Habari za leo rafiki?

Nina imani unaendelea vyema sana na kufanyia kazi malengo na mipango yako. hongera sana kwa hilo na nikukaribishe kwenye mazungumzo yetu ya siku hii nzuri ya leo.

Kwenye mazungumzo yetu ya leo mimi nitakaa pembeni kidogo na kwa pamoja tutamsikiliza na kujifunza kutoka kwa rafiki yetu ambaye amechagua kuwa mshindi na kuanza maisha ya ushindi.

Kabla hatujaingia kwenye kumsikiliza rafiki yetu mshindi, naomba nikukumbushe kwamba mwezi wa kumi tulikuwa na semina ya MIMI NI MSHINDI. Semina hii ilikwenda vizuri sana na watu waliondoka na maazimio makubwa sana ya kufanyia kazi. Ni katika semina hii ndipo tunapata mazungumzo ya leo.

Katika kila semina ninayoendesha, huwa mwishoni natoa nafasi ya watu kuniandikia kile walichoondoka nacho na wanakwenda kufanyia kazi na pia maoni yao kuhusu semina hiyo na zijazo. Kwa semina hii nimepokea shuhuda na maoni mengi sana, yote ni mazuri na nafarijika sana kwa hatua hizi ambazo watu wanachukua kwenye maisha yao.

Hapa nakuletea moja kati ya shuhuda ambazo marafiki zetu wameniandikia. Karibu sasa tujifunze wote kwa pamoja.

Kwanza kabisa namshukuru Mungu kwa uzima na afya njema aliyotupa.
Coach kama ulivyokuwa umeomba kupata tathmini ya semina ya Mimi ni Mshindi kutoka kwetu, naomba nifanye kama ifuatavyo:-

Kwanza natanguliza shukrani zangu za dhati kwako kwa kuamua kutumia kipaji na taaluma yako kuwasaidia wengine na hasa sisi vijana ili tuweze kujitambua!

Mimi binafsi namshukuru sana Mungu kwa kunikutanisha na wewe!
Kupitia makala zako mbalimbali ndani ya Amka Mtanzania na Kisima cha Maarifa na zaidi kupitia semina ya Mimi ni Mshindi, ambapo ni mara yangu ya kwanza kushiriki semina zako.
Kupitia semina hii nimeweza kubadilika na kuwa kiumbe kipya kabisa. Nitaeleza kwa kifupi kwa kila kipengele cha semina hii.

NILIZALIWA KUSHINDA

Nilikuwa na tabia ya kujilinganisha na ndugu zangu waliofanikiwa na hata wenzangu niliosoma nao na kujihukumu. Lakini kupitia mafunzo haya nimetambua kuwa mimi sifanani na yeyote, nina kitu cha tofauti na ndicho kinanifanya mimi kuwa mshindi. Niko hai, sina kilema chochote, nimelelewa vema na wazazi wangu nk.

MAISHA YANGU NI JUKUMU LANGU
Kushindwa kwangu kunatokana na mimi mwenyewe. Kwa sababu ni mimi mwenyewe natakiwa nifanye jitihada fulani ili nifanikiwe.
“Hakuna muujiza kwenye mafanikio yangu”

NINAAMINI NINAWEZA KUSHINDA
“Imani ni kuwa na hakika na yatarajiwayo. Sina tatizo lolote la kiafya, sina kilema chochote hivyo ninaamini nikiweka juhudi nitashinda japo kuna changamoto.

NINAPIMA USHINDI WANGU KWA MALENGO.
Coach sikudanganyi sijawahi kuwa na malengo “written” katika maisha yangu yote niliyoishi. Mf. Hata shuleni ratiba yangu ya kusoma sikuwahi kuifuata hata mara moja, nilikuwa nasoma kwa mkumbo.
Kwa lugha nyingine nimekuwa nikiishi maisha ya ndoto za alinacha. Kupitia semina hii nimetambua umuhimu wa kujiwekea malengo maana ndio kipimo chenyewe cha kufikia mafanikio.
“Kwangu malengo nimeyachukulia kama deni ambalo natakiwa nililipe hata kama nitakuwa nimehama nchi.”

MIMI KAMA MSHINDI NI MWAMINIFU
Ili nifanikiwe nahitaji kuwa mwaminifu kwa lugha nyingine naweza sema kuwa mkweli kwa nilivyouchambua uaminifu. Si kuishi tabia za mafundi nguo au seremala (Asilimia kubwa wanakosa uaminifu).

NIMEJITOA KUFANYA KWA JUHUDI NA MAARIFA.
Hakuna mazoea kwenye ushindi.
Juhudi na maarifa vinatakiwa ili uwe bora zaidi. Natakiwa nipende ninachofanya kwanza. Pia natakiwa kuwa mtu ninayependa kujifunza kupitia wengine na hata kusoma vitabu na makala mbalimbali ili huduma/kazi yangu iwe bora!

MUDA NI MALI YA THAMANI KWANGU.
Katika watu waliokuwa hawatumii muda vizuri mimi ni mmoja wao, kuamka saa nne, saa sita, kuangalia tamthilia hadi usiku wa manane. Kufanya mambo yasiyokuwa kwenye ratiba ili mradi siku imeenda. Lakini sasa naamka alfajiri, nafanya mazoezi na kufuata mipango ya siku nzima na kutoshabikia mambo ya kijinga.

NIMEZISHINDA HOFU ZOTE
Kama nilivyowahi kushirikisha kwenye group, nilikuwa naogopa sana kubishana na wazazi kwa kuogopa laana. Hivyo nilifanya mambo mengi hata kama siyapendi kisa tu mzazi kasema.
Pia hofu ya kukataliwa na kubezwa ninapotamani kufanya jambo fulani la kuelekea ushindi. Lakini sasa naweza kufanya maamuzi magumu bila kumhofia yeyote wala laana.

KUJIFUNZA KILA SIKU NDIO NGUZO YANGU.
Mimi nilikuwa sina tabia ya kusoma vitabu, lakini sasa imejijenga na pia napenda kuuliza maswali kwa waliofanikiwa kuwa walianzaje anzaje, wanafanyaje, kugoogle na kupitia page muhimu facebook.

NIMEACHA KUTAFUTA SABABU
Hapo kabla nilikuwa ni mtu wa kudhani “Riziki ni mafungu saba” Aliyempa yeye ndio kaninyima mimi”
Na kuona ni watu fulani wamesababisha maisha yangu kuwa hivi.

WAKATISHAJI  TAMAA HAWANIYUMBISHI
Kiukweli kwa sasa simpi mtu nafasi ya “kunilisha sumu”- Maneno ya kukatisha tamaa.

NINAFANYA KILE NILICHOPANGA KUFANYA LEO.
Mf.
Nilikuwa na tabia ya kupanga kitu fulani usiku mfani, Kesho mapema naenda mjini kumwona mtu fulani anipe ushauri juu ya jambo fulani.
Nikiamka natoa lundo la nguo za kufua,h adi nimalize siku ishaisha! Kesho ninapoamua kufuata ile ratiba ya jana Naambiwa huyo mtu jana alikuwepo ila sasa amesafiri.
Kiukweli kwa sasa nafanya kile nilichopanga kufanya leo, maana gharama yake nimeionja.

KUKOSEA NI SEHEMU YA USHINDI
Zamani nilijua nikikosea unakuwa ndio mwisho wa habari. Lakini kupitia semina hii nimejifunza kwamba kunakujenga zaidi.

NINAKAZANA KUWA BORA NA SIO KUWASHINDA WENGINE.
Hahahaha Coach sikutanii wakati mwingine nilikuwa nafanya jitihada kwenye kitu fulani ili nilipize kisasi.
Hasa pale mzazi anapokuwa anamsifia mtoto mmoja tu na kumtolea mifano kwenu.
Lakini kumbe ninachotakiwa kufanya ni kuwa bora kwa viwango vyangu na si kumkomoa mwingine.

NINAJUA HAKUNA NJIA YA MKATO.
Kiukweli nilikuwa naamini kuwa “ukipanda mbegu” kanisani na Pastor akakuwekea mikono kichwani unaweza pata hela. How? Sijui!
Lakini somo hili limenijenga zaidi.
Wakati mwingine niliamini naweza kujishindia bahati nasibu zinazotangazwa na mitandao ya simu. Hivyo kupoteza pesa nyingi kununua vocha.

KULAUMU NA KULALAMIKA NI MWIKO KWANGU.
Maisha yangu yote nimeishi kwa kuwalaumu sana wazazi wangu hasa katika kunifanyia maamuzi, pia serikali na mifumo yake mbalimbali.
Ila sasa nimetambua kuwa kulalamika hakuniongezei kitu chochote zaidi kunadhoofisha mawazo.

MIMI NI KING’ANG’ANIZI SIKUBALI KUKATA TAMAA.
Nilikuwa mwepesi sana wa kukata tamaa, lakini kumbe siri ya mafanikio ni kung’ang’ana.

NINASHUKURU KWA MAISHA HAYA YA USHINDI.
Cha kwa kwanza kabisa namshukuru Mungu kunikutanisha nawe Coach. Umenipa kujiamini sana!
Nilikuwa nimejikatia tamaa na mtu wa kulaumu kila mtu na kila kitu na kujifariji kwa sababu kibao.
Nimejifunza kushukuru hata kwa kidogo ili nipate zaidi.

NINASHIRIKIANA NA WASHINDI WENZANGU.
“Kidole kimoja hakivunji chawa”

NINACHUKUA HATUA MARA MOJA.
Yote niliyojifunza coach, nayafanya kwa vitendo sasa!

MWISHO.
Coach Mungu akubariki sana kwa semina hii uliyoikamilisha kwa asilimia mia bila kutoa na sababu za kushindwa kutimiza wajibu wako. Nimejifunza kwa vitendo pia kupitia hili. Uishi milele.
Coach wakati mwingine ukiweza andaa baadhi ya “Scenario” utakazokuwa unatupa ili tufanye mazoezi baada ya somo ulilofundisha.
Asante kwa cheti pia, ni kizuri mno! Ukikiona unakionea aibu mwenyewe unapokuwa hujatimiza kile ulichopanga. Ni sawa na mtu anayekudai.
“Dawa ya deni kulipa”

Ahsante!

Sekela.

Hayo ndiyo aliyotushirikisha mshindi na rafiki yetu. Nimekushirikisha hapa kwa sababu ninaona kuna mengi sana ya kujifunza kutoka kwake, kwa sababu najua kuna wengi ambao wanapitia alikokuwa yeye, na kuona labda hakuna njia nyingine tena. Ni wakati wa kuamka sasa na kuchukua hatua juu ya maisha yako.

Semina ilishaisha ila bado una nafasi kubwa ya kujifunza kupitia kisima cha maarifa, kwa kuwa kwenye kundi la wasap la kisima, unapata nafasi nzuri sana ya kujifunza na kuanza kuchukua hatua za kuboresha maisha yako.

Kama bado hujaingia kwenye KISIMA CHA MAARIFA, unajikosesha nafasi nzuri sana ya kujifunza na kuboresha maisha yako, hakikisha leo hii haipiti kabla hujajiunga.

Nakutakia kila la kheri kwenye safari hii uliyochagua, ni safari ya kipekee sana, usishangae pale wengine watakapokuwa hawakuelewi.

Rafiki na kocha wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

AMKA CONSULTANTS