Mambo Kumi (10) Kuhusu Maisha Na Mafanikio Niliyojifunza Kutoka Kwa Edward Ngoyai Lowassa.

Napenda sana kujifunza kupitia watu ninaokutana nao au ninaowasoma katika maandiko mbalimbali. Na kupitia watu wengi ninaojifunza kutoka kwao, kuna wachache ambao nawaita “MY VIRTUAL MENTORS” yaani washauri wangu wa mbali. Hawa ni watu ambao wanakuwa wamefanya mambo makubwa sana kutokana na vipimo vyangu na napenda na mimi kuweza kufikia pale walipofikia wao.
Katika orodha yangu ya virtual mentors kuna watu wengi walioishi zama tofauti na wengine bado wanaishi. Na pia wapo watu wa mataifa mbalimbali duniani. Mmoja wa watu walioingia kwenye orodha yangu hii kwa siku za hivi karibuni ni aliyekuwa mgombea wa uraisi wa Tanzania Edward Ngoyai Lowassa.
Katika kipindi chote cha kampeni, mpaka kufika uchaguzi na baadaye kutangazwa kwa matokeo, kuna mambo mengi sana niliyojifunza kwa mentor wangu huyu. Na hata maisha yake kabla ya uchaguzi huu kuna mengi pia ya kuweza kujifunza.

