Sikuombei mabaya lakini kama unashindwa kujibadilisha wewe mwenyewe, basi kuna kitu kimoja kitakachoweza kukubadilisha. Na kitu hiko ni matatizo mapya.

Unahitaji matatizo mapya ambayo yatakufanya ufikiri tofauti na unavyofikiri sasa.

Unahitaji matatizo mapya yatakayokusukuma ufanye kuliko unavyofanya sasa.

Unahitaji matatizo mapya yatakayokupa uthubutu wa kuchukua hatua licha ya kujawa na hofu kubwa.

Kadiri tatizo linavyokuwa kubwa, ndivyo inavyokusukuma wewe kuchukua hatua ya kubadili maisha yako.

Unaweza kuwa kwenye biashara ambayo huipendi au haikupi faida, lakini unaendelea kuifanya kwa sababu ndio ulichozoea kufanya. Ikitokea leo biashara hiyo ikafa kabisa, bila ya matarajio yako, utalazimika kufikiri tofauti na ulivyokuwa unafikiri mwanzo.

Unaweza kuwa upo kwenye ajira ambayo huipendi, au inakusumbua, au haikutimizii mahitaji yako. lakini ni kama umesharidhika kwani hujitumi zaidi ya hapo. Ukiambiwa leo kwamba ajira hiyo imeisha rasmi, utalazimika kufikiri zaidi na utaanza kuchukua hatua zaidi.

Kuwa na matatizo yale yale tuliyozoea kila siku, hakukusukumi sana kwa sababu huenda umeshajifunza jinsi ya kuishi na matatizo hayo. Lakini linapokuja tatizo jipya, utalazimika kukaa chini na kuwaza upya, kuchukua hatua kubwa ili kuhakikisha maisha yako yanaendelea kuwa bora.

Upande mbaya wa matatizo mapya yanaweza kukupoteza kabisa kama hujajijua vizuri na kama ni mtu wa kukata tamaa mapema. Hivyo ni vyema kujijua vizuri, na kuwa mvumilivu, ukijua ya kwamba hata kitokee kitu gani, kama bado hujafa, maisha yako yanaweza kuwa bora zaidi.

Wanaofanikiwa sana hawasubiri matatizo mapya yawafikie, bali wao wanayatafuta matatizo mapya. Kwa kufanya mambo mapya na makubwa mara kwa mara, wanatengeneza matatizo mapya, ambayo yanawasukuma kufanya zaidi.

Anza na wewe kutafuta matatizo mapya, hayo uliyonayo sasa umeshayazoea sana, na umeshajua kuishi nayo. Unahitaji matatizo yatakayokusukuma zaidi ya hapo ulipo sasa.

SOMA; Kama Unataka Kumaliza Matatizo Yako Ya Fedha Fanya Kitu Hiki Kimoja.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba kuwa na matatizo yale yale kila siku hakunisukumi sana kuchukua hatua, kwa sababu nakuwa nimeshajua jinsi ya kuishi na matatizo hayo. Kuanzia sasa nitaanza kutafuta matatizo mapya, ambayo yatanisukuma zaidi ya hapa nilipo sasa. Kwa matatizo hayo mapya nitafikiri zaidi na kuchukua hatua kubwa zaidi ya ninazochukua sasa.

NENO LA LEO.

A problem is a chance for you to do your best.

Duke Ellington

Tatizo ni nafasi nzuri kwako kufanya kwa ubora wa hali ya juu sana.

Tafuta matatizo mapya yatakayokusukuma kufikiri zaidi na kuchukua hatua zaidi ya unavyochukua sasa. Usiogope matatizo, yakaribishe na yatatue, hapo ndio penye ukuaji wako.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.