Kama ungeweza kuziona fursa haraka kama unavyoyaona makosa ya wengine, basi ungekuwa mbali sana.

Kama ungekuwa unachukua hatua haraka kama unavyochukua kuwakosoa wengine, maisha yako yangekuwa bora sana.

Lakini hufanyi hivyo, kwa sababu labda hujajua jinsi ya kufanya, na nitakushirikisha hapa.

Urahisi wa kuona makosa ya wengine.

Ni rahisi sana kuona makosa ya wengine. Hii ni kwa sababu kwa tulivyozoea, tunaona mabaya haraka sana. Hii ni kwa sababu tunayatafuta mabaya hayo na kwa sababu unachotafuta utakipata, basi huwa tunayapata kiurahisi sana makosa ya wengine.

Kama unataka kuziona fursa iwe rahisi kama unavyoyaona makosa ya wengine, basi anza kutafuta fursa kila mahali. Kila unachofanya, kila unapokuwa, kila mazungumzo unayofanya, jiulize ni fursa gani iko hapa ambayo bado sijaiona. Jiulize ukiwa bado eneo hilo hilo.

Kwa kujiuliza swali hilo mara kwa mara kutakusukuma wewe ufikiri zaidi na utaanza kuziona fursa kila utakapokuwepo.

Urahisi wa kuwakosoa wengine.

Ni rahisi sana kukosoa watu wengine kwa sababu ni rahisi. Haihitaji utumie nguvu za ziada katika kukosoa, na hata unapokosoa sio wewe ambaye una mzigo mzito wa kufanyia marekebisho. Na hata hivyo huenda hujui ugumu aliokutana nao mtu mpaka hapo alipopita. Hivyo ni rahisi sana kusema, hapo singefanya hivyo, angefanya hivi.

Unaweza kuitumia hii kuweza kuchukua hatua kwenye zile fursa unazoziona. Kwenye kila fursa unayoiona ambayo inaendana na wewe, jiulize ni sehemu gani rahisi ambayo unaweza kuanzia kuchukua hatua. Tafuta sehemu rahisi sana au kitu kidogo sana unachoweza kuanza kufanyia kazi, na anza mara moja.

Unaweza kuwa umepanga kufanya makubwa sana. Sasa yagawe kwenye visehemu vidogo vidogo sana ambavyo vitaonekana rahisi kufanya na anza kuvifanya mara moja.

Kuwa makini kuziona fursa kama unavyoyaona makosa ya wengine kirahisi na chukua hatua ya kuzifanyia kazi fursa hizo haraka kama unavyoweza kumkosoa mtu haraka.

SOMA; Huoni Fursa Za Mafanikio Kwa Sababu Hii Kubwa.

TAMKO LANGU;

Nimejua ni rahisi kwangu kuyaona makosa ya wengine na pia ni rahisi kuchukua hatua ya kuwakosoa. Lakini sio rahisi kwangu kuziona fursa na kuanza kuzifanyia kazi. Kuanzia sasa nitakazana kuzioana fursa zaidi na nitatafuta sehemu ndogo kabisa ya kuweza kuchukua hatua. Kila wakati na kwa kila jambo nitajiuliza ni fursa gani ipo hapa, na nikishaipata nitajiuliza ni sehemu gani ndogo kabisa naweza kuanzia kuitekeleza fursa hii.

NENO LA LEO.

The reason why we so often judge correctly concerning the faults of others, is because we are always in search of them.

NORMAN MACDONALD

Sababu kubwa kwa nini tunaweza kuwahukumu wengine kwa usahihi kuhusu makosa yao, ni kwa sababu mara zote tunatafuta makosa ya wengine.

Anza sasa kuzitafuta fursa kila mahali na utazioana nyingi sana, pamoja na kuweza kuchukua hatua haraka.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.