Habari za leo rafiki?
Naamini unaendelea vyema sana na majukumu yako ya kila siku. Na nina imani kabisa ya kwamba kama unafanyia kazi haya ambayo tunashirikishana hapa basi mambo yako yatakuwa yanabadilika kadiri siku zinavyokwenda.
Naomba nikukumbushe pia ya kwamba mabadiliko hayaji mara moja kama mvua, bali yanakuja kidogo kidogo na siku moja unashangaa kila kitu kinakwenda vizuri kuliko ilivyokuwa awali.
Hivyo hata kama unafanyia kazi lakini huoni mabadiliko ya haraka, usikate tamaa.
Karibu tena kwenye mazungumzo yetu ya leo ambapo tunashirikishana yale muhimu kwa ajili ya kuwa na maisha bora na yenye mafanikio.
Leo nataka tugusie sehemu muhimu sana ambapo inahusu watu walioajiriwa. Na hata kama hujaajiriwa endelea kusoma maana inaweza kuhusika hata kwa waliojiajiri au wanaofanya biashara.
Mara zote tumekuwa tukiona watu wakienda shuleni wakiwa na matumaini makubwa kwamba wakimaliza watapata kazi nzuri na maisha yatakuwa bora. Na pale wanapomaliza na wakapata kazi, japo kwa sasa ni vigumu, wengi huwa wanakaa kwenye kazi zile kama wafungwa. Unakuta mtu yupo kwenye kazi miaka mingi, kazi haifurahii na pamoja na hayo bado anakuwa hawezi kuondoka kwenye kazi hiyo.
Kwa kifupi mtu huyu anakuwa ameshapoteza uhuru wake na hana tena njia nyingine ya kufanya zaidi ya kuendelea kuitegemea kazi.
Huenda wewe upo kwenye hali ya mtu huyu, na kama hupo basi unawajua watu wengi ambao wapo kwenye hali hii. Leo hii tutapata nafasi ya kupitia hili kwa undani na kujua hatua za kuchukua kwa wale ambao wameshaingia kwenye mtego huu.
Kujenga Nyumba Kwenye Kiwanja Cha Kukodi.
Nimewahi kuandika makala moja nikasema usijenge nyumba kwenye kiwanja cha kukodi. Yaani mtu anakupangishia wewe kiwanja, halafu wewe unajenga nyumba kwenye kiwanja hiko. Unajua ni nini kinatokea baadaye? Mwenye kiwanja atakuambia nataka kiwanja changu, hivyo ondoa nyumba yako, na kwa kuwa huwezi kuondoa , basi itabidi ukubaliane na chochote ambacho atakuambia yeye, na hapo ndipo unapopoteza kabisa uhuru wako kwenye nyumba yako uliyojenga mwenyewe. Kwa kosa dogo tu la kushindwa kujua ya kwamba kiwanja cha kukodi siyo sehemu sahihi ya kujenga nyumba.
Hii inafananaje na kwenye ajira?
Inafanana kwa kila hatua. Mtu anaajiriwa na kuanza kufanya kazi, hapa kuajiriwa ni sawa na kukodishiwa kiwanja. Maana haijalishi umedanganywa kiasi gani, ajira siyo mali yako.
Sasa nini kinatokea baada ya mtu kuajiriwa? Anaanza kufanya mambo makubwa ambayo yanategemea ajira yake moja kwa moja. Anachukua mkopo wa miaka mingi, labda mitano kupitia ajira yake. Anaingia madeni mengine mengi kwa kutumia kivuli cha ajira yake. Hapa sasa ndipo nyumba inaanza kujengwa kwenye uwanja wa kukodi.
Kama mtu ameingia kwenye kazi na mwaka wa kwanza au wa pili kachukua mkopo wa miaka mitano, ina maana kwa miaka hii mitano amejifunga kuendelea kumtumikia mwajiri, hata kama hali itakuwa hovyo kiasi gani. Na kwa sababu anaendelea kuyajenga maisha yake kwenye ile ajira, basi anaendelea kuweka mizizi ambayo inazidi kumaliza uhuru wake.
Huu mkopo wake wa miaka mitano unaweza usikamilishe kile anachotaka, hivyo anachofanya ni nini? Anaenda kuomba mkopo mwingine, labda sasa anafika hata miaka kumi. Mh miaka kumi ni mingi sana kuwa umefungwa sehemu moja, na ukiwa huna nguvu ya kupinga au kukataa kile usichotaka.
Hivi ndivyo waajiriwa wanapoteza uhuru wao
Sahau kuhusu sheria na mikataba.
Utaniambia lakini kuna sheria za ajira, kuna sheria zinanilinda, kuna mikataba nimeingia. Na mimi nitakuambia sawa, subiri utakapoingia kwenye matatizo utajua sheria inaegemea wapi. Sheria iko vizuri pale ambapo hujaingia kwenye matatizo, lakini ukishaingia kwenye matatizo, na huku umeshauza uhuru wako, huna tena ujanja rafiki yangu. Kama umewahi kupitia hili utakuwa shahidi mzuri, kama hujawahi kupitia jaribu kuongea na wenzako ambao wameshapitia hayo.
Kwa hiyo unasema tusitegemee ajira zetu kujenga maisha yetu.
Hapana, sijasema hivyo, ninachosema ni kwamba usiuze uhuru wako wa maisha kwenye ajira kwa kisingizio kwamba unajenga maisha. Kuna njia nyingine bora sana za kujenga maisha yako bila ya kuuza uhuru wako.
Na wafanyabiashara pia wamo.
Kuna kipindi nilipata nafasi ya kumshauri mfanyabiashara mmoja, alikuja na tatizo kwamba alipata mkataba wa kusambaza mzigo mkubwa kwa kampuni fulani. Waliingia mkataba kabisa ya kwamba atawasambazia mzigo huo kwa mwaka mzima. Akaenda na mkataba benki na akaomba mkopo mkubwa, kwa sababu alishakuwa na uhakika mwaka mzima angeweza kuurejesha. Miezi mitatu baadaye ile kampuni aliyokuwa anaisambazia wakaanza kutotimiza sehemu ya wajibu wao, mwishowe wakaacha kuchukua mzigo kabisa.
Alikuja kwangu kwa changamoto ya kuwa na deni kubwa sana benki, na hajui atalilipaje maana muda wakulipa ulishapita na benki walikuwa wanataka kuuza nyumba yake. Si alikuwa na mkataba? Ndio na alifungua kesi mahakamani, lakini kama nilivyokwambia hapo juu, ukishaingia kwenye matatizo ndio utajua kwamba sheria inaegemea wapi.
Kama nilivyosema hapo juu, usijenge msingi imara kwenye kitu ambacho huwezi kukiathiri moja kwa moja, angalau kuwa na mpango mbadala, kama unataka kuendelea kuwa na uhuru wako na kufanya kile ambacho ni bora kwako.
Ufanye nini sasa ili usiingie kwenye mtego huu.
Kwa wale ambao wameajiriwa siku sio nyingi, au kama utakwenda kuajiriwa, kuwa makini sana kabla hujaingia kwenye mambo ambayo yatapoteza kabisa uhuru wako. Unapotaka kufanya maamuzi makubwa ambayo yatategemea sana ajira yako, angalia njia mbadala ya kufanya hivyo na isiwe ajira. Kuna njia nyingi sana za kuanzia, ikiwa kujipa muda wa kujijenga, yaani usitake umeanza kazi leo na baada ya muda una nyumba, gari na vingine vingi, na vyote umepata kwa njia ya mkopo. Jipe muda kidogo, na jenga vyanzo vingi vya kipato ambavyo vitakupa uhuru mkubwa.
Ufanyeje ili uondoke kwenye hali hii kama umeshaingia?
Kwanza pole rafiki yangu.
Pili acha kile ulichofanya mpaka ukafika hapo ulipo. Wanasema ukishajikuta kwenye shimo, kwanza acha kuchimba. Acha kuendelea kufanya maamuzi makubwa ukitegemea ajira yako moja kwa moja. Acha kuendelea kuchukua mikopo mikubwa ukitegemea ajira. Kwa mfano wa mfanyabiashara niliotoa hapo juu, mpango wake ulikuwa ni kuchukua mkopo mwingine ili kuondoka pale alipokuwa, alikuwa anataka kuchimba zaidi.
Tatu, anza kutengeneza vyanzo mbadala vya kipato ambavyo vitakuwezesha wewe kununua uhuru wako. Angalia kwa pale ulipo na ujuzi na uzoefu ulionao, ni nini unaweza kufanya cha ziada kisha anza kufanya.
Naamini haya uliyojifunza leo yatakusaidia uondoke kwenye utumwa au yatakuzuia usiingie kwenye utumwa.
Kama unavyojua, hakuna kitakachofanya kazi kama wewe mwenyewe hutafanya kazi.
Kila la kheri, kama utahitaji ushauri zaidi tuwasiliane.
Rafiki na kocha wako,
Makirita amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
AMKA CONSULTANTS
Ahsante kocha nimekutana na rafiki yangu ananishawish nikope lakin mh sijawah fikiria kuchukua mkopo wa kununua kiwanja nafurah kukufahamu kwa mafunzo yako uliyonipa ubarikiwe
LikeLike
Vizuri sana,
Usikubali kuingia kwenye mtego huo, utajutia maisha yako yote.
Kila la kheri.
LikeLike