Mambo 20 Niliyojifunza Kutoka Kwenye Kitabu Cha Midas Touch.

Habari ndugu msomaji wa makala za uchambuzi wa vitabu. Wiki hii tunajifunza kutoka kwenye kitabu kinaitwa Midas Touch kilichoandika na waandishi wawili ambao ni maarufu na waliofanikiwa sana, mmoja ni bilionea na mwingine ni milionea. Waandishi hao ni Donald Trump (Bilionea) na Robart Kiyosaki (Milionea). Kitabu kinafundisha mambo mengi sana ambayo kwa mjasiriamali yeyote hapaswi kuyakosa. Pia kitabu hiki kinatoa sababu kwa nini wajasiriamali wengi hawafikii mafanikio na kwa nini wachache tu ndio wanaofanikiwa. Mafundisho ya kitabu hiki yamegawanywa katika sura kuu tano, na kila sura imezungumzia sifa moja. Pia waandishi wamefananisha sifa hizo za mjasiriamali kufanikiwa kama vidole vya mkono. Kila kidole kikiwakilisha sifa moja. Akianzia na kidole gumba. Kidole gumba amekipa sifa ya uwezo au uimara wa tabia (strength of character), Kidole kinachofuatia ambacho tunapenda kunyoosha, anakipa sifa ya FOCUS. Kidole cha katikati kinawakilisha sifa ya Brand, kidole cha pete kinawakilisha sifa ya Mahusiano katika biashara, na kidole kile kidogo kinawakilisha mambo madogo yenye tija (small things that count). Ukishika kitabu hiki hutatamani kukiweka chini. 

 
Karibu tujifunze
1. Wajasiriamali ndio wanaoweza kutengeneza ajira nzuri. Serikali haiwezi kutengeneza ajira. Ni wajasiriamali pekee ndio wanaoweza kufanya hivyo, maana wao ndio wenye uwezo wa kuona kesho na kuthubutu kuchukua vihatarishi (take risk) bila kujali kushindwa.
2. Shule na Vyuo havitengenezi wajasiriamali. Shule zimetengenezwa ili kuzalisha waajiriwa. Maana hata wanaowafundisha ni waajiriwa na sio wajasiriamali. Utakua unafundishwa na Profesa wa entrepreneurship lakini hana hata kibada cha MPESA. Hii itakufanya pia na wewe ukose ujasiri, maana utaona kama yule anayekufundisha pamoja na kwamba anajua mambo mengi kuliko wewe lakini ameshindwa wewe je utaweza? Kumbuka wanafunzi wanawaamini waalimu wao zaidi kuliko wanavyowaamini wazazi wao au ndugu na marafiki zao.
3. Zile zama za viwanda (industrial age) zimefikia mwisho. Hizi ni zama za taarifa (Information Age) na wenye taarifa sahihi ndio wanaofanikiwa. Zama za viwanda, ulikua unaambiwa soma ufaulu vizuri halafu upate kazi inayolipa vizuri. Ila sasa mambo yamebadilika, unaweza ukamaliza na daraja la kwanza (First Class) na ukazunguka na bahasha kutafuta kazi bila mafanikio. Aa ukaishia kwenye kazi za kawaida sana. Wenye taarifa sahihi ndio wanaoongoza dunia.
4. Wajasiriamali lazima wajifunze jinsi ya kuhimili msongo wa mawazo na hofu. Stress na hofu vinapaswa kumhamasisha mjasiriamali kuwa mbunifu zaidi, kujifunza kwa haraka, kuongeza ufahamu wake kuhusu watu na biashara. Kwa maneno mengine mjasiriamali anapaswa kua mtu wa kujifunza vitu vipya kila wakati, mawazo na ubunifu mpya bila kujali anapitia kwenye stress au la.
5. Ukuaji wa biashara unategemea na ukuaji wa mjasiriamali. Kama mjasiriamali ukidumaa na biashara itadumaa. Lazima uwe mtu wa kuongezeka katika maarifa na ufahamu. Jifunze vitu vipya, soma vitabu na majarida ya biashara unayofanya. Tafuta watu waliofanikiwa katika hilo eneo pata ushauri kwao, na tekeleza unachoshauriwa.
6. Kuuza (selling) ni juzi namba moja ambao kila mjasiriamali anapaswa kua nao. Mjasiriamali yeyote itambidi auze bidhaa au huduma kwa wateja, pia anapaswa kuuza ile mission yake kwa wafanyakazi wake ili wafanye kazi kwa hamasa, pia mjasiriamali anapaswa awe na uwezo wa kuuza mawazo yake kwa wawekezaji, ili waone thamani ya kuwekeza fedha zao. Mjasiriamali yeyote anayeshindwa kuuza lazima atasumbuka sana kifedha.
SOMA; Jinsi Unavyoweza Kuondokana Na Changamoto Za Kuendesha Biashara Na Kuweza Kufikia Mafanikio Makubwa.
