Mwishoni mwa mwezi wa kumi, watanzania tulifanya uchaguzi wa kuwachagua madiwani, wabunge na hata raisi wa nchi yetu. Baada ya zoezi la kupiga kura na kuhesabiwa, tume ya uchaguzi ilitutangazia kwamba asilimia 58 ya watanzania wamemchagua Dr. John Pombe Magufuli kuwa raisi wa nchi yetu kwa miaka mitano ijayo.
Kutokana na misingi ya demokrasia ambayo ndio inatuongoza kwenye uchaguzi, anayepata kura nyingi ndiye raisi wa nchi yote. Hivyo Magufuli ndio raisi wetu wa Tanzania kwa miaka mitano ijayo.
Wakati wa kampeni, Dr Magufuli alikuwa akijinadi kwa kauli ya HAPA KAZI TU. Na wananchi wengi waliibeba kauli hii na kuifurahia sana. Na hata baada ya ushindi wananchi wengi wamekuwa wakijinasibu kwa HAPA KAZI TU.
Katika makala hii ya leo nataka tutafakari kwa kina, je kweli watanzania tunaiweza hiyo KAZI TU? Au hata kabla hatujafika mbali, tumeielewa hiyo kazi tu? Na hatimaye tutaangalia ni hatua gani za wewe kuchukua kwenye miaka mitano ijayo ili utakapofanyika uchaguzi mwingine uone tofauti kubwa kwenye maisha yako.

 
Nini maana ya HAPA KAZI TU?
Kipindi cha kampeni na hata hapa mwanzoni mwa uongozi wa Dr Mgufuli, watanzania wengi tuna mategemeo makubwa sana. Tumeahidiwa mengi mazuri ambayo yatafanyika katika uongozi huu. Na hivyo hata kauli hii ya HAPA KAZI TU, wengi wameelewa kwamba kutakuwa na nafasi nyingi za kazi na hivyo tatizo la uhaba wa ajira litafutika haraka sana.
Ni mategemeo mazuri sana na hakuna linaloshindikana, kwa sababu wote tunaielewa nchi yetu vizuri.
Ila nataka nikupe tahadhari kama utanielewa kwamba mategemeo haya makubwa ambayo tunayo hayataweza kufikiwa, hasa kwa kipindi hiki cha miaka mitano. Sisemi haiwezekani kwa sababu nina mtazamo hasi, bali nasema hivyo kutokana na uhalisia na kutokana na sababu nyingine nitakazoeleza hapo chini.
Kwa hiyo kama uliielewa hapa kazi tu kama fursa ya wewe kupatiwa kazi unayotaka na kufurahia maisha, utakuwa umejipoteza. Kwa uelewa wa kawaida HAPA KAZI tu ni kwamba kila mmoja wetu inabidi ajitume zaidi pale alipo sasa. Kama unauza maembe basi uweke juhudi kubwa kwenye kuuza maembe hayo, uuze maembe mazuri na watu wanufaike na kuuza kwako maembe. Kama unafagia barabara basi ufanye hivyo kwa ustadi mkubwa kiasi kwamba kila anayepita kwenye barabara atamani kukutana na yule aliyeifagia.
SOMA; Sababu Tatu(3) Zinazokuzui Kufanikiwa Kwenye Kazi Unayofanya.
Hii ndio maana ya HAPA KAZI TU.
Watanzania pia tunaamini kwamba kutokana na rekodi nzuri ya ufanyaji kazi ya Magufuli basi HAPA KAZI TU alimaanisha atafanya kazi sana yeye. Ndio huenda atafanya kazi sana yeye, lakini taifa halitegemei mtu mmoja kufanya kazi sana ndio maendeleo yaje. Maendeleo ya taifa yanategemea ufanyaji kazi wa kila mwananchi ili kuongeza thamani kwa kila mmoja na maisha kuwa bora zaidi. Hivyo ni vyema ukaelewa mapema kwamba HAPA KAZI TU ni jukumu lako wewe, na sio la rais na viongozi peke yao.
Na bado kuna sehemu ya watanzania ambao wanaishi mwaka 47, hawa ni wale ambao bado wanasubiri serikali iwaletee maisha bora, wale wanaoamini kwa sababu walimchagua mtu fulani basi watapata nafasi ya kunufaika na uongozi wake. Ngoja nikukumbushe kitu kimoja kama bado unaishi mwaka 47, serikali haitakuja kukuletea wewe chakula kwenye sahani. Serikali haitakusaidia wewe moja kwa moja, serikali inahitaji msaada wako ndio iweze kufanya shughuli zake. Wewe unafikiri hiyo mishahara wanayolipwa viongozi inatoka wapi? Inatoka kwenye kodi zetu. Na hizo kodi zinatoka wapi? Zinatokana na sisi kufanya kazi. Hivyo HAPA KAZI TU bado inakurudia wewe mwananchi, ni lazima ufanye kazi sana.
