Habari za leo rafiki?
Unaendeleaje? Nina imani harakati zako za kuboresha maisha yako na ya wale ambao wanakuzunguka zinaendelea vizuri sana. Hongera kwa hilo.
Karibu tena kwenye mazungumzo yetu haya ya leo, tuendelee kupeana maarifa na mbinu za kuboresha maisha yetu. Kumbuka hakuna kilele cha ubora, kila siku kwenye maisha yako kuna eneo unaloweza kuboresha, hata kama upo juu kiasi gani. Safari hii uliyochagua, ya kuiwa bora haina mwisho, ndio maana kila siku tupo pamoja katika kushirikishana maarifa haya muhimu.
Kitu kimoja ambacho nimejifunza kwenye maisha ni kwamba kila mmoja wetu bado anakua. Ndio haijalishi una miaka 27 au 57, bado tunakua, kila siku. Kadiri siku zinavyokwenda tunajifunza vitu vipya ambavyo hatukuvijua hapo awali, au tulikuwa tukijua tofauti na tunavyojua sasa.
Hivyo kila siku tunakua, leo unaweza kuwa unajua hivi na kuamini hivi lakini kesho ukapata maarifa yanayoonesha kwamba ulichokuwa unajua sio sahihi, na ulichokuwa unaamini sio sahihi.
Sasa inapofikia hali kama hii kuna watu wengi sana wamekuwa wakiumia na kuona ni kama wanavunja misimamo yao wenyewe. Hasa wale ambao umri umekwenda, na utaratibu wa jamii zetu kwamba mkubwa hakosei unawafanya watu wengi kushindwa kuwa na maisha bora.
Leo nataka tulijadili hili ili tunapomaliza hapa uondoke ukiwa na mawazo tofauti na ya kuboresha maisha yako kabisa.
Wiki iliyopita nilikuwa nawasiliana na mmoja wa marafiki zangu ambao hatujawasiliana kwa muda mrefu. Kuna kitu aliniuliza nikamjibu, na akabaki kushangaa, akaniuliza umebadilika lini wewe, si ulikuwa tofauti kabisa na hilo? Nilimjibu ndio, lakini nimejifunza mengi na nimeona nilichokuwa naamini mwanzo sio.
Hakuna mtu ambaye hajawahi kuamini kitu ambacho sio cha kweli, hakuna mtu ambaye hakui, hii ni kawaida kwa binadamu na duniani kote.
Wakati wa utawala wa roma, ilikubaliwa kwamba dunia sio duara kama tunavyoamini sasa, walisema dunia iko flat na pia walikubaliana kwamba jua ndio linazunguka dunia, na sio dunia kuzunguka jua kama tunavyoamini sasa. Walijitokeza watu waliofanya majaribio na kuja na matokeo tofauti kwamba dunia ni duara na dunia ndio inazunguka jua, walikataliwa na mbaya zaidi walinyongwa kwa kupotosha uma. Lakini baadae ilikubalika ni kweli imani ya kwanza ilikuwa uongo.
Kwa miaka mingi ilikuwa inaaminiwa kwamba vidonda vya tumbo vinasababishwa na kula pilipili au vitu vichachu. Na watu waliamini hili, na kujihadhari na vitu hivyo. Ila baadae imekuja kugundulika vitu hivyo sio chanzo bali ukishapata vidonda vya tumbo ambavyo vinasababishwa na vitu vingine, kutumia vitu vichachu kunachochea zile dalili.
Kwa nini nakuambia yote hayo?
Kwa sababu nataka upate picha kwamba sio wewe mwenyewe ambaye unakuwa na imani ambayo inabidi baadae ubadili.
Chochote unachojua na kuamini sasa, ni kutokana na maarifa ambayo mpaka sasa unayo. Siku zijazo, unaweza kupata maarifa bora sana na kujikuta inakubidi kuwa na imani tofauti.
Jipe nafasi ya kukua kila siku, jipe nafasi ya kubadili mawazo yako kila siku.
Ila usibadili mawazo kwa kufanya kitu ambacho kinakwenda kinyume na misingi yako ya uadilifu na uaminifu, na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.
Leo ondoka na hili kwamba unachojua na kuamini leo ni kutokana na maarifa ambayo unayo mpaka sasa, au kutokana na ulivyokuta wengine wanaamini hivyo. Jua kabisa utakapopata maarifa mengi zaidi yanayoonesha ushahidi wa tofauti unaweza kubadili kile unachoamini sasa. Ubora wa maisha yako sio kung’ang’ana na ambacho hakifai kwa sababu tu uliamini hivyo awali, bali kuangalia kipi ni bora na kukifanya.
Jipe ruhusa ya kukua, bila ya kujali umri wako wa sasa ni mkubwa au mdogo kiasi gani. Jipe ruhusa ya kubadili mawazo, bila ya kujali kwa sasa una mawazo gani au una imani gani.
Unataka uchokozi zaidi kwenye kile unachoamini au kufanya?
Anza kuhoji kila kitu, yaani kila kitu unachoamini au kufanya sasa, anza kukihoji. Jiulize je hiyo ni kweli au ndio ulivyozoea. Kama ukijihoji vizuri na kuanza kutafuta maarifa zaidi, utajikuta unapata mwanga mkubwa sana. Uwe na kifua lakini, maana kuna vitu vingine utavijua ambavyo hukutaka kuvijua.
Una haki ya kuwa na maisha bora, na hakuna anayekufunga kuendelea kuamini kile ulikuwa unaamini awali. Maisha ni yako, chaguo ni lako. Chagua kuwa na maisha bora.
Nakutakia kila la kheri katika kuboresha maisha yako, kwa kujihoji kwa kila unachofanya.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
MAKALA ZA KUSOMA;
Bonyeza kufungua ili usome.
1. Sababu Tano Kwa Nini Biashara Nyingi Zinazoendeshwa Na Waajiriwa Huwa Zinakufa.
2. Chanzo Kikuu Cha Kuona Maisha Yako Ni Mabaya.
3. Mwongozo Wa Kufanya Biashara Ukiwa Bado Umeajiriwa. Mambo Muhimu Ya Kuzingatia.