Maisha ni maigizo.

Ukienda kwenye msiba, hata kama mtu sio wa karibu kwako, ni lazima utakuwa na huzuni. Hata kama una furaha kiasi gani siku hiyo, utaiweka furaha yako pembeni na kuvaa uhusika wa msiba, ukitoka hapo unaweza kurudi kwenye furaha yako. kama haya sio maigizo ni nini?

Hata kama umekasirishwa au una hasira kiasi gani, ukipewa mtoto mchanga umshike, ni lazima utaanza kumchekea. Utaonesha furaha kubwa kwa kitoto hiko na kujaribu kumchekesha chekesha. Unaweza kuendelea na hasira zako baadae ila kwa sasa wakati uko na mtoto, utaonesha furaha. Je hili sio igizo?

JIONE VILE AMBAVYO UNGETAKA KUWA, NA ISHI VILE AMBAVYO UNGETAKA KUWA.
JIONE VILE AMBAVYO UNGETAKA KUWA, NA ISHI VILE AMBAVYO UNGETAKA KUWA.

Maisha ni maigizo na kila kitu tunachofanya kwenye maisha yetu tunaanza kwa kuigiza baadae kinakuwa sehemu ya maisha yetu.

Na katika maigizo haya, watu wote tumegawanyika katika makundi mawili.

Kundi la kwanza ni wale ambao wanaigiza kile ambacho wanakitaka kweli. Unaamua ni nini unataka kwenye maisha yako halafu unakiigiza mpaka unakipata. Watu waliopo kwenye kundi hili wanakuwa na maisha mazuri na yenye mafanikio.

Kundi la pili ni wale watu ambao wanaigiza maigizo ya watu wengine. Hawajui ni kitu gani hasa wanataka, ila wanaangalia wengine wanafanya nini na wao wanaigiza. Watu waliopo kwenye kundi hili wanakuwa na maisha mabovu ya kubadilibadili maigizo na kutokujua ni wapi wanakwenda.

SOMA; KUJIAMINI; Jinsi Ya Kujijengea Tabia Ya Kujiamini.

Kama unataka kuwa na maisha bora, kama unataka kufika mbali zaidi ya ulipo sasa, jua ni nini unataka kwenye maisha yako, na anza kuigiza kitu hiko. Anza kufanya kile ambacho waliofanikiwa kwenye eneo hilo wanafanya. Anza kubadili tabia ulizonazo ambazo zinakuzuia kufika huko. Na kuwa tayari kukutana na vikwazo na kuvivuka. Kama utaweza kuigiza hivi kwa muda mrefu, ni lazima utakutana na mafanikio, tena makubwa.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba maisha ni maigizo na kila tunachofanya kwenye maisha tunaanza kwa kuigiza. Hata kufikia mafanikio makubwa, kunaanza kama igizo, kwa kujua ni wapi ninapotaka kwenda, kujua tabia zitakazonifikisha pale na kuanza kuziigiza. Pia najua ninahitaji kuigiza kile ambacho kitanifikisha ninapotaka kwenda na sio kuigiza tu kwa sababu wengine wanafanya hivyo.

NENO LA LEO.

“You must be the person you have never had the courage to be. Gradually, you will discover that you are that person, but until you can see this clearly, you must pretend and invent.”
― Paulo Coelho

Ni lazima uwe mtu ambaye hujawahi kuwa na ujasiri wa kuwa hivyo. Baada ya muda utajikuta umeshakuwa mtu unayetaka kuwa, lakini kabla hili halijatokea, ni lazima uigize kuwa mtu wa aina hiyo.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.