7. Focus ni kule kufuata jambo moja mpaka limefanikiwa kikamilifu. Mtihani mkubwa wa wajasiriamali wengi ni kua na focus. Je unaweza kufuatilia jambo moja mpaka lifanikiwe? Hata liwe gumu kiasi gani, je unaweza kuendelea kua focused kwenye jambo ambalo ni sahihi pamoja na ugumu wake? Wengi huishia kusema, “hii haifanyi kazi bana” na kutupilia mbali na kwenda kwenye jambo lingine rahisi zaidi. Without focus, it’s just about impossible to be successful at anything.
8. Maskini na watu wa daraja la kati wanaweka fedha zao benki kuzitunza huko, matajiri wao wanazitumia kuendelea kua matajiri. Wakati maskini na watu wa daraja la kati wakiogopa kufanya biashara na kuhifadhi fedha zao benki, benki hizohizo zinafanyia hizo hela biashara kwa kuwapa matajiri mikopo na kuwekeza kwenye biashara zao. Hivyo hivyo hata kwa mifuko ya hifadhi ya jamii kama NSSF, PPF, LAPF n.k, hivi unadhani mfanyakazi anapokatwa makato ya NSSF au PPF, hua yanawekwa tu hapo mpaka siku unapokuja kuchukua? Hapana, hizo fedha ndizo zinazofanyia biashara kubwa kubwa. Hizo fedha ndio zinazojenga majengo makubwa ya biashara. Cha ajabu ni kwamba wengine ndio wanaonufaika, lakini wewe utapewa ile hela yako tu uliyoweka, wakati faida walishakula wengine. Somo hapa ni kwamba wakati wewe ukiogopa kufanya biashara matajiri ndio wanazichukua na kuwekeza kwenye biashara zao. Mara nyingi sana matajiri hua hawatumii fedha zao, wanatumia fedha za watu wengine, hasa za maskini na watu wa daraja la kati.
9. Kabla hujaanza biashara au kampuni yako, pata kwanza uzoefu mahali. Unaweza kuajiriwa mahali kwa muda, hasa kwenye kampuni inayofanya vizuri. Fanya kazi kujifunza na sio kuangalia mshahara. Unapoweka lengo lako kwenye mshahara tu, unashindwa kujifunza. Ukiwa ndani ya kampuni ni rahisi kujifunza kuliko ukiwa nje. Jifunze utendaji kazi wa hiyo kampuni, wanawezaje kufanikisha mambo na kwa nini pia mambo yanaenda vibaya. Ukishapata uzoefu endelea na mission yako.
10. Mjasiriamali aliyefanikiwa lazima uheshimu brand. Ukiwa mdanganyifu kwa kuiba brand za wengine ujue ipo siku na ya kwako itaibiwa. Kutengeneza brand ikaingia sokoni na kufanya vizuri sio kazi ndogo. Sasa wajasiriamali wengi hasa wale wanaoibukia, hudhani ni jambo jepesi tu la kuchukua na kubandika tu. Brand ni utambulisho wa biashara, ni uhai wa biashara. Mfano brand kama AZAM, Coca-Cola, Google, Adidas, Vodacom na nyingine nyingi, juhudi kubwa sana zimetumika kufikia hapo walipo. Brand zinalindwa sana. Mfano mtu aanzishe kiwanda chake cha soda halafu aziite Coca-cola na aziingize sokoni bila kufuata utaratibu wa kisheria kuwasiliana na mmiliki wa brand ya Coca-cola, yaani lazima atashitakiwa na atalipa faini za kutosha. Hivyo ili ufanikiwe kwenye ujasiriamali ni Lazima uheshimu brand ya mtu mwingine.
11. Kuna tofauti kati ya biashara na brand. Brand ndio uhai wa biashara, brand ni zaidi ya biashara. Brand inathamani kubwa kuliko biashara yenyewe. Kuna wengi wanadhani brand ni logo, sio kweli, brand sio logo ya kampuni. Brand ni ile ahadi ya mjasiriamali kwa wateja wake. Brand ya kweli inaanzia nafsini/moyoni mwa mjasiriamali na kuiunganisha na nafsi ya wateja wake. Ni mahusiano na wateja zaidi ya kufanya manunuzi. If your business is not a brand, it is a commodity.
SOMA; Sababu Tano Kwa Nini Biashara Nyingi Zinazoendeshwa Na Waajiriwa Huwa Zinakufa.
12. Moja ya sababu ambazo zinawafanya wajasiriamali wengi kushindwa kuzikuza biashara zao kwenda kwenye brand ni kwa sababu wanachukulia fedha kama ndio kitu muhimu kuliko brand. Hivyo ni rahisi kufanya chochote ili tu wapate fedha. Mtu yuko tayari adanganye hata kama ukweli uko wazi ili tu aingize fedha. Kufanya hivyo ni kujinyonga mwenyewe. Utanufaika kwa muda mfupi sana.
