Ndio kila mmoja wetu anapenda mafanikio makubwa kwenye maisha.

Lakini jambo moja la ukweli ambalo huenda hujawahi kulipa uzito ni kwamba mafanikio yako hujiletei wewe mwenyewe.

Kwa dunia tunayoishi ambayo kila kitu unamtegemea mwingine, huwezi kusema kwamba utajipa mafanikio yako wewe mwenyewe.

Mafanikio yako yatatoka kwa watu wengine.

Yaani wengine ndio watakufanya wewe ufanikiwe, japokuwa malengo, mipango na juhudi utaweka wewe mwenyewe.

Hivyo basi kabla wewe hujafanikiwa kuna mtu au watu ambao inabidi wafanikiwe kwanza. Na watu hawa watafanikiwa kupitia wewe. Yaani wewe utawafanya hawa wafanikiwe, halafu na wao watakufanya ufanikiwe.

Ni raha iliyoje!!

Sasa je ni nani unatakiwa kumfanya afanikiwe?

Kwako wewe ni yule ambaye anategemea kile unachokifanya.

Kama unafanya biashara basi biashara yako imwezeshe mteja wako kufanikiwa na mteja atakuwezesha wewe kufanikiwa. Kwa kuendelea kuwa mteja wako na kuwaambia wengine pia.

Kama umeajiriwa hakikisha unamwezesha mwajiri wako kufanikiwa na yeye atakuwezesha wewe kufanikiwa pia. Na pia wale wanaopokea huduma unayotoa wawezeshe kufanikiwa, na wao watakuwezesha pia.

Unaona jinsi ambavyo tupo kwenye dunia ya kuwezeshana?

Haya nimeshakuwezesha wewe kwa kukupa maarifa ya kutumia nguvu ya uwezeshanaji. Niwezeshe na mimi kuwafikia wengi zaidi, kwa kuwatumia marafiki zako wote link ya makala hii ili nao wajifunze.

Na tuendelee kuwezeshana, ili kwa pamoja tufikia mafanikio makubwa.

SOMA NA HII PIA; Unaweza Kupata Chochote Unachotaka Kwa Kufanya Kitu Hiki Kimoja.

TAMKO LANGU;

Najua ya kwamba mafanikio yangu yanategemea sana mafanikio ya watu wengine. Kuanzia sasa nitahakikisha wale wanaopokea huduma zangu wanafanikiwa kwa kiasi kikubwa ili nao waniwezeshe mimi kufanikiwa. Hii ni dunia ya kuwezeshana, nitawezesha ili na mimi niwezeshwe.

NENO LA LEO.

You can have everything in life you want, if you will just help enough other people get what they want.

– Zig Zigler

Unaweza kupata chochote unachotaka kwenye maisha yako, kama utawasaidia watu wengi zaidi kupata kile wanachotaka.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.