Mpendwa rafiki,

Hakuna wito ambao utachagua wewe kuishi na ukakosa changamoto. Na hakuna maisha ambayo utakayotaka wewe kuishi usikumbane na changamoto. kila kitu kinaweza kuwa kizuri au kibaya kadiri ya mtazamo wako.

Nilishawahi kuandika katika miaka ya nyuma na katika moja ya vitabu vyangu kuwa adui wa kwanza katika mahusiano ya ndoa ni wana ndoa wenyewe. Wengi wanafanya uzembe na wanajikuta wanaanguka kijinga kabisa katika mahusiano yao halafu utashangaa wanasema ni shetani kampitia, tutaendelea kumsingia shetani mpaka lini? Kitu ambacho kipo ndani yako na umefanya kwa uzembe kabisa halafu unamtafuta adui mwingine katika maisha yako na kusingizia watu wengine.

Adui wa mtu ni mtu mwenyewe, hakuna kitu kibaya kama uko katika mahusiano ya ndoa halafu unakosa uaminifu. Wengine wanajidanganya eti waendelee kula starehe na wakishaingia katika maisha ya ndoa watakuwa waaminifu, hapa ni pagumu unawakuta ndiyo hao hao ambao wakishaingia katika ndoa wanavua ngozi yao ya kondoo na kuendelea na maisha yake ya kawaida. Hizi tabia za kijinga watu wanazitengeneza na kisha tabia zinakuja kuwatengeneza.

a7ca2-ndoa

Ujinga mkubwa wanaofanya baadhi ya wanandoa waliokosa uaminifu ni pale ambapo wako kwenye ndoa halali halafu bado wanaendelea kuwasiliana na x wake yaani mtu aliyekuwa na mahusiano naye kabla ya huyo aliye naye sasa katika maisha ya ndoa. Ni ujinga kweli, ulikula kiapo wewe mwenyewe utakuwa mwaminifu halafu tena unakuwa na tabia za kijinga za kuendelea kuwa na mahusiano ya nje na watu wako wa zamani.

SOMA; Hawa Ndio Maadui Wakubwa Wawili Wa Uchumba Au Ndoa Yako.

Kuna msemo wa waswahili unasema hawara hana talaka ukimtaka unampata hivyo ukiwa kwenye ndoa halafu unaendelea kuwasiliana na hawara basi moja kwa moja unakaribisha matatizo tu huwezi kubaki salama. Wengine wanaishi maisha ya maigizo kweli ya kutokuwa na amani ya mke au mume kutomruhusu mwenza wake kugusa simu yake. ‘’Kuna siku moja nilikuwa safarini  mkoa fulani hapa Tanzania.  Sasa  nikiwa huko niliingia saluni moja hivi nikawa nasubiria huduma, kuna ndugu mmoja alikuwa ananyoa ghafla akajisachi mfukoni akajikuta amesahau simu katika ofisi ya mke wake ikiwa inachajiwa na ofisi  ilikuwa siyo mbali na pale alipokuwa yeye ananyoa. Hivyo alimuamuru yule kinyozi aache kumnyoa akachukue simu yake kwani mke wake akiiona na ataipasua ile simu kwa sababu malaya wake asije akapiga halafu mke wake akapokea ile simu’’.

Rafiki, kweli nilimuona yule ndugu anaishi maisha ya utumwa sana tena ni gereza alilojitengenezea yeye mwenyewe. Kwanini uishi maisha ya wasiwasi kama vile mtu anayeoga nje? Kwanini usiwe mwaminifu ufurahie maisha na mwenza wako mmoja au kwa wale ambao wana wenza zaidi ya mmoja kadiri ya imani yao ya kidini?

Kama uko katika ndoa basi kubali kuishi katika uaminifu na uadilifu. Maisha ya ndoa yanahitaji sana uaminifu tena kwa karne hii ambayo watu wamekosa kabisa nidhamu binafsi. Huwezi kufanikiwa kama unatawanya nguvu zako kila kona,utachoka haraka sana na hutopata matokeo mazuri. Kutumikia mabwana wawili ni kazi na hutoweza kuwatosheleza wote.

SOMA; Haya Ndiyo Maisha Bora Wanayostahili Kuishi Wanandoa Katika Karne Ya Ishirini Na Moja (21)

Hatua ya kuchukua leo, kama umeingia katika mahusiano ya ndoa basi vunja mahusiano yote ya kimapenzi uliyokuwa nayo kabla hujaingia katika ndoa. Uliyefunga naye ndoa ndiyo muhimu na unampenda na ukaalika watu mbalimbali waje kushuhudia katika siku yenu ya kufunga ndoa je iweje leo unamgeuka na mliapa mbele ya Mungu na kadamnasi?

Kwahiyo, matatizo mengi ya wanandoa wasabishi wakubwa ni wao wenyewe. Wao ndiyo wanajua kiini cha matatizo ya mahusiano yao. Mnapoingia katika mgogoro wa kitu fulani mnatakiwa kuutatua siyo kukimbilia nje na kutafuta mtu wa kukufariji nje. Watu wanaoumia pale wanandoa wanapoingia katika mgogoro ni watoto ambao hawastahili kabisa kuyapata yote hayo.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea tovuti yangu kwa kujifunza zaidi kila siku na kupata huduma mbalimbali kama vile vitabu  kwa kutembelea tovuti  hii hapa  www.mtaalamu.net/kessydeo .

Asante sana na karibu sana !