13. Biashara ya kweli ni ile inayotatua tatizo fulani na kuyafanya maisha kua bora zaidi. Je jiulize biashara unayofanya inatatua tatizo gani katika jamii? Kama unachokifanya hakinufaishi wengine, basi hakina maana. Kama biashara yako ipo kutengeneza fedha pekee basi ujue, biashara yako ina maisha mafupi sana. A true business only exists to solve a problem and to make life better.
14. Ili kufahamu ni nini kitaifanya biashara yako iwe na maana, kaa chini fikiri na jiulize maswali yafuatayo:
· Ni tatizo gani unataka kutatua?
· Kwanini ni tatizo?
· Ni nini kinasababisha hilo tatizo?
· Je ikitokea biashara yako inakufa kesho, ni nini dunia itakua imepoteza?
· Ni nini kinakufanya udhani kwamba unaweza kutatua hilo tatizo?
· Ni jinsi gani bidhaa au huduma yako itatatua hilo tatizo?
· Ni jinsi gani bidhaa au huduma yako itayafanya maisha ya wateja wako kua bora zaidi?
· Ni nini hasa unadhani wateja wako wanakihitaji kutoka kwenye kampuni kama hiyo yako?
Chukua muda kujiuliza hayo maswali. Tafuta rafiki yako mmoja mwambie akuulize haya maswali mpaka uwe umeyaelewa vizuri. Rudia tena na tena huu mchakato wa kujiuliza haya maswali mpaka umeelewa haswa ni nini hicho kinakufanya uwe na maana.
15. Kuwa mkweli kwako binafsi (Be true to yourself). Huwezi kuwa kila kitu kwa kila mtu. Huwezi kumfanya kila mtu kuwa na furaha. Usitafute kumfurahisha kila mtu, maana hakuna siku watu wote wataridhika. You have to decide what it is you want to be known for. You have to be true to yourself. You have to please yourself first.
16. Kutengeneza brand ni sawa na kutengeneza ghorofa, ili ghorofa liende juu zaidi, msingi kwanza unabidi uingie chini zaidi ili kuweza kubeba ghorofa hilo. Hivyo hivyo ili uwe na brand kubwa yakupasa uwe na msingi imara kwanza. Brand inapokua kubwa inaleta usalama wa kazi, inakua ni rahisi kua na wafanyakazi wazuri. Mtu anayefanya kazi kwenye kampuni yenye jina kubwa anajihisi fahari na kujiona salama zaidi kuliko Yule anayefanya kwenye kampuni yenye jina dogo.
17. Ukosefu wa elimu ya fedha (financial education) ni moja ya visababishi vya ukuaji wa tabaka kati ya matajiri na masikini, na watu wa daraja la kati watapungua, wengi wataangukia kwenye kundi la maskini baada ya muda.
18. Ushirika kwa kibiashara (business partnership) ni kama ndoa, unaweza kua mzuri au mbaya. Unapaswa uwe makini sana tena sana pindi unapotafuta mshirika wa kibiashara, yaani unapotafuta mshirika wa kibiashara ni kama vile unatafuta mke au mume. Umakini unahitajika. Kwa vile mtu ni rafiki yako haimaanishi anafaa kuwa partner wako kwenye biashara. Wengi sana ni wazuri kabla ya kufanikiwa, ila pale mafanikio yanapoanza watu hao hubadilika, na tabia zao zilizofichika huanza kujionyesha. A business partnership is like a marriage.
SOMA; USHAURI; Hatua Za Kuchukua Pale Mwenza Wako Anapokuwa Chanzo Cha Biashara Zako Kufa.
19. Matajiri wa kweli ni watu wakarimu. Tofuti kabisa na imani za watu wengi wanavyoamini, matajiri sio watu wenye tamaa. Wengi hudhania kwamba matajiri ni watu wenye tamaa. Utajiri wao wanaupata kwa sababu wanahudumia watu, yaani karama au zawadi walizopewa na Mungu wanawashirikisha wengine. Jiulize nini hicho ambacho ni cha kipekee Mungu amekupa ili kuishirikisha dunia? Je unacho kitu cha kuipa dunia? Kabla hujafikiria utanufaikaje kutoka kwa watu, fikiri kwanza watu watanufaikaje kutoka kwako. Hivi ndivyo matajiri wanavyofikiri. Roho ya ukarimu.
20. Vitu vidogo 4 unavyopaswa kuvifanya au kujihoji kabla hujafikiria kua tajiri au kumiliki biashara kubwa
· Je Wewe ni mtu mkarimu?
· Je unacho kitu cha kuipa dunia?
· Je unayo mskumo wa dhati (dedication and drive) wa kuijenga biashara yako kutoka biashara ndogo kwenda kwenye hatua ya biashara kubwa na hata kuwa mwekezaji?
· Je upo tayari kufanya maisha ya watu wengine yafanikiwe? Yaani upo tayari kuwatajirisha na wengine?
Kama majibu yako ni ndio basi ujue unayo tabia ya msingi (foundational character) kwa ajili ya kua mjasiriamli aliyefanikiwa sana
Kama utahitaji kitabu hiki waweza kukikipata kwa kuwasiliana na mimi kupitia mawasiliano yangu hapo chini.
Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s