Waswahili wanasema usichokijua ni sawa na usiku wa giza.

Umewahi kutafakari na kujiuliza maana halisi ya kauli hiyo?

Kama hujawahi basi tuanzie hapo. Na tuanze na usiku wa giza. Usiku wa giza ni nini? Giza ni nini hasa? Kama umekuwa unasoma hapa kila siku tayari jibu unalo. Kwamba giza sio kitu, bali ni ukosefu wa mwanga. Si tunakubaliana kwa hilo? Kwamba sehemu yenye giza ukipaleka mwanga giza linapotea kabisa.

Hivyo giza linaweza kukutisha, giza linaweza kukupa hofu, lakini giza sio kitu, ni ukosefu wa mwanga.

Hapa ndipo wahenga walipopata ufanano na kitu usichokijua. Unaweza kuogopa sana, unaweza kuona utashindwa kwa sababu ya kitu fulani ambacho hukijui. Lakini usichokijua sio kitu, bali ni kukosekana kwa ujuzi. Hivyo kuondokana na hili ni kujifunza. Ukijifunza unaondokana na ile hali ya kutokujua, unaondokana na hofu na mara moja unaanza kujiamini na kuweza kuchukua hatua.

Haya na tuanze, baada ya kukumbushana hayo ya wahenga.

Kitu ambacho kinakurudisha nyuma mpaka sasa, kitu ambacho kinakuzuia usifikie mafanikio makubwa. Kitu ambacho kinakufanya uanguke hata unapojitahidi, ni kile ambacho hukijui.

Usichokijua ni kikwazo kikubwa sana kwako kuweza kufika mbali. Na kama tulivyosema, usichokijua sio kitu, bali ukosefu tu wa ujuzi huo. Lakini bado wengi hawatafuti ujuzi huu.

Kuna vitu vingi sana unavyotakiwa kujua kuhusiana na kile unachofanya. Iwe ni kazi ya kitaalamu, iwe ni biashara na pia hata maisha kwa ujumla. Na kadiri unavyojua vitu hivi ndivyo unavyoepuka kufanya makosa ambayo yanakurudisha nyuma.

Unajuaje vitu hivi vingi sana?

Kwa kujifunza kila siku, ndio kila siku, la sivyo unabaki nyuma.

Unahitaji kujifunza kila siku, hili ni hitaji la msingi sana la wewe kufanikiwa. Kama hufanyi hivi kila siku, unachagua njia ya kupotea, na kwa njia hiyo mafanikio utaishia kuona kwa wengine.

Jifunze kila siku, jifunze kuhusu kile unachofanya, jifunze kuhusu mafanikio, jifunze kuhusu kuishi maisha bora, jifunze jinsi ya kwenda na watu vizuri, jifunze jinsi ya kupambana na changamoto na mengine mengi.

SOMA; Ndio, hakuna jipya, lakini bado unahitaji kujifunza “KILA SIKU”.

TAMKO LANGU;

Nimejua kinachonirudisha nyuma ni kile ambacho sikijui. Na nimejua njia ya uhakika ya kujua vitu vingi ninavyohitaji kujua ni kujifunza kila siku. Kwa kujifunza vitu vidogo vidogo kila siku najiweka kwenye nafasi nzuri ya kuwa na maisha bora. Kuanzia sasa, nitahakikisha siku haipiti bila ya kujifunza kitu kipya.

NENO LA LEO.

If a man empties his purse into his head, no man can take it away form him. An investment in knowledge always pays the best interest.
– Benjamin Franklin

Kama mtu atamwaga mfuko wake wa fedha kwenye kichwa chake, hakuna mtu anayeweza kumwibia mfuko huo wa fedha. Uwekezaji kwenye elimu ndio uwekezaji pekee unaolipa riba kubwa sana.

Jifunze kila siku.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.