Kipindi cha nyuma, na hata sasa kwa kiasi fulani, watu wamekuwa wanaamini kwamba mafanikio na wema haviwezi kuwa pamoja.
Ni labda uchague kuwa mwema au uchague kuwa na mafanikio.
Na hivyo fikra za aina hii ziliwaweka watu wema njia panda na kuyaogopa kabisa mafanikio kwa sababu waliaminishwa kupata mafanikio kungeharibu wema wao.
Lakini hili sio la kweli hata kidogo. Na lilipata umaarufu kwa sababu watu wengi walikuwa hawana maarifa sahihi ni kwa jinsi gani unaweza kupata mafanikio kwa njia sahihi na ukaendelea kuwa mwema.
Na pia watu wengi hawakuwa na nidhamu ya kuweza kuendelea na yale mema hata baada ya kupata mafanikio. Na kwa kuwa mafanikio yalionekana kwa wachache ambao hawakuwa wema, basi jamii ilikubali kwamba wema na mafanikio havikai chungu kimoja. Na kwa kuwa watu hawakuwa na uvumilivu, basi ilikuwa vigumu kupata mafanikio kwa njia sahihi.
Kwa sasa kauli hii haipaswi hata kukatiza kwenye akili yako, hasa kama umekuwa unasoma makala hizi kwa muda sasa. Kwa sababu kwa sasa wewe umeshaiva kuhusu mafanikio, tayari unajua ni njia zipi sahihi za kuyapata, kuna changamoto utakutana nazo, na pia uvumilivu ni muhimu sana.
Kwa mfano upo kwenye kijiji ambacho watu wana shida kubwa sana ya maji, wanatembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji. Wewe ukatafuta njia ya kutatua hilo, na hatimaye ukaweza kuchimba kisima ambacho kinatoa maji safi na salama, na ukawauzia watu, kwa gharama ambayo wanaimudu. Kutokana na hitaji kubwa la maji ukachimba visima vingi zaidi, maeneo ya jirani. Hili likakuletea mafanikio makubwa ya kifedha. Je kuna ubaya gani hapo?
Kama kuna chembechembe yoyote ya fikra hii bado inakuzuia kuchukua hatua ivunje mara moja. Na kama imani yako ya dini uliyonayo imekuwa inakuaminisha usitafute mafanikio basi ni wakati pia wa kuitafakari vyema kama inakufaa wewe kweli.
Mafanikio ni jukumu la kila mtu, na mafanikio hayana uhusiano wowote na ubaya. Kuna watu wenye mafanikio makubwa ambao ni wema na kuna wenye mafanikio makubwa ambao ni wabaya. Vile vile kuna watu ambao hawana mafanikio na ni wema na kuna ambao hawana mafanikio na ni wabaya. Hivyo wema na ubaya ni tabia za watu, mafanikio ni kitu kingine tofauti kabisa.
Yasake mafanikio, ni kitu kizuri kwako na kwa wanaokuzunguka. Usilale, weka juhudi kubwa kwenye hilo.
SOMA; Njia Kumi na Mbili za Kutengeneza Thamani Kwenye Biashara.
TAMKO LANGU;
Leo nimejikumbusha ya kwamba hakuna uhusiano kati ya mafanikio na ubaya. Sio kweli kwamba nikifanikiwa nitakuwa mtu mbaya kwa wanaonizunguka. Bali nikifanikiwa nitakuwa msaada mkubwa kwao. Naondoa kabisa mawazo haya ya kuhusisha mafanikio na ubaya kwenye akili yangu. Nitayasaka mafanikio kwa juhudi zangu zote, sitazembea kwenye hili.
NENO LA LEO.
“Try not to become a person of success, but rather try to become a person of value.” Albert Einstein
Usikazane kuwa mtu wa mafanikio pekee, bali kazana kuwa mtu wa thamani.
Sio kweli tena ya kwamba huwezi kuwa na mafanikio na ukawa mwema. Unaweza kuwa na mafanikio makubwa na bado ukawa mtu mwema sana. Jenga mafanikio yako kwenye msingi wa kuongeza thamani.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.