 
Hapa nakushirikisha mambo kumi muhimu niliyojifunza kutoka kwa Lowassa, huenda na wewe ukaweza kuyafanyia kazi na maisha yako yakawa bora zaidi. Kumbuka hivi ni vigezo nilivyoweka mwenyewe kwa hiyo inaweza isionekane ni kitu kikubwa kwako. Karibu tujifunze kupitia mentor wangu huyu…
1. Unapokitaka kitu, jitoe hasa.
Lowassa alikuwa na ndoto za kuwa raisi wa Tanzania, na alijitoa kweli kupigania ndoto yake hiyo. Hakukubali kitu chochote kimzuie yeye kufikia ndoto yake hiyo kubwa. Ndio maana hata baada ya kutopitishwa na chama cha mapinduzi aliangalia njia nyingine anayoweza kutumia na hatimaye akaweza kugombea kupitia chama cha upinzani.
Ili uweze kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako, unahitaji kujitoa hasa, unahitaji kuangalia kila njia unayoweza kutumia ili kufikia lengo lako. Hata kama njia moja uliyokuwa unategemea imefungwa, basi angalia njia yoyote mbadala unayoweza kutumia. Na kama umejitoa kweli ni lazima utapara njia mbadala. Jitoe na pigania kile unachotaka, hakuna kitu rahisi.
2. Watu wengi hawatakuelewa.
Katika safari yako ya mafanikio, safari ya kufikia kile unachotaka, watu wengi hawatakuelewa. Kwa sababu wewe umejitoa kweli na hukubali kitu chochote kikuzuie kupata kile ambacho unakitaka, watu wengi watasema una tamaa, una uchu na mengine mengi. Wengi wanatumia maneno kama haya kwa njia hasi, kama vile kutaka kitu kwa moyo sana ni dhambi kubwa.
Kutokana na Lowassa kutaka sana nafasi ya urais na kuhakikisha anajitoa kweli, wengi waliona ana tamaa na uchu wa madaraka. Wengi walisema ni mtu hatari kwa sababu akipata nchi anaweza kufanya mambo yasiyotegemewa. Lakini hili linatokana na wengi kutokuelewa jitihada zinazohitajika ili upate kile unachokipata.
Unapochagua njia hii ya mafanikio, na kujitoa kwa kila ulichonacho, wengi hawatakuelewa, ila hili lisikuzuie, endelea kusonga mbele.
SOMA; Mambo Kumi(10) Muhimu Usiyojua Kuhusu Mafanikio, Na Jinsi Yanavyokurudisha Nyuma.
3. Kuanguka sio mwisho wa safari.
Katika safari yako ya mafanikio, katika maisha yako, kuna maeneo mengi ambapo utaanguka. Na haijalishi utaanguka vibaya kiasi gani, kama bado upo hai basi sio mwisho wa safari.
Lowassa alianguka sana kwenye safari yake ya kisiasa. Kuanzia alipojiuzulu kutokana na kasha ya Richmond mwaka 2008. Pamoja na kuanguka huku kutokana na kasha kubwa, hakutaka hii iwe ni kikwazo kwake, badala yake aliendelea kujijenga ili kutimiza ndoto yake yakuwa raisi wa nchi yake.
Hata wewe unapochagua safari hii ya mafanikio, safari ya kuwa na maisha bora, safari ya kufanya kazi au biashara yako kwa ubora, ni lazima utaanguka. Lakini kuanguka huku kusikufanye uachane na ndoto yako kubwa uliyonayo. Hata kitokee kitu gani, ni lazima safari yako iendelee.
4. Marafiki. (sehemu ya kwanza)
Tangu zamani imekuwa ikijulikana kwamba rafiki wa karibu sana wa Lowassa ni Kikwete. Na hata baada ya kujiuzulu, kuna kauli ilikuwa inasikika mara kwa mara kutoka kwa wawili hawa kwamba wao ni marafiki na hawakukutana barabarani. Yaani wao ni marafiki wa ndani sana na wametoka mbali sana. Hivyo kama rafiki, Lowasa alitegemea msaada mkubwa wa yeye kufikia ndoto yake kutoka kwa rafiki yake. Lakini mwishowe tulimsikia Lowasa akitoa kauli za kuonesha kutelekezwa na rafiki yake huyu mkubwa.
Kikubwa cha kujifunza hapa ni kwamba unaweza kuwana rafiki ambaye mmetoka mbali sana na mkawa mmekubaliana kusaidiana, lakini ikafika kipindi rafiki yako huyu akaacha kuwa na wewe. Hivyo jua ni jinsi gani utakavyoweza kuendelea kutimiza ndoto yako hata kama rafiki unayemtegemea ataacha kukusaidia. Ndoto yako isifike mwisho kwa sababu rafiki yako uliyemtegemea sana hayupo tena na wewe. Muhimu zaidi ni usimfanye mtu yeyote kuwa na madhara makubwa sana kwenye maisha yako kwa kuwepo au kutokuwepo kwake.
5. Unachotegemea hakitatokea.
Wakati Lowassa anaondoka CCM na kwenda CHADEMA alitegemea angeondoka na watu wengi sana. Alitegemea angeondoka na wabunge wasiopungua 50, mawaziri na wanachama wasiopungua milioni moja. Lakini hili sio lililotokea, japo kuna wengi waliomfuata, lakini sio kwa idadi ile ambayo alitegemea.
Katika safari yako ya maisha na mafanikio, kuna mambo mengi sana ambayo utapanga na utategemea. Lakini sio mambo yote yatakayotokea kama utakavyopanga. Hivyo jiandae kwa hili na jua ni hatua gani utakayochukua kama mambo hayataenda kama ulivyopanga. Kwa kujiandaa hivi itakuwezesha kukabiliana na changamoto utakayokutana nayo.
6. Kukazana na kile unachotaka, kuachana na kelele.
Kuna neno la kiingereza linaitwa FOCUS, maana yake ni kuweka nguvu zako zote kwenye kile ambacho unakitaka, na kuachana na kelele nyingine zozote. Lowassa aliweza kufanya hivi kwa kupelekea nguvu zake kwenye kuutaka uraisi. Na kwa kufanya hivyo alikazana kulenga yale ambayo yatampatia kura na sio kujibizana na watu. Katika kampeni za uraisi, tuliona wengi wakimkashifu, wengi wakimtukana, na wakitegemea atajibu mapigo lakini yeye hakufanya hivyo, aliendelea na juhudi zake za kuupata uraisi.
Unahitaji FOCUS sana kwenye safari yako ya mafanikio kama unataka kuyafikia kweli. Hii ni kwa sababu chochote utakachofanya au utakachopanga kufanya, kuna wengi watakupinga, kuna wengi watakukatisha tamaa na kuna wengine wengi watataka kukurudisha nyuma. Sasa kama wewe utaamua kupambana na watu hawa, utapoteza muda wako bure. Badala yake wewe waache wafanye hayo yanayowafurahia, ila wewe kazana kufikia ndoto yako kwa kuwajibu wanaokupinga, bali utaifikia kwa kuifanyia kazi.
Acha mara moja kujaribu kumjibu kila anayekupinga. Acha mara moja kupambana na kila anayekurudisha nyuma. Peleka nguvu zako kwenye kufikia kile unachotaka.
SOMA; Hivi Ndivyo Unavyoweza Kutajirika Kwa Kuanza Na Shilingi Elfu Moja.
7. Elimu, elimu, elimu.
Kitu kimoja ambacho Lowassa alisema angekitilia mkazo kama angechaguliwa kuwa raisi ni ELIMU. Ni kweli kabisa ya kwamba elimu ndio msingi muhimu sana kwenye maendeleo ya mtu mmoja mmoja na hata taifa kwa ujumla. Ukosefu wa elimu bora unatugharimu sana kama taifa. Na ni wakati sasa umefika tutengeneze mfumo mpya wa elimu utakaoendana na matakwa yetu.
Tumeona mfumo tulionao ukizalisha waajiriwa wengi kuliko nafasi zilizopo. Na hii inaendelea kuleta shida kubwa kwa wengi.
Na pia elimu sio ile rasmi tu, kuna elimu kubwa ambayo wewe unatakiwa uipate ili uweze kufikia mafanikio yako. unahitaji kufanya kile unachofanya kwa utaalamu mkubwa na hata kwa utofauti na wanavyofanya wengine. Yote haya utaweza kama utaweka kipaumbele chako cha kwanza kuwa elimu.
Usikubali siku ipite hujajifunza kitu chochote kipya kuhusiana na kazi au biashara unayofanya, kujifunza kutakusaidia sana kufikia mafanikio makubwa.
8. Marafiki. (sehemu ya pili)
Kuna marafiki ambao wapo na wewe wakiwa na ajenda zao. Na wengi wanaangalia ni jinsi gani wao wananufaika na wewe. Hivyo wakiona kuna nafasi za kunufaika watakuwa na wewe pamoja, wakiona hakuna nafasi hiyo wataachana na wewe.
Lowassa alikuwa na marafiki wengi alipokuwa CCM, na aliamini ni watu wake wa karibu sana na wangekuwa tayari kwenda naye popote atakapokwenda. Lakini wengi hawakuweza kwenda naye, kwa sababu yale maslahi waliyokuwa wanaona watapata mwanzo, hawakuyaona tena.
Jua kuna watu wa aina hii kwenye maisha yako, na wasikuumize kichwa pale ambapo wataondoka kutokana na kuona maslahi yao hayapo tena.
9. Kuendelea kuwa na moyo wa ushindi.
Hata baada ya kushindwa uraisi, Lowassa ameendelea kuwa na moyo wa ushindi. Na moja ya kauli aliyotoa baada ya kushindwa ni kwamba; I might have lost a battle, but not a war. Akimaanisha kwamba amepoteza pambano moja, ila hajashindwa vita nzima.
Huu ni moyo unaohitaji kuwa nao kama kweli unataka kufikia mafanikio makubwa. Kwa sababu kwenye safari yako hii utapoteza mapambano mengi sana. Lakini kama hutakata tamaa lazima utashinda vita.
SOMA; Kama Una Tabia Hizi 30 Tayari Wewe Ni Mjasiriamali, Chukua Hatua.
10. Kujali maslahi mapana ya taifa.
Baada ya kupiga kura na kura zikaanza kuhesabiwa, matokeo yalipoanza kutangazwa, watu wengi walishtushwa na kusikitishwa na matokeo yaliyokuwa yanatolewa. Wengi walisema Lowassa aliibiwa kura na mwenyewe alidhibitisha hili. Baada ya hili wananchi wengi walikuwa na hasira na walikuwa wanataka kusikia neno moja tu kutoka kwa Lowassa kwamba wafanye nini. Lakini kwa busara kubwa Lowassa hakutaka kusababisha machafuko kwenye nchi, kitu ambacho angeweza kufanya kama angewasisitiza wafuasi wake kudai ushindi wao. Lowassa alijali maslahi mapana ya taifa.
Naamini kuna mambo ambayo umejifunza na utayafanyia kazi. Lengo kubwa hapa ni wewe kuweza kuchukua hatua na kuboresha maisha yako. hakuna kinachoshindikana pale unapoamua kweli ni nini unataka.
Nakutakia kila la kheri katika utekelezaji wa haya uliyojifunza.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
0717396253
AMKA CONSULTANTS

2 thoughts on “Mambo Kumi (10) Kuhusu Maisha Na Mafanikio Niliyojifunza Kutoka Kwa Edward Ngoyai Lowassa.

Add yours

 1. Asante Mbaruku,
  Fanyia kazi yale uliyojifunza.
  Kuhusu kutokupokea email jaribu kuangalia email zako vizuri kama unatumia gmail. Na kama huoni kabisa basi jiandikishe tena.
  Kama utaendelea kupata tatizo tuwasiliane 0717396253.
  Karibu sana,
  TUPO PAMOJA.

  Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

Create a website or blog at WordPress.com

Up ↑

%d bloggers like this: