu.
Hii ni kwa sababu utajikuta unaona huna tena mchango mkubwa kwako na hata kwa wanaokuzunguka.
Hivyo lengo lako kubwa liwe mafanikio, kuwa bora zaidi kadiri siku zinavyokwenda. Na kwenye maeneo yote ya maisha yako, kuanzia kazi au biashara unayofanya, fedha, familia na kila kitu.
SOMA; Maisha Yako Yanaweza Kuwa Bora Zaidi, Anza Hivi….
Unapokazana kuwa bora kila siku, hata utakapokuwa na fedha nyingi kiasi gani, bado utaendelea kuyafurahia maisha kwa sababu unaendelea kuvuka changamoto mbalimbali kwenye safari yako ya ubora. Na kwa sababu unajua hakuna siku utafika useme wewe ndio umeshafika mwisho, hivyo hata uwe na fedha nyingi kiasi gani, bado utaendelea kufanya kwa ubora kile ambacho kimekuletea fedha ulizonazo.
Na hapa mafanikio yako yatakuwa ni ya kudumu. Tumeelewana sasa?
TAMKO LANGU;
Ninajua safari ya mafanikio niliyoanza ni safari ya kudumu. Safari hii haina kituo cha kushuka. Hii ni safari inayoendelea kila siku mpaka pale nitakapoondoka kwenye dunia hii. Hivyo nimejiandaa vya kutosha nakila siku nitahakikisha nakuwa bora zaidi ya siku iliyopita. Mimi ni mwana mafanikio ya kweli, na mafanikio ni sehemu muhimu ya maisha yangu kwenye kitu chochote ninachofanya.
NENO LA LEO.
“After you reach a certain point, money becomes unimportant.
What matters is success.”
Aristotle Onassis
Baada ya kufikia kiwango fulani, fedha inaacha kuwa muhimu. Kinachokuwa muhimu ni mafanikio.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.
