Giza sio kitu, bali ni ukosefu wa kitu.

Giza sio kitu kwa sababu huwezi kulifanyia chochote, huwezi kulifanyia vipimo vya kitaalamu, ni giza tu basi huwezi kwenda zaidi.

Giza sio kitu bali ukosefu wa mwanga, mwanga unapokuja, giza linaondoka, wala hakuna ushindani wowote, mwanga ukiwepo hakuna giza.

Mwanga ni kitu, na unaweza kuufanyia vipimo au hata kuutumia kwa shughuli nyingine muhimu.

Hivi pia ndivyo ilivyo kwa hofu,

Hofu sio kitu, bali ni ukosefu wa kitu.

Hofu sio kitu, bali hofu ni ukosefu wa upendo. Unapokuwa huna upendo ndipo hofu inapoingia. Leta upendo na hofu itakimbia yenyewe, wala hakuna kushindana.

Hofu yoyote uliyonayo sasa, inaanzia kwenye kukosa upendo, jaribu kuchunguza. Labda umekosa upendo kwako wewe mwenyewe, au umekosa upendo kwa wale wanaokuzunguka au umekosa upendo kwa kile unachofanya. Anza kuweka upendo na mambo yatakuwa mazuri, hofu itatoweka.

Ukitaka giza ondoa mwanga, ukitaka hofu, ondoa upendo.

SOMA; TABIA ZA MAFANIKIO; Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Wakati Unajenga Tabia Za Mafanikio.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba hofu yoyote niliyonayo inatokana na kukosa upendo kwenye eneo fulani. Hofu sio kitu bali ukosefu wa upendo. Kuanzia sasa nitaweka upendo na mapenzi ya dhati kwangu mimi binafsi, kwa wanaonizunguka na kwa kile ambacho ninafanya.

NENO LA LEO.

“There are two basic motivating forces: fear and love. When we are afraid, we pull back from life. When we are in love, we open to all that life has to offer with passion, excitement, and acceptance.”
― John Lennon

Kuna nguvu kuu mbili zinazotupa motisha; HOFU na UPENDO. Tunapokuwa na hofu tunashindwa kuishi maisha yetu. Tunapokuwa na upendo, tunayakubali maisha yetu na kile ambacho maisha yanatupatia kwa hamasa na utayari mkubwa.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.