Kitabu MIDAS TOUCH ni kitabu ambacho kimeandikwa na wajasiriamali wakubwa wawili wa nchini marekani. Wajasiriamali hawa ni ROBERT KIYOSAKI na DONALD TRUMP. Kitabu hiki kinaelezea misingi mikuu mitano ya ujasiriamali ambayo inawatofautisha wajasiriamali wanaofanikiwa na wale ambao wanashindwa. Misingi hii mitano inafananishwa na vidole vitano vya mkono na hivyo mjasiriamali anayekuwa na misingi hii mitano, kila atakachoshika kitageuka kuwa dhahabu. Ndio maana jina la kitabu limeitwa midas touch yaani mshiko ambao unageuza kitu chochote kuwa dhahabu.

Mambo makuu matano yaliyoongelewa kwenye kitabu hiki ni kama ifuatavyo;

Moja; ambalo linaendana na kidole gumba ni TABIA NJEMA NA IMARA. Hii ina mchango mkubwa sana kwa mafanikio ya mjasiriamali yeyote, kila kitu kinategemea tabia yake.

Mbili; ambalo linaendana na kidole kinachofuatia baada ya kidole gumba ni UMAKINI AU MKAZO(FOCUS). Hapa ni kupeleka nguvu zote kwa kile ambacho unafanya na hivyo kuweza kupata matokeo mazuri. Wajasiriamali wenye mafanikio wana umakini mkubwa kwenye kile wanachofanya.

Tatu; ambalo linaendana na kidole cha katikati ni SIFA/JINA LA BIASHARA(BRAND). Wajasiriamali wanaofanikiwa ni wale ambao wanajenga sifa nzuri sana kwa biashara zao na pale jina lao linaposikika watu wanajua ni nini hasa kinaongelewa.

Nne; ambalo linaendana na kidole cha pete ni MAHUSIANO. Wajasiriamali wenye mafanikio makubwa ni wale ambao wana mahusiano mazuri sana na wale wanaowazunguka. Na wanaowazunguka ni wateja, wabia, wafanyakazi na kadhalika.

Tano; ambalo linaendana na kidole kidogo ni VITU VIDOGO LAKINI MUHIMU. Wajasiriamali wenye mafanikio makubwa ni wale ambao wanazingatia kufanya vitu ambavyo vinaonekana ni vidogo sana, lakini ni muhimu sana kwenye ukuaji wa biashara. Vitu hivi ni kama kuwajali zaidi wateja, kuboresha biashara zao na kadhalika.

Karibu sasa tushirikishane mambo 20 muhimu niliyojifunza kwenye kitabu hiki kinachoitwa MIDAS TOUCH.

1. Kuna roho fulani ya ujasiriamali. Roho hii inamwezesha mjasiriamali kuwa na ndoto kubwa, kuzifanyia kazi, kushinda, kushinda na kushinda tena na tena. Roho hii ndio inawatofautisha wajasiriamali wanaofanikiwa na wale wanaoshindwa. Pia inawatofautisha wale wanaotamani kuwa wajasiriamali na wale wanaokuwa wajasiriamali kweli.

2. Nguvu ya kutengeneza ajira sasa ipo kwa wajasiriamali. Serikali haziwezi tena kutengeneza ajira za uhakika. Wajasiriamali wenye mafanikio ndio pekee wenye uwezo wa kutengeneza ajira nyingi. Dunia inahitaji wajasiriamali wengi sana, ili kuweza kutengeneza ajira nyingi. Ndio maana ni muhimu sana wewe kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio.

3. Kuna vitu vitatu vinavyowazuia wengi kuingia kwenye ujasiriamali; cha kwanza ni ukosefu wa mtaji, cha pili ni ukosefu wa uzoefu wa ujasiriamali, na cha tatu ni kukosa tabia nzuri na imara za ujasiriamali. Katika sababu hizo tatu, sababu ya tatu ambayo ni kukosa tabia nzuri na imara za ujasiriamali ndio inayowazuia wengi kufanikiwa kupitia ujasiriamali.

4. Japokuwa kila mtu angependa kuwa mjasiriamali, sio kila mtu yupo tayari kuwa mjasiriamali. Sio kila mtu anaiweza safari ya ujasiriamali, hasa ujasiriamali wa mafanikio makubwa. Njia hii ni ngumu na inahitaji kutoa kafara(sucrifice). Kuna njia nyingine rahisi kwa wengi, ila ujasiriamali unahitaji waliojitoa kweli.

