Je ni nini ambacho unataka kwenye maisha yako?
Unataka zaidi au unataka bora?
Dunia na jamii zimekuwa zinatupeleka vibaya, zikituaminisha kwamba tunahitaji zaidi na zaidi na zaidi.
Ubaya wa zaidi ni kwamba hauna mwisho, kadiri unavyopata ndivyo unavyohitaji zaidi.
Lakini ili uwe na maisha unayoyafurahia na yenye mafanikio, huhitaji zaidi, bali unahitaji bora. Huhitaji kupata zaidi na zaidi, kwa sababu kadiri unavyoenda kwenye zaidi, ndivyo unavyokuwa mtumwa wa zaidi. Lakini unapoenda kwenye ubora, unakuwa huru na unaweza kufurahia kile bora ulicho nacho, na maisha yako yakawa bora zaidi.
Dunia imekuwa inatuaminisha kwamba kuonekana unafanya zaidi ndio alama ya mafanikio, lakini hiyo ni kwa nje tu, ambayo mara nyingi haina uhalisia wowote kwa ndani yako. muhimu ni wewe kufanya kwa ubora, iwe ni vichache unafanya au ni vingi, fanya kwa ubora wa hali ya juu sana. Na hapa ndipo mafanikio yataanzia kwako na hata kuonekana kwa wengine.
Unahitaji maisha mangapi ili uweze kuwa na furaha? Huhitaji maisha zaidi ya uliyonayo sasa, bali unahitaji maisha bora zaidi ya uliyonayo sasa, kwa kuchakua kutaka bora na sio zaidi.
Unahitaji uongezewe muda kiasi gani katika masaa haya 24 ya siku ili uweze kufikia malengo yako? huhitaji muda zaidi, bali unahitaji kutumia muda huu ambao unao sasa kwa ubora, na hiyo itakuwezesha kuchukua hatua na kuwa na maisha bora, na yenye mafanikio.
Huhitaji nguo zaidi ili kuwa nadhifu, unahitaji nguo bora.
Chochote unachofikiri unahitaji zaidi kwenye maisha yako, sio kweli kwamba unahitaji zaidi, bali unahitaji kilicho bora zaidi. Na ubora ndio umebeba mafanikio yako.
Ondoka kwenye mtego huo wa zaidi, karibu kwenye ubora.
MUHIMU;
Asante kwa wote ambao tumekuwa kwenye kurasa hizi 365 za mwaka 2015. Leo ni ukurasa wa mwisho lakini mengine mengi mazuri yanakuja. Kama ulikosa kurasa yoyote bonyeza hapa.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba mafanikio yangu hayatatokana na kupata zaidi au kufanya zaidi, bali kupata kilicho bora na kufanya kilicho bora. Zaidi ni mtego ambao umewanasa wengi wanaoshindwa kufikia mafanikio ya kweli kwenye maisha yao. Ubora ndio njia ya uhakika ya kufikia mafanikio ya kweli. Kuanzia sasa nitafanya kila ninachofanya kwa ubora zaidi, na kila ninachohitaji nitachukua kilicho bora na sio zaidi.
NENO LA LEO.
“No matter who you are, no matter what you did, no matter where you’ve come from, you can always change, become a better version of yourself.”
― Madonna
Haijalishi wewe ni nani, haijalishi umefanya nini, haijalishi unatokea wapi, mara zote unaweza kubadilika, na kuwa toleo bora kabisa kwako binafsi.
Usitake kupata zaidi, taka kupata kilicho bora.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.