Umeshapiga kura yako na hutakuja kuidai kwa sababu hukutimiziwa kile ulichofikiri wewe, hivyo ni vyema kuelewa haya ya msingi ili uweze kujipanga vizuri.
SOMA; Sehemu Kubwa Ya Watanzania Hatufanyi Kazi, Na Hili Ni Tatizo Kubwa Kwa Maendeleo.
Je watanzania tupo tayari kwa HAPA KAZI TU?
Kwa masikitiko makubwa, na bila ya kubembelezana naomba nikuambie kwamba sehemu kubwa ya watanzania hatupo tayari kwa HAPA KAZI TU. Wengi tumefurahia tu huu usemi lakini bado hatupo tayari. Na nasema hili sio kwa kuwa hasi au kukatisha tamaa, bali kutokana na uhalisia.
Nimepata bahati ya kuwa nakutana na watanzania mbalimbali kwa ajili ya mafunzo na hata ushauri. Na nimekuwa najifunza mambo mengi sana kupitia kila mtu ninayewasiliana naye au kukutana naye.
Na kikubwa sana nilichojifunza ni kwamba watu wengi hatupo tayari kwa kazi tu. Watanzania wengi wana kila sababu kwa nini hawachukui hatua au kwa nini maisha yao sio bora. Watakupa sababu za kutosha na sababu zote hizo ni za uongo.
Huwa nakutana au kuwasiliana na watu kwa ajili ya ushauri labda wa biashara, na mtu anaahidi kabisa ya kwamba atakwenda kufanyia kazi kile mlichoshauriana, lakini cha kushangaza hachukui hatua kabisa, na hata ukimtafuta unakuta hajafanya na ana sababu za kutosha.
Ukienda maeneo ya kazi, hasa kwenye taasisi za umma ndio kabisa watu hawapo tayari kufanya kazi. Watu wapo kwenye eneo la kazi kuonekana kwamba na wao wapo, ila ufanyaji wao kazi ni mdogo sana au wa chini sana kuliko uwezo wao au wanavyotegemewa.
Watu wengi wamekuwa wakifanya kazi kwa kiwango kidogo sana kiasi kwamba hawatafukuzwa na kila siku wanaendelea kulalaika kwamba kipato chao ni kidogo.
Kitu kingine kinachoonesha kwamba watanzania wengi bado hatujawa tayari na HAPA KAZI TU ni kutegemea njia za mkato kupata kipato. Sehemu kubwa sana ya watanzania wanategemea njia za mkato katika kujitengenezea kipato, kuchukua rushwa kutokana na eneo mtu alipo, kuiba na hata kutegemea bahati iwaangukie. Vijana kwa sasa wanatumia muda wao mwingi kubashiri matokeo ya michezo mbalimbali ili waweze kushinda bahati nasibu kwenye kamari mpya inayoitwa Betting.
Sasa yote haya hayaendani na kazi tu, kazi tu ni falsafa ambayo kama kweli tumeamua kwenda nayo tunahitaji kufanya mabadiliko makubwa sana kila mmoja wetu. Tunahitaji kubadili kwanza mtizamo wetu kuhusu kazi na kipato na kuanza kufanyia kazi kweli kile ambacho tunakitaka.
SOMA; Kosa Kubwa Ambalo Waajiriwa Wengi Wanafanya Na Linawazuia Kufanikiwa (Kama Umeajiriwa Usiache Kusoma Hapa).
Mabadiliko makubwa ya wewe kufanya kwa miaka mitano ijayo.
Sasa tujadili mambo ya msingi kuhusu wewe, sio Magufuli tena wala sio watanzania tena, sasa hivi ni kuhusu wewe.
Labda nianze na swali, kama una miaka 28 na kuendelea kaa chini tafakari na jipe jibu la swali hili. Jiangalie ulipokuwa miaka 10 iliyopita, wakati Jakaya Kikwete anaingia madarakani, na jiangalie ulipo leo wakati anaondoka. Angalia ni mabadiliko gani makubwa wewe mwenyewe umeweza kufanya kwenye maisha yako. angalia kipato chako kilikuwa kiasi gani kipindi kile na angalia sasa kipo kiasi gani.
Kama hujawahi kufanya zoezi kama hili mara kwa mara ukifanya leo ni lazima utaumia sana kwani utaona miaka hii kumi hakuna hatua kubwa uliyopiga, wewe binafsi hasa katika maswala ya kazi na kipato. Ndio unaweza kuwa ulisoma na kuongeza elimu kwenye kipindi hiki, lakini je thamani ya kazi au biashara unayofanya iliongezeka? Je kipato kimeongezeka, na hapa sizungumzii kipato cha kuandamana ndio kiongezwe, nazungumzia uwezo wako wa kipato kwa wewe kama wewe.
Sasa nataka leo ujipange kwa miaka mitano ijayo, usiingie tena kishabiki na uache kuishi mwaka 47 ukifikiri kwamba serikali ndio ina jukumu la kukuletea maendeleo wewe. Nataka miaka mitano ijayo, siku unafanyika uchaguzi mwingine mkuu, uweze kuangalia nyuma na kusema miaka hii mitano imekuwa bora sana kwangu.
SOMA; Tabia Tano(5) Za Wafanyakazi Ambao Ni Sumu Kwenye Eneo La Kazi Na Jinsi Ya Kuepuka Kuwa Mmoja Wao.
Ni mabadiliko gani ya kufanya kwenye hii miaka mitano?
1. Inunue na kuishi falsafa hii ya HAPA KAZI TU.
Hatua ya kwanza na ya muhimu sana ni wewe kuinunua na kuiishi falsafa hii ya HAPA KAZI TU, ninaposema kuinunua simaanishi ulilipie, hapana namaanisha ulielewa na kukubali kuifanyia kazi.
Kwa miaka mitano ijayo jitoe kufanya kazi kweli, na jitoe kufanya kazi kwa juhudi kubwa na maarifa makubwa pia. Kwa miaka hii mitano weka malengo ya kuongeza thamani kubwa sana kwenye kile ambacho unafanya.
Iwe ni kazi ambayo umeajiriwa, iwe ni biashara yako au umejiajiri, jitoe kutoa thamani kubwa sana. Amua kutoka ndani ya moyo wako kwamba chochote ambacho utakigusa kitabaki kuwa bora sana.
2. Weka malengo ya kufikia asilimia 1000 ya ulipo sasa.
Kitu kingine kikubwa cha wewe kufanya ni kuweka malengo makubwa kwenye miaka hii mitano ijayo. Elewa vizuri hapo, sio kuweka tu malengo, bali kuweka malengo makubwa na makubwa sana.
Kwa mfano anza kwa kupitia kipato chako kwa sasa, unapata kiasi gani, unaweka akiba kiasi gani, unawekeza kiasi gani. Baada ya kujua ulipo sasa, piga asilimia elfu moja ya pale ulipo sasa, kwa kifupi ni kuzidisha mara kumi ya pale ulipo sasa.
3. Acha maneno na fanya kazi.
Najua umekuwa na maneno mengi sana. Najua umekuwa ukijipa sababu nyingi sana. Najua umekuwa ukiona unafanya zaidi ya unachopata. Lakini nakuambia kwamba maneno hayatakufikisha popote, sababu hata zingekuwa nzuri kiasi gani, hazikusaidii, kitakachokusaidia ni kufanya kazi.
Acha kupika kelele na fanya kazi, acha kutafuta sababu na fanya kazi, acha kulalamika na fanya kazi. Fanya kazi ukilenga kuongeza ubora katika kile ambacho unafanya.
Unahitaji kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye ufanyaji wako wa kazi, unahitaji kufanya mabadiliko makubwa sana kwenye mtizamo wako kuhusu kazi. Na ifanye miaka hii mitano kuwa ya KAZI TU kweli na kuleta mabadiliko chanya kwenye maisha yako.
Hakuna kinachoshindikana kama kweli utaamua kuweka juhudi. Nakutakia kila la kheri katika ufanyaji huu kazi mpya wa maendeleo makubwa kwako na kwa taifa kwa ujumla.
Endelea kutembelea AMKA MTANZANIA, www.amkamtanzania.com kila siku ili kujifunza na kupata hamasa ya kuendelea kufanya kwa ubora kila siku.
Pia tembelea na jiunge na KISIMA CHA MAARIFA, www.kisimachamaarifa.co.tz ili kupata maarifa bora zaidi ya kukuwezesha kuboresha kila unachofanya na maisha yako kwa ujumla.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
AMKA CONSULTANTS.