Karibu tena kwenye kona yetu hii ya mjasiriamali ambapo tunajifunza mambo muhimu kuhusu biashara na ujasiriamali. Kupitia kona hii unapata mbinu mbalimbali za kuiwezesha biashara yako kwenda vizuri na wewe kufikia malengo yako ya kibiashara. Kama wote tunavyojua biashara zina changamoto nyingi. Kabla hujaingia kwenye biashara unaweza kuwa na mipango mizuri sana, lakini unapoanza biashara unakutana na changamoto nyingi ambazo hukufikiria kama ungekutana nazo.
Kutokana na changamoto hizi kuna baadhi ya biashara zinamudu na biashara nyingine zinashindwa na hivyo kufa. Na biashara zinazokufa au kushindwa kukua ni nyingi kuliko zile ambazo zinapona changamoto hizi na kukua zaidi. Kwa wafanyabiashara wengi ambao biashara zao zinakuwa zimeshindwa huwa wanakuwa na sababu nzuri na zinazoonekana ni za kweli kwa nini biashara zao zimekufa. Na mara zote sababu hizo huwa ni za nje ya biashara.
Wafanyabiashara wengi huona kufa kwa biashara zao ni kwa sababu ambazo zipo nje ya uwezo wao au nje ya biashara. Kwamba wao walifanya kila jitihada lakini hawakuweza. Baadhi ya sababu za nje ya biashara ambazo zimekuwa zikitumiwa sana kama chanzo cha biashara kufa ni kama zifuatazo; hali ngumu ya uchumi, kuongezeka kwa ushindani, mabadiliko ya hali ya hewa, mabadiliko ya sera za utawala, mabadiliko ya biashara nyingine na mengine mengi.
Lakini sababu hizi sio chanzo halisi cha biashara kufa, bali hizi zinachangia biashara kufa. Maana yake kuna sababu kuu ambazo zipo kwenye biashara ambazo zinapokutana na changamoto hizi za kawaida kwenye biashara yoyote, biashara inashindwa. Ingelikuwa sababu za nje ndio zinazopelekea biashara kufa, basi tungetegemea biashara zote kufa wakati zinapitia hali ngumu. Badala yake baadhi ya biashara zinafanya vizuri sana wakati ambao ni mgumu. Hata wakati ambao uchumi ni mbovu na watu wengi hawanunui, kuna biashara ambazo zinafanya vizuri sana.
Hivyo biashara yako inapokufa au inapoelekea kufa, badala ya kuangalia sababu za nje za biashara hiyo kufa, hebu anza kuangalia sababu za ndani ambazo zinaifanya biashara hiyo kuwa rahisi kutikiswa na sababu za nje. Na ili uweze kujua na kufanya maamuzi mazuri hapa tutajadili baadhi ya sababu za ndani za biashara kufa;
1. Usimamizi mbovu.
Katika kila biashara inayokufa, hiki ni kitu namba moja. Usimamizi mbovu unachagia sana biashara kushindwa kuhimili nyakati ngumu na hivyo kufa. Usimamizi huu mbovu unatokana na mfanyabiashara au kiongozi wa biashara kutokuwa na maarifa bora ya kuendesha biashara au kuendesha biashara kwa mazoea. Kwa njia hii biashara inakuwa na udhaifu mkubwa sana kiasi kwamba zikitokea changamoto zinaleta athari kubwa sana kwenye biashara hiyo.
2. Mipango na matumizi mabaya ya fedha.
Fedha ndio damu ya biashara na popote unapoona biashara inakufa, jua damu ya biashara inavuja, maana yake biashara inapoteza fedha. Biashara inaweza kupoteza fedha kutokana na mipango mibovu ya fedha au matumizi mabaya ya fedha hizo.
Mipango mibovu ni pale mpangilio wa mtaji kwenye biashara hauendani na hali halisi ya biashara. Kwa mfano wakati ambao biashara ni ngumu ni vyema mtaji ukawekwa zaidi kwenye yale maeneo ya biashara ambayo yanafanya vizuri. Kuendelea kugawanya mtaji kwa usawa kwenye kila eneo la biashara, ni kuruhusu hali hii mbaya kuiathiri sana biashara yako.
Matumizi mabaya ya fedha ni pale fedha ya mtaji wa biashara inapotumia kwa shughuli nyingine ambazo hazihusiani na biashara. Au mfanyabiashara na wafanyakazi wake kukosa uaminifu na kuchukua fedha kwenye biashara kwa mambo yao binafsi. katika nyakati ngumu matumizi kama haya ya fedha ni lazima yatachangia kifo cha biashara.
3. Kukosekana kwa mpango wa ukuaji wa biashara.
Biashara ambayo inaendeshwa kwa mazoea tu ni biashara ambayo inaweza kuharibiwa sana na changamoto itakazokutana nazo. Ndio maana ni muhimu sana kuwa na mchanganuo wa biashara. Katika mchanganuo huu kunakuwa na mpango wa ukuaji wa biashara na pia kunakuwa na mpango wa kukabiliana na changamoto za biashara zitakazojitokeza. Kwa kuendesha biashara ukijua ni wapi unakwenda kwa miaka ijayo ni rahisi kujiweka mbali na zile changamoto ambazo zitawasumbua wafanyabiashara wengine. Kwa mfano kama ulipanga soko lako kuanzia eneo fulani na kisha kukua zaidi, na ukafuata mpango huo, washindani watakaokuiga wataona wewe unaenda mbele badala ya kushindana nao kwenye soko lako la awali.
Ukiweza kudhibiti biashara yako vizuri kwa ndani, changamoto za nje haziwezi kuiua biashara yako. ila kama umeshindwa kuidhibiti biashara yako kwa ndani, chochote kitakachotokea nje kitaacha athari kubwa sana kwenye biashara yako. anza kufanya kazi kubwa ndani ya biashara yako na utaona biashara yako ikizidi kuwa imara hata pale wengine wanapokazana kuokoa biashara zao zisife.