Katika jambo lolote lile, yule anayeongea sana ndiye anayepoteza.
Iwe ni kwenye kufikiana makubaliano au hata kwenye biashara, anayeongea sana anapoteza.
Anayeongea sana anapoteza nafasi nzuri ya kuweza kunufaika zaidi. Anakosa nafasi ya kujua kwa undani hasa.
Hii ni kwa sababu anayeongea sana anakosa nafasi ya kusikiliza kwa makini, na kuangalia pia. Anayesikiliza kwa makini anajua kwa undani. Kama ni tatizo analielewa hasa na kama ni makubaliano anajua udhaifu uko wapi na anaweza kuutumiaje.
Wakati huo anayeongea sana anaonesha udhaifu wake, na kukosa nafasi yakufikiri kwa kina.
Tumewahi kujifunza tena hapa ya kwamba umepewa masikio mawili na mdomo mmoja kwa sababu maalumu kabisa. Ya kwamba usikilize zaidi ya unavyoongea. Sasa wewe ukitaka kuongea zaidi ya unavyosikiliza, ni lazima upoteze.
Leo tuongeze tena ya kwamba umepewa masikio mawili na macho mawili, ili usikilize na kuangalia zaidi. Na umepewa mdomo mmoja ili uongee kidogo.
Na uzuri ni kwamba ukisikiliza kwa makini na ukaangalia vyema, utajua vizuri na hutahitaji kuongea sana. Kwa sababu utaongea yale ambayo ni muhimu tu, na utaweza kupata kile unachotaka.
SOMA; Una Mdomo Mmoja Na Masikio Mawili Kwa Sababu Hii Kubwa.
TAMKO LANGU;
Najua ya kwamba yule anayeongea sana ndiye anayepoteza. Hivyo kuanzia sasa nitapunguza kuongea na badala yake nitasikiliza kwa makini na kuangalia kwa makini pia. Na itakapofika wakati wangu wa kuongea, nitaongea machache ambayo ni muhimu sana. Kwa njia hii nina uhakika wa kupata kile ambacho ninataka.
NENO LA LEO.
“We have two ears and one tongue so that we would listen more and talk less.” –Diogenes
Tuna masikio mawili na ulimi mmoja ili tuweze kusikiliza zaidi ya tunavyoongea.
Kuwa msikilizaji zaidi ya mwongeaji, utajifunza mengi sana kwenye kusikiliza.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.