Habari mpenzi msomaji wa Amka Mtanzania? Karibu tena katika makala yetu ya leo ambapo leo tutajifunza kuhusu maadui katika ndoa yako au uchumba wako.
Miongoni mwa matatizo mengi ambayo yanayowasumbua watu moja ni mapenzi lakini watu bado hawajagundua nini chanzo cha matatizo haya. Kuna watu wanateseka sana na kupata taabu katika uhusiano wao wa kimapenzi mpaka watu wengine wanaamua kuapa na kusema hawataki kusikia kitu kinachoitwa mapenzi hii ni baada tu ya kutendwa vibaya au kusalitiwa na mwenzi wake.

 
Katika safari ya mapenzi kuna mambo mawili ambayo ni uchumba na ndoa. Kabla hatujaanza kujua kiini cha matatizo ya ndoa au uchumba tuangalie kwanza nini maana ya ndoa na uchumba.
Uchumba ni mahusiano ya mwanzo kati ya mwanamke na mwanaume kabla ya kufunga ndoa. Huwezi kuingia kwenye ndoa bila kupitia uchumba hivyo basi uchumba ni daraja la kupitia kuelekea kwenye ndoa. Hapa katika uchumba watu wawili hao kila mmoja asipokuwa wazi kuonyesha vilema au kilema chake ndio chanzo cha matatizo katika ndoa. Kipindi hiki cha uchumba kama wapenzi mnatakiwa kuwa wawazi, kila mmoja amjue mwenzake amchunguze na kumjua vema na pia kuwekeana misingi ya kuishi falsafa moja katika maisha yenu. Kama mtu ana ugonjwa wa kurithi ni vema amwambie mwenzake kama atakupenda akupende na kilema chako.
SOMA; Viungo Vikuu Vitatu(3) Vya Furaha Ya Kudumu Kwenye Maisha.
Ndoa ni makubaliano halali kati ya mwanaume na mwanamke kuishi kama mke na muwe. Ndoa ni makubaliano ya watu wawili kuishi kama mke na muwe bila kushurutishwa na mtu yeyote. Hapa siyo kipindi cha kuchunguzana bali hapa ni kuishi maisha ya ndoa na kuyafurahia.
Sasa tuangalie maadui wakuu katika uchumba au ndoa yako.
Maadui wakuu katika ndoa yako ni kama ifuatavyo;
Maadui wa kwanza ni Nyinyi Wenyewe; usianze kumtafuta adui katika ndoa au uchumba wako kwanza jiulize na kujitafakari wewe mwenyewe kabla ya kuanza kumtafuta mchawi. Maisha ya ndoa au uchumba ni siri ya watu wawili sasa matatizo yanaanzia hapa kati ya wawili hawa kuanza kuanika hadharani mambo yao ya ndani baadaye mambo yanakwenda mrama huanza kulalamika na kumtafuta mchawi. Haitakiwi kueleza mambo yenu kwa watu hata kama ni mzazi wako kaeni chini nyinyi wenyewe kwanza msemezane nini tatizo. Kumbuka kuwa katika ndoa yenu au uchumba wenu waamuzi wa mwisho katika mambo yenu ni nyinyi wenyewe usikubali mtu wa pembeni awatawale au awaamulie mambo yenu.
Mnatakiwa kuishi maisha ya upendo, uaminifu na maisha ya kumpendeza Mwenyezi Mungu. Mchague kuishi maisha ya falsafa moja hii itawasaidia sana kuliko kila mmoja anaishi maisha ya falsafa tofauti ndani uhusiano wenu. Ukianza kumwelezea kila mtu matatizo yako ya ndani ni sawa na kujivua nguo na kutembea uchi wa mnyama. Watu hawapendi kuwaona wengine wakipendana mtapata majaribu mengi sana kwa watu lakini cha msingi kuwa na msimamo na malengo wala msiyumbishwe kama bendera kuweni imara sana muda mwingine shetani ni watu kwa sababu shetani anapitia katika nafasi za watu hivyo ni vema kuchukua tahadhari na watu ndio maana waswahili wanasema kikulacho kinguoni mwako.
SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Kijana Wa Kitanzania(kama una miaka kati 20 mpaka 30 soma hapa)
Maadui wa pili ndugu na marafiki; marafiki wa karibu ndio adui wako kabisa utampatia siri nyingi juu yenu lakini rafiki huyohuyo wa karibu ndio adui wako mkubwa. ‘’Jihadharini na maadui wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali’’ nukuu kutoka katika kitabu cha Biblia. Ndugu au marafiki watawafanya nyinyi mfarakane ili wao wacheke. Wakiona nyinyi mnapendana watatafuta mbinu na hila za kuwafanya mgombane. Kauli kama hizi ‘’ aaa! Wanajifanya wanapendana mbona wamegombana hawana lolote’’ hivyo marafiki na ndugu zenu mnapaswa mjihadhari nao sana msianze kutoa siri zenu kwa marafiki zenu.
Siri za mume na mke zibaki chumbani humohumo mkosoane humohumo. Usitoe siri zako za ndoa kwa rafiki hata awe rafiki wako wa namna gani hata muwe mmeshibana vipi ni sumu unaua uhusiano wako.
Mtu wako wa kwanza kumueleza matatizo yako ni mwenzi wako siyo mtu mwingine wa pembeni sasa cha ajabu mmeunganika kuwa kitu kimoja unaenda kumwambia mtu wa pembeni mambo yako ili iweje? Hapo ndio unaanza kujichimbia shimo.
SOMA; Hizi Ndizo Sababu 7 Zinazosababisha Msongo Wa Mawazo.
Hivyo basi, unatakiwa kujifunza mambo yanayohusiana na uchumba na ndoa kwa kusoma vitabu mbalimbali vinavyohusiana na mada tajwa, semina nakadhalika.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com au unaweza kutembelea tovuti yake www.actualizeyourdream.blogspot.com