Watu wengi wanapofanya jambo fulani wanafurahi na kujisikia vizuri pale wanapokubalika na jamii katika yale wanayoyafanya. Wengi hupata sababu ya kuendelea zaidi na zaidi na hata kuweza kufanikiwa zaidi kwa kuwa tu wapo wengi wanaokubali kile wanafanya, hivyo hawa wanaendelea tu kwa kuwa wapo wanaowakubali kwa kazi/shughuli zao. Lakini mambo yanapoenda kinyume, pale ambapo watu hawa watakutana na watu wenye mtazamo hasi, wasioelewa au kukubali kile wanafanya , basi huo unaweza kuwa ndio mwisho wao, wanaweza wasiendelee tena, wanakosa sababu ya kuendelea tena, maana wao nguvu ya kuendelea kufanya kile wanafanya ilikuwa inatoka nje. Hawana msukumo wa ndani wa kuwafanya wafanye kile.

JICHAGUE MWENYEWE, AMINI UNAWEZA NA FANYA.

 
Kuna wengine wao wenyewe wanafanya kile wanasikia ndani mwao kuwa ni sahihi kufanya na wanafurahia kufanya, hawa hawahitaji mtu wa nje kuwapongeza au kuwasifikia na kuwakubali ili waendelee. Naweza sema hawa ni watu ambao wanajitambua, wanajua kwa nini wanafanya kile wanafanya, na wao wanafanya tu haijalishi ni watu wangapi wanawaelewa au kuwakubali kwa wakati huo, hawaruhusu chochote kuwazuia kuendelea na safari yao, hawaruhusu kikwazo chochote kushinda ndani mwao, wana uhakika wa kufika mwisho wa safari maana wanajua wanakoenda, wanajua wanachofanya, hawabahatishi hawa. Huyu hata akutane na changamoto gani , atasonga tu, changamoto zinakuwa ni ngazi za kumsaidia kufika kule anaenda, inakuwa ni darasa, changamoto hazichukuliwi kama vikwazo bali zinachukuliwa kama njia ya kufika kule anaenda, mtu huyu anafurahia hata anapopingwa au hata kuambiwa kile asichopenda kusikia, maana inamsaidia pia kujitathmini na hata kuangalia kama ipo sehemu ya kurekebisha, lipo la kujifunza au ni kupuuzia tu.
SOMA; Jambo Moja Muhimu Unalotakiwa Kujua Kuhusu Miasha Na Kulitumia Kila Siku Ili Kufanikiwa.
Mtu anayejitambua ni rahisi kwake kufika mwisho wa safari kwa maana anajielewa, anaelewa anachofanya, ana sababu za msingi za kumfanya afanye anachofanya, huyu pengine anakuwa anajua au anategemea kuwa atakutana na changamoto za aina fulani katika safari hiyo na anakuwa yu tayari kukabiliana nazo bila kukata tama au kurudi nyuma. Mtu anayejitambua hata ikitokea akakutana na watu wanaompinga hawezi kuwachukia wanaompinga, maana huyu atakuwa anaweza hata kutofautisha kati ya mtu na hoja , kati ya mtu na kile kinapingwa, anaweza kuelewa kirahisi kuwa huyu mtu ananipinga mimi au kile ninachofanya, na kwa kufanya hivyo inakuwa ni rahisi kujifunza vipya na hata namna ya kushirikiana na watu inakuwa ni rahisi zaidi.
Mtu asiyejielewa na kujitambua huyu ana shughuli nzito, kutokujitambua ni tatizo kubwa sana na linaweza kukufanya ukamchukia na kumlaumu kila mtu, maana si haujielewi, hujui wewe ni nani, inakuwa rahisi kwako au niseme inakufanya ujisikie vizuri pale unapowalaumu wengine au kuhamishia lawama kwa wengine hata kwa vitu ambavyo unalo ambalo ungeweza kufanya na mambo yakawa sawa tu kwa nafasi yako.
SOMA; Mambo Mawili Muhimu Unayotakiwa Kujua Kuhusu Maisha
Katika maisha haya hakikisha kwamba unajielewa wewe ni nani, ili uweze kuwa mtu huyo, kama haujielewi ni rahisi kutamani kuwa kama mtu fulani kwa kuwa kuna vitu vinakufurahisha kwa mtu yule, pengine unatamani kwa kuwa upande wa mtu yule uliobahatika kuufahamu kwa mtu ule unapendeza, ni mzuri hauna vitu vibaya ndio maana unatamani na kupenda hivyo, lakini je unamfahamu vyema huyo unayetamani kuwa kama yeye? Ndugu yangu nawe unavyo vitu ambavyo kuna mtu mahali anatamani angeumbwa kama wewe na kufanya kama wewe, una uwezo mkubwa sana ndani yako wa kufanya mambo mengi na makubwa hapa duniani ambayo hakuna mwingine zaidi yako anaweza kuyafanya, INUKA, JIAMINI. Hata kama hakuna anayekuelewa au kukubali leo, wewe fanya kile unafanya na unafurahia kukifanya , tambua wengine ni akina Tomaso mpaka waone matunda ya kile unafanya ndio wakukubali, au kwa kuwa nao hawajitambui hivyo hawaelewi hicho unafanya pengine nao ni mpaka waone mtu fulani labda maarufu amekukubali ndio nao wakukubali. Hivyo ili mradi wewe ndani mwako una uhakika kuwa hicho ni kitu sahihi kwako na kinakupa ile amani ya ndani ya kweli kabisa, endelea kufanya usiruhusu lolote likuzuie kufikia malengo yako ndugu yangu. UNA NGUVU NA UWEZA mkubwa sana ndani mwako.
Makala imeandikwa na Beatrice Mwaijengo
+255755350772