Kuishi ni hatari, ndio kila siku tunakutana na hatari mbalimbali, lakini hatuachi kuishi.
Katika maisha tunakutana na hatari mbali mbali, kuna ambazo tunaweza kuziepuka na kuna ambazo hatuwezi kuziepuka.
Kuna hatari moja ambayo wengi wetu huwa tunafikiri tunaweza kuiepuka au kuikwepa na hivyo kukazana kuikwepa, na mwishowe tunajikuta tunahangaika na kitu ambacho hakiwezekani.
Hatari hii ni kufanya makosa, hata ungekazana kiasi gani, bado utafanya makosa.
Na katika hatari hii ya kufanya makosa tunapata makundi mawili ya watu.
Kundi la kwanza ni wale wanaofanya maamuzi yao kuepuka kufanya makosa. Hawa hukazana kuhakikisha hawafanyi makosa, hawapotezi. Na kwa njia hii hujikuta wakikosa fursa nzuri za kunufaika zaidi.
Kundi la pili ni wale wanaojua makosa yapo ila wanakazana kuyapunguza. Hawa wanajua huwezi kukwepa kabisa makosa, badala yake unaweza kuyapunguza, kwa kuwa na maarifa sahihi na kuchukua hatua wakati sahihi. Hawa hunufaika sana kwa sababu huzichangamkia fursa wakati wengine bado wanaogopa kuchukua hatua.
Watu hawa wa kundi la pili sio kwamba hawaogopi au wanajitoa kichwa kichwa, ila wanakuwa na maandalizi ya kutosha na hivyo kupunguza sana hatari ya kufanya makosa.
Je wewe upo kwenye kundi lipo kati ya haya mawili?
TAMKO LANGU;
Ninajua ya kwamba kufanya makosa ni kitu ambacho huwezi kukiepuka kabisa kwenye maisha yangu. Kitu pekee ninachoweza kufanya ni kuyapunguza, na nitaweza kufanya hivi kwa kuwa na maarifa sahihi na kuchukua hatua sahihi katika wakati sahihi. Sitakimbia tena kufanya makosa, bali nitapunguza makosa na kujifunza kwa yale makosa ninayofanya.
NENO LA LEO.
If you’re not making mistakes, then you’re not doing anything. I’m positive that a doer makes mistakes.
John Wooden
Kama hufanyi makosa, basi hufanyi kitu chochote. Wanaofanya mambo makubwa wanafanya makosa.
Usijaribu kuepuka makosa, hutafikia hatua yoyote kubwa kwenye maisha yako.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.