Unapoangalia maisha ya wengine, kuna vitu vingi sana unavyoviona kwa nje.
Na wakati mwingine unaweza kutamani vitu hivyo vingekuwa kwako pia.
Au unaweza kuona mtu huyo ana maisha bora sana kuliko maisha yako wewe.
Lakini hapo umeona kwa nje tu, hujui upande wa pili ni kitu gani kinachoendelea.
Mara zote kile unachokiona kwa nje kwa mtu, ni kile ambacho anataka wewe uone.
Na katika dunia hii ya mitandao ya kijamii, kila siku utaona picha nzuri zinawekwa kwenye mitandao hii na watu wakiandika jumbe nzuri kuonesha ni jinsi gani maisha yao ni bora. Huwezi kukuta mtu akiandika makosa anayofanya kila siku, au changamoto nyingine kubwa anazopitia.
Kwa wewe kuona mambo hayo ya juu juu na ya nje, unaweza kuona wenzako wana kila kitu wanachokitaka.
Lakini huo sio ukweli, kila mtu kuna changamoto nyingi anazopitia, kuna vikwazo anavyopambana navyo na pia kuna makosa ambayo anayafanya. Lakini mara nyingi huwezi kuona yote haya. Wewe utaona kile anachotaka wewe uone. Na hivyo kujihukumu wewe kwa picha hizi za juu juu sio kujitendea haki.
Usitumie maisha ya wengine kujilinganisha au kujihukumu wewe, utakuwa unajidanganya. Kama hujayaishi maisha ya mwingine kwa undani, basi humjui mtu huyo. Unachojua ni kile ambacho anataka wewe uone, ukweli wa mambo sio huo.
SOMA; Kauli KUMI Za Marcus Aurelius Zitakazokufanya Uyaone Maisha Kwa Utofauti.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba vile ninavyoona kwa wengine ni sehemu ndogo sana ya maisha yao, tena ile wanayotaka nione. Najua kuna sehemu kubwa ambayo hawataki nione. Kuanzia sasa nitaacha kulinganisha maisha yangu na ya wengine kwa sababu siwezi kuwajua vizuri. Mimi nitakazana kuwa bora kwenye kile ninachofanya, na kupambana na changamoto zangu, kuvuka vikwazo vyangu na kujifunza kutokana na makosa ninayofanya.
NENO LA LEO.
“Be thankful for what you have; you’ll end up having more. If you concentrate on what you don’t have, you will never, ever have enough”
― Oprah Winfrey
Shukuru kwa kile ulichonacho, na utaendelea kupata zaidi. Kama utafikiri zaidi kuhusu vile ambavyo huna, kamwe hutakuja kupata vya kukutosha.
Angalia zaidi kile ulichonacho kwenye maisha yako, na sio kile ambacho wengine wanacho na wewe huna. Ni vigumu kujua undani wa maisha ya wengine.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.