Watu wengi wanaingia kwenye ujasiriamali kwa sababu wanaona ndio sehemu nzuri ya kujitengenezea kipato huku ukiwa na uhuru mkubwa. Ni kweli kabisa kwamba ujasiriamali unakupatia uhuru mkubwa. Lakini pia kuna mambo mengi ambayo watu wengi wanaoingia kwenye ujasiriamali huwa hawajui mpaka pale wanapokutana nayo. Na hata baada ya kukutana nayo bado wengi wanakuwa hawajifunzi kupitia mambo hayo.
Pia pamoja na kutolewa kwa mafunzo ya ujasiriamali, bado kuna mambo muhimu ambayo wajasiriamali huwa hawaambiwi. Kwenye mafunzo mengi ya ujasiriamali watu wanapewa mbinu nzuri za kuhusiana na ujasiriamali, ila zile mbinu zinazowahusu wao binafsi kuhusiana na ujasiriamali huwa hazifundishwi.
Leo katika makala hii ya kona ya mjasiriamali utapata nafasi ya kujifunza mambo muhimu kuhusiana na safari ya ujasiriamali ambayo hujapata nafasi ya kuambiwa sehemu nyingine yoyote.
1. Safari ya ujasiriamali ni safari ya upweke.
Kuna wakati kwenye safari hii ya ujasiriamali utakuwa mpweke sana. Kuna wakati unakuwa na mawazo mazuri kabisa ya kuboresha kile unachofanya lakini kila unayejaribu kumwambia anakuambia unakosea au utashindwa. Unaweza kujaribu kuwashawishi watu lakini bado ukabaki wewe mwenyewe ndiye unayeamini hiko unachotaka kufanya.
Unapokutana na hali hii usijisikie vibaya na wala usione kama umepotea. Jua kwamba ujasiriamali ni safari ya upweke na kuna wakati ambapo utahitaji kusimama wewe mwenyewe. Hata kama wengi wanakupinga au wanakukatisha tamaa, kumbuka wewe ndio una maono makubwa na endelea kuyafanyia kazi. Mapinduzi makubwa kwenye ujasiriamali yanaletwa na wale wanaoweza kusimama wenyewe hata mambo yanapokuwa magumu.
2. Kipato sio cha uhakika.
Watu wengi wanapoingia kwenye ujasiriamali huwa wanaamini kwamba wanakwenda kupata uhuru wa kifedha. Wanafikiri ya kwamba kwa kuwa kwenye ujasiriamali basi watakuwa na wateja na kupata faida na hivyo kujilipa vizuri kulingana na faida wanayopata. Kwenye mipango hii ni kweli kabisa, ila kwenye utendaji sio kweli. Safari ya ujasiriamali, hasa mwanzoni, kipato sio cha uhakika. Unaweza kuona watu wengi wanaonekana kupenda kile unachotoa lakini wakawa hawanunui. Au wakanunua lakini isitoshe kutoa gharama za uendeshaji na wewe kubaki na faida.
Jua kabisa unapoingia kwenye safari ya ujasiriamali, kipato chako kitakuwa sio cha uhakika. Mwezi mmoja kupata faida ya milioni moja, haimaanishi na mwezi ujao utapata faida hiyo. Kuna vitu vingi vinaweza kutokea ambavyo wewe huwezi kuvizuia moja kwa moja. Kwa kujua hili itakusaidia kuwa na mipango mizuri ya fedha, usitumie fedha yote unayopata kwa kufikiri nyingine inakuja, ni vyema ukajihakikishia kwamba una uwezo wa kuendelea na maisha hata kama kipato hakitakuwa cha uhakika.
3. Unahitaji kusema HAPANA mara nyingi mno.
Unapokuwa mjasiriamali kwanza una uhuru mkubwa, na uhuru huu unaweza kuja na madhara yake pia. Kwa kuona unamiliki muda wako mwenyewe ni rahisi kukubali kufanya vitu ambavyo sio muhimu kwa biashara yako. kwa sababu hakuna anayekulazimisha kuwahi kwenye eneo lako la kazi, ni rahisi kujipa sababu kwa nini siku fulani huwezi kuwahi.
Unapokuwa mjasiriamali jua unahitaji kusema hapana kwa kitu chochote ambacho sio muhimu kwa maendeleo ya biashara yako. kama kitu unataka kufanya au unashawishiwa ufanye lakini hakina mchango kwenye biashara yako, sema hapana. Hata kama ni watu wako wa karibu ambao wanataka ufanye yale ambayo ni muhimu kwao ila yanaathiri biashara yako sema hapana. Najua ni vigumu kusema hapana, lakini anza kujizoesha hivyo. Hii ni njia itakayokuwezesha wewe kuwa na matumizi mazuri ya muda wako.
4. Vitu vingi utajifunza kwa kukosea.
Pamoja na kwamba utajifunza vitu vingi kwa kusoma au kuhudhuria mafunzo ya ujasiriamali, bado sehemu kubwa ya vitu utajifunza kwa kukosea wewe mwenyewe. Kutokana na kutokuwa na uzoefu utapanga kufanya mambo mengi na mazuri, katika kufanya mambo hayo utakosea na ni katika kukosea huko ambapo unajifunza somo zuri sana.
Kwa kulijua hili kunakusaidia pale unapokosea kwenye ujasiriamali. Usichukulie makosa kama mwisho, bali chukulia kama darasa muhimu sana kwako. Na hakikisha kwa kila kosa unatafakari ni mambo gani umejifunza ili iwe msaada kwako na usije kurudia tena wakati mwingine.
5. Ujasiriamali sio “jeshi la mtu mmoja”
Wengi wanapokuwa wanaingia kwenye ujasiriamali hufikiri jitihada zao binafsi ndio zitakazowaletea mafanikio kwenye ujasiriamali. Ni kweli jitihada binafsi ni muhimu sana, ila mchango wa wengine ni muhimu zaidi. Hata kama biashara unayofanya ni ya mtu mmoja bado unahitaji kuwa na ushirikiano mzuri sana na watu mbalimbali ambao ni muhimu kwenye biashara yako.
Unahitaji kuwa na ushirikiano mzuri na wateja wako, unahitaji kuwa na ushirikiano mzuri na wafanyabiashara wenzako, unahitaji kuwa na ushirikiano mzuri na wale wanaokupatia huduma mbalimbali na pia unahitaji kuwa na ushirikiano mzuri na familia yako pia. Kwa sababu wote hawa wana mchango muhimu sana kwako wewe kufanikiwa kwenye ujasiriamali.
Hongera sana kwa wewe kuwa mjasiriamali, kwani pamoja na changamoto zote unazopitia, wewe una mchango mkubwa kwa jamii na pia utaleta mabadiliko makubwa. Yajue vizuri mambo hayo matano ambayo mara nyingi huambiwi na yafanyie kazi, yatapunguza ukali wa safari hii ya ujasiriamali. Nakutakia kila la kheri.
Rafik na Kocha wako,
Makirita Amani