Pamoja na changamoto nyingi zinazotuzuia kufikia mafanikio, kipimo nacho kimekuwa ni changamoto kubwa.

Kipimo unachotumia kwenye kupima mafanikio yako, kinaweza kukusukuma zaidi au kinaweza kukukatisha tamaa.

Aina za vipimo vya mafanikio.

Kuna aina mbili za vipimo vya mafanikio, moja inakusukuma kwenda mbele na nyingine inakukatisha tamaa.

Aina ya kwanza ni kipimo cha umbali uliobaki wewe kufikia mafanikio yako. yaani hapa unapima kile ambacho bado hujafanya. Kipimo hiki ndio ambacho wengi wanapenda kutumia na kimekuwa kinawarudisha wengi nyuma. Kama umepanga kufikia mafanikio makubwa, una mengi mbele yako ya kufanya, kadiri unavyofikiri yale ambayo hujafanya, ndivyo unavyoona bado ni magumu na makubwa.

Aina ya pili ni kipimo cha umbali uliokwenda mpaka sasa. Yaani hapa unapima kile ambacho tayari umeshafanya mpaka sasa. Kipimo hiki kinatumika na wachache na kimekuwa kinawasukuma kwenda mbele zaidi. Kama umepanga kufikia mafanikio makubwa, kwa kuangalia yale ambayo umeshafanya tayari, unapata moyo kwamba hata yaliyopo mbele yako utayaweza.

Hali ni moja, lakini unavyoipima inaleta tofauti kubwa sana kwako na kwenye kufikia kile unachotaka.

Pima kile ambacho umeshafanya tayari na utasukumwa kwenda mbele zaidi. Pima kile ambacho bado hujafanya na itakuwa rahisi kwako kukata tamaa.

SOMA; Kipimo Hiki Kitaonesha Kama Unaishi Au Unasukuma Siku.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba kipimo ninachotumia kupima mafanikio yangu nacho kinaweza kuwa kikwazo kwangu. Naweza kupima mafanikio yangu kwa kuangalia kile ambacho bado sijatekeleza, na hii itakuwa rahisi kunikatisha tamaa. Au naweza kupima mafanikio yangu kwa kuangalia kile ambacho nimeshatekeleza tayari, hii itanisukuma kwenda mbele zaidi.

NENO LA LEO.

Always concentrate on how far you have come, rather than how far you have left to go. The difference in how easy it seems will amaze you. – Heidi Johnson

Mara zote angalia ni urefu gani umekwenda mpaka sasa badala ya kuangalia ni urefu gani uliobaki wa kwenda. Tofauti ya jinsi gani inavyoonekana rahisi, itakushangaza sana.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.