5. Wajasiriamali wanahitaji kufanya kazi kwenye mfumo wa masaa 24 kwa siku, siku saba za wiki hasa mwanzoni mwa biashara zao. Wanahitaji kufanya kazi kwa muda mrefu na wakati mwingine bila hata ya malipo. Hapa ndipo msingi imara wa ujasiriamali unapojengwa. Na wachache sana wanaweza kujenga msingi huu ndio maana wengi wanaishia kushindwa.

6. Kile ambacho hukijui ndio kinachokwenda kuua biashara yako. sababu namba moja kwa nini biashara nyingi zinazoanzishwa zinakufa ni kukosa maarifa muhimu ya biashara. Watu wengi wamekuwa wakiingia kwenye biashara kwa kuiga na kuziendesha kwa mazoea. Hii ni hatari kubwa sana. Kile ambacho hukijui, yale maarifa ambayo huna, zile mbinu unazokosa ndio zitakazochangia biashara yako kufa. Kujifunza ni muhimu sana.

7. Kwenye mfumo rasmi wa elimu, kukosea ni dhambi kubwa sana, na unapewa adhabu kubwa. Hivyo kila mwanafunzi anajitahidi asifanye makosa mengi. Kwenye ujasiriamali kukosea ndio kujifunza kwenyewe, hivyo badala ya kuogopa kufanya makosa, unahitaji kufanya makosa mengi na mapema ili uweze kujifunza haraka na kusonga mbele.

8. Wajasiriamali wenye mafanikio wanajua kuna kupata na kusoka, na wanajua kuna wakati wanapata na kuna wakati wanakosa, hawawezi kuwa kati kati. Kinachowatofautisha wajasiriamali wenye mafanikio na wanaoshindwa sio kupata au kukosa, bali wanavyozichukulia hali hizi za kupata na kukosa. Mwenye mafanikio anapokosa anaendelea kuweka juhudi, anayeshindwa anapokosa anakata tamaa na kuacha.

9. Umakini na kuzingatia jambo moja ni muhimu sana kwa wajasiriamali. Wajasiriamali wanaweza kuwa na mambo mengi sana wanayohitaji kuyafanya, lakini sio yote ambayo ni muhimu. Wajasiriamali wenye mafanikio ni wale wanaojua yale ambayo ni muhimu na kuyawekea mkazo na yale ambayo sio muhimu wanaachana nayo.

10. Kitu kikubwa kinachowapoteza watu na kushindwa kufikia mafanikio ni pale wanapofikiri kwamba maisha ni rahisi. Na hivyo kukimbilia kutafuta njia rahisi za kupata kile ambacho wanakitaka. Wanafuata ushauri ambao ni rahisi na kuweka malengo madogo na hatimaye kuishia kuwa na maisha ya hovyo.

11. Badala ya kuweka umakini kwenye kupata faida tu, wajasiriamali wenye mafanikio huangalia ni jinsi gani wanatoa huduma kwa wale wanaohitaji. Wanaangalia matatizo ambayo watu wanayo na kuona ni jinsi gani wanaweza kuyatatua. Kwa njia hii wanawasaidia watu wengi zaidi na hivyo kupata faida kubwa zaidi. Ila wale wanaoangalia faida tu, wanakosa fursa ya kutoa huduma kwa wengi wanaohitaji.

12. Heshima ya jina la biashara yako ni muhimu sana kwenye mafanikio ya ujasiriamali. Sifa za biashara yako zinasambaa pale ambapo unatoa huduma nzuri na zinazotatua matatizo ya watu. Wajasiriamali wenye mafanikio wanatumia muda na rasilimali kuhakikisha jina la biashara linakuwa kwenye akili za watu wengi zaidi.

13. Kama jina la biashara yako halijulikani na halina heshima yoyote basi wewe sio mjasiriamali bali ni mchuuzi. Na tatizo la kuwa mchuuzi ni kwamba huwezi kujenga biashara kubwa na yenye faida kubwa. Unapokuwa mchuuzi huwezi kupanga bei zako mwenyewe, utaweka bei sawa na wachuuzi wengine. Unakuwa kwenye ushindani mkali sana ambao unaweza kukupoteza.

14. Jina la biashara yako na heshima yake vitajengwa kwa uaminifu wako wewe kama mjasiriamali. Wajasiriamali wenye mafanikio wana uaminifu mkubwa sana. Wakiahidi kitu wanakitekeleza, na wanasema ukweli hata kama utapelekea wao kupata hasara. Wanahakikisha mteja anapata kile ambacho amelipia. Uaminifu huu unawajenga sana na watu wanawaambia wengine kuhusu biashara hizo.

