Mwaka 2015 unakwisha na tunakwenda kuanza mwaka 2016. Je unaweza kusema kwa maneno machache mwaka 2015 ulikwendaje kwenye biashara yako? je unaweza kuangalia kwa mwaka wote 2015 na ukaona ukuaji uliotokea kwenye biashara yako? kwa sababu kama hakuna tofauti, basi ni vigumu sana kwa biashara yako kukua zaidi.

Kila mwanzo wa mwaka, watu wengi huweka malengo ya mwaka husika, na japo sio malengo halisi, watu wengi huwa na matarajio makubwa kwa mwaka huo. Lakini kadiri siku zinavyokwenda watu husahau malengo hayo na kurudi kwenye maisha yao waliyoyazoea. Ili biashara yako ikue na uweze kufikia mafanikio makubwa, unahitaji kuweka malengo ya ukuaji wa biashara yako, na kufanyia kazi malengo hayo.

Kabla ya kuanza mwaka 2016 kibiashara, ni vyema ukachukua muda na kuupitia mwaka 2015 umekwendaje kwenye biashara yako. ni mambo gani ambayo uliyafanya mwaka 2015 ambayo yamepeleka biashara yako kukua zaidi. Pia fikiria ni mambo gani uliyofanya ambayo yalichangia kuirudisha biashara yako nyuma, au kukuchelewesha kwenda mbele zaidi. Kwa kujua vizuri 2015 imekwendaje kwako, kutakuwezesha kupanga vizuri mwaka 2016. Hapa utajua ni wapi pa kufanyia kazi zaidi na mambo gani ya kuepuka ili usiendelee kujirudisha nyuma.

Leo kupitia makala hii ya KONA YA MJASIRIAMALI, tutajadili malengo matano muhimu kwa kila mfanyabiashara kuweka kwa mwaka huu tunaoanza 2016. Inawezekana tayari una malengo yako tofauti, pia inawezekana malengo haya yakaingiliana na uliyokuwa nayo, yapitie malengo haya na angalia ni jinsi gani unaweza kuyafanyia kazi.

1. Boresha huduma kwa wateja.

Biashara ni wateja, na dhumuni la biashara yoyote ile ni kumhudumia vyema mteja ili aweze kuja tena na pia awalete wengine wengi. Hata kama sasa unatoa huduma nzuri kwa wateja wako, hakikisha hili pia linakuwa lengo lako kwa mwaka 2016.

Huduma kwa wateja ni eneo muhimu sana kwa biashara yako. kwa dunia ya sasa ambapo mteja ambaye hajaridhishwa na huduma anaweza kusambaza ujumbe kwa wengi, kupitia mitandao ya kijamii, unahitaji kutoa huduma bora sana kwa wateja wako.

Hakikisha unampatia mteja kile ambacho umeahidi kumpatia, na pale linapotokea tatizo kwa mteja kupitia biashara yako, basi hakikisha unawajibika. Msaidie mteja wako kuweza kupata mahitaji yake, au kutatua matatizo yake kupitia biashara yako.

2. Kuza biashara yako.

Haijalishi biashara yako ni kubwa kiasi gani kwa sasa, bado kuna nafasi ya biashara hii kukua zaidi. Wafanyabiashara wengi hufikia hatua fulani na kuridhika na ukuaji wa biashara, na kuacha kuweka juhudi zaidi, na hapa ndipo biashara zinapoanza kuporomoka. Malengo ya ukuaji wa biashara ni muhimu kwako kuweka kila mwaka na kuyafanyia kazi.

Weka malengo ya ukuaji wa biashara yako kwa kupanga kuwafikia watu wengi zaidi ya unaowafikia sasa, kutoa huduma nyingi na bora zaidi ya unazotoa sasa na hata kuongeza ukubwa wa biashara yako, ikiwa ni pamoja na kufungua biashara yako kwenye maeneo mengine.

3. Kuza mtandao wako wa kibiashara.

Mtandao ni muhimu sana kwenye mafanikio yako ya kibiashara. Dunia ya sasa, sio unajua nini sana kunajali, bali unamjua nani na nani anakujua. Na hii sio kwa dhana ya kupata upendeleo, ila kadiri unavyojuana na watu wengi, ambao nao wanafanya biashara au wanahusika na biashara, ndivyo unavyoweza kufungua fursa nyingi zaidi za kibiashara.

Mwaka huu 2016 weka malengo ya kukuza mtandao wako wa kibiashara, kujuana na watu ambao hukuwahi kujuana nao hapo mwanzo. Jua kuhusu biashara za wengine na angalia ni jinsi gani unaweza kuzitumia kama fursa ya ukuaji wa biashara yako.

4. Gatua majukumu yako.

Kama bado biashara yako inakutegemea wewe kwa kila kitu, basi huu ni wakati wa kuanza kubadili hilo. Unahitaji kuanza kugatua majukumu yako ya kibiashara. Kama kuna kitu chochote unachofanya ambacho mtu mwingine anaweza kukifanya vizuri basi tafuta mtu wa kukifanya. Hii itakupa wewe nafasi ya kufanyia kazi yale mambo muhimu kwenye biashara ambayo yatapelekea biashara yako kukua.

Wafanyabiashara wengi huogopa kugatua majukumu yao kwa wengine kwa kuamini kwamba hakuna anayeweza kufanya vizuri kama wao. Ila kama ni vitu vidogo vidogo vya kawaida, kung’ang’ania kuvifanya ni kupoteza muda ambao ungeweza kuutumia kukuza biashara yako zaidi.

5. Pata muda wa kuishi.

Wafanyabiashara wengi wamekuwa wanamezwa kabisa na biashara zao. Kila siku na siku nzima wanakuwa kwenye biashara zao, japo kwa kufanya hivi kunaweza kuikuza biashara, kunaweza kuharibu maeneo mengine muhimu ya maisha. Mwaka 2016 hata kama una mambo mengi kiasi gani ya kufanya, hakikisha unapata muda wa kuishi. Unapata muda wa kuwa na familia yako, unapata muda wa kuwa na marafiki na watu wengine wa karibu kwako. Na muhimu zaidi unapata muda wako wewe mwenyewe wa kutafakari biashara yako na maisha yako kwa ujumla.

Na unaweza kupata muda wa kuishi kama utapanga kuwa na matumizi mazuri ya muda wako, kwa kuepuka mambo ambayo yanakupotezea wewe muda.

Hakikisha mwaka 2016 utakapoisha, unaweza kuangalia nyuma na kusema mwaka huu nilileta mabadiliko makubwa kwenye biashara yangu. Na hii inawezekana kama utaweka malengo na kuyafanyia kazi. Anza na malengo hayo matano muhimu kwa biashara yako na kama kuna mengine yaongeze. Unapofanya kitu kwa malengo ni rahisi kujipima na kujua wakati ambao unaondoka kwenye malengo yako. kila la kheri.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani.