Mara zote sema ukweli, ni rahisi sana kwa sababu hutakuwa na haja ya kukumbuka mengi. Unapodanganya inabidi utunze kumbukumbu sana, ili wakati mwingine usiseme kinachopingana na ulichosema mwanzo. Halafu pia unapodanganya, unahitaji kuendelea kudanganya zaidi, ili kufunika uongo wa kwanza, na inafika hatua huwezi kuendelea kudanganya tena na ukweli wote unajitokeza hadharani.
Kuepuka yote haya ni vyema kusema ukweli, mara zote, kwa sababu hii itakusaidia sana. Ni changamoto kubwa sana kufanya hivi kwa sababu huenda kuna mambo mengine unaona ukisema ukweli utapoteza. Lakini ukweli ni kwamba hata ukipoteza, ni kidogo kwa sasa na baadaye mambo yatakuwa mazuri.
Sasa kuna changamoto nyingine ya kusema ukweli, na changamoto hiyo ni ujasiri wa kusema ukweli, uthubutu wa kusema ukweli. Unaweza kuwa upo tayari kabisa kusema ukweli, ila ukakosa ujasiri wa kufanya hivyo, ukakosa uthubutu.
Na changamoto hii inakuwa kubwa zaidi pale ambapo wewe pekee ndiye unayesimamia ukweli, na wanaokuzunguka wote wanakwepa ukweli. Ni rahisi kuzuiwa na nguvu hii ya wengine na kujikuta unaukimbia ukweli, lakini kumbuka uongo ni uongo, na kuna siku mambo yatakuwa wazi. Na hutakuwa na utetezi kwamba hukuthubutu kusimamia ukweli.
Pale unapokuwa na wasiwasi, pale unapokosa ujasiri wa kusimamia ukweli, hapo ndipo unahitaji kujikumbusha kwamba ukweli hauuliwi, bali unaweza kufichwa kwa muda. Na kadiri unapouficha ukweli ndipo unazidi kutengeneza matatizo mengine makubwa baadaye.
SOMA; Unachokiona Na Unachokisikia Sio Ukweli, Ukweli