15. Ni lazima ujue kwamba biashara yako haiwezi kumridhisha kila mtu. Wajasiriamali wenye mafanikio wanajua wateja wa biashara zao ni watu wa aina gani na hivyo kuwahudumia kulingana na mahitaji yao. Wajasiriamali wasiokuwa na mafanikio hufikiri kila mtu ni mteja wao na hivyo kujikuta wanashindwa kutatua tatizo maalumu. Wajue hasa wateja wako na wapatie huduma stahili kwao, utajenga sana jina lako.

16. Ni lazima wewe kama mjasiriamali uamue unataka kufahamika kwa lipi. Ni kitu gani ambacho unafanya kwa ubora na utofauti sana ambacho wateja wako wanaweza kunufaika nacho sana. Kwa kujua kitu hiki kutakuwezesha kujenga jina lako sana. Wajasiriamali wote wenye mafanikio kuna kitu fulani ambacho wanajulikana kupitia kitu hiko.

17. Ushirikiano ni muhimu sana kwenye mafanikio ya biashara yoyote ile. Wajasiriamali wenye mafanikio makubwa ni watu wa watu. Wanajua vizuri kuendana na watu tofauti tofauti na wanajua watu ndio msingi wa biashara. Unapokuwa mjasiriamali ni lazima utakutana na watu, ambao hata usingependa kukutana nao. Jinsi unavyoweza kujenga mahusiano mazuri na watu wengine ndivyo kutakuwezesha kufanikiwa.

18. Unapofanya biashara ya ubia unahitaji kuwa makini sana kabla hujaingia kwenye ubia. Na unapochagua mtu wa kuwa na ubia nae kwenye biashara, unahitaji kuwa makini sana kama unavyochagua mtu w akufunga naye ndoa. Hii ni kwa sababu matatizo ya mbia mmoja yanaweza kuharibu biashara na kuvunja kabisa mahusiano yaliyokuwepo.

19. Kama mtu humwamini, usiingie naye kwenye ubia wa kibiashara. Kama mtu sio mwaminifu kwenye maisha yake ya kawaida usiingie naye kwenye ubia wa kibiashara. Usifikiri kwamba mtu atabadilika kwa sababu amekuambia atabadilika. Anaweza kuvumilia mwanzoni, lakini baadae mambo yatakapokuwa magumu sana au yatakapokuwa mazuri sana, atarudia tabia zake na atakuwa mzigo mkubwa kwako na anaweza kupelekea biashara mliyoijenga kwa nguvu kufa.

20. Kuna vitu vinavyoonekana ni vidogo sana lakini vina umuhimu mkubwa sana kwenye ukuaji wa biashara. Wajasiriamali wenye mafanikio wanavijua vitu hivi na wanaviwekea mkazo sana. Vitu hivi ni kama kuhakikisha mteja anapata huduma bora sana, kutatua changamoto za wateja, kuongeza ubora kila mara na kujifunza zaidi kuhusu biashara unayofanya. Wajasiriamali wasio na mafanikio hupuuza vitu hivi vidogo vidogo na kushindwa kufanikiwa huku wasijue nini tatizo.

Hayo ni yale muhimu sana kutoka kwenye kitabu hiki ambayo unaweza kuanza kuyafanyia kazi na ukawa mjasiriamali mwenye mafanikio makubwa. Kumbuka dunia inahitaji wajasiriamali wengi wenye mafanikio, na wewe ni mmoja wao, hivyo chukua hatua.

Jambo muhimu zaidi la kukumbuka;

Unapohitaji kujua ni nini unachotaka ili kufanikiwa angalia mkono wako na jikumbushe haya;

Kidole gumba; tabia nzuri na imara, kama uvumilivu, uadilifu.

Kidole kinachofuatia; umakini na kufanya yale ambayo ni muhimu.

Kidole cha kati; kujenga jina la biashara yako, liwe kubwa na linaloheshimika

Kidole cha pete; kujenga mahusiano bora na wale wote wanaohusika na biashara yako.

Kidole kidogo; kujali mambo ambayo yanaonekana ni madogo lakini ni muhimu sana kwa biashara yako.

Nakutakia kila la kheri kwenye kufanyia kazi haya uliyojifunza. Nina hakika utakuwa mjasiriamali bora sana wa kiazi hiki.

Rafiki na kocha wako,

Makirita Amani.