Dhumuni letu kubwa kwenye maisha ni furaha.

Tunafanya kile tunachofanya kwa sababu tunajua kitatuwezesha kuwa na furaha zaidi.

Hakuna mtu anayefanya kitu huku akijua ya kwamba kitamfanya asiwe na furaha.

Tumeshajifunza mengi sana kuhusu furaha, na jambo la msingi kabisa ambalo unatakiwa kujua ni kwamba FURAHA INAANZIA NDANI YAKO MWENYEWE. Furaha inaanza na wewe, kwa maisha unayochagua kuishi na vile unavyoendesha maisha yako.

Leo nakushirikisha kanuni rahisi sana ya furaha, ambayo kama utaweza kuikumbuka kila siku, utaweza kuishi maisha yenye furaha sana.

Karibu kwenye kanuni hii ya furaha….

FURAHA = UHALISIA – MATARAJIO.

Furaha ni ile tofauti ya uhalisia wa maisha yako na matarajio uliyokuwa nayo kwenye maisha yako.

Kama una matarajio makubwa sana lakini kwenye uhalisia ukapata chini ya matarajio hayo, hutakuwa na furaha. Kwa mfano umefanya kitu na ukawa unategemea kupata laki moja, halafu mwishowe ukapata elfu kumi, hutajisikia furaha.

Matarajio yanapokuwa makubwa, na kwa uhalisia ukapata zaidi ya matarajio hayo, unakuwa na furaha. Ulitegemea kupata laki moja na ukapata laki mbili, utakuwa na furaha.

Ufanye nini sasa ili kuhakikisha unakuwa na maisha ya furaha?

1. Kumbuka kanuni hii FURAHA = UHALISIA – MATARAJIO.

2. Endelea kuwa na matarajio makubwa kwako wewe mwenyewe, ila kwa wengine usiweke matarajio makubwa.

3. Chochote unachopata kwenye uhalisia, hata kama ni chini ya matarajio, jua ya kwamba ni hatua ya kupata kilicho bora zaidi. Usione kama ndio mwisho wa safari yako, bali jua ni hatua muhimu ya kwenda mbele zaidi.

Maisha ni yako na una haki ya kuwa na furaha, usikubali matarajio yako yakuzuie kufurahia maisha yako.

SOMA; Ishi Maisha Haya Kila Siku Na Utakuwa Na Furaha Na Mafanikio.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba furaha ni tofauti ya uhalisia wa maisha na matarajio yangu. Kadiri tofauti inavyokuwa hasi, yaani matarajio kuwa makubwa kuliko uhalisia, ndivyo ninavyokosa furaha. Nimeamua kuendelea kuwa na matarajio makubwa, lakini uhalisia wowote nitakaoupata nitaukubali na kuona ni moja ya hatua muhimu za kwenda mbele zaidi.

NENO LA LEO.

High expectations are the key to everything.

Sam Walton

Matarajio makubwa ndio ufunguo wa kila kitu kwenye maisha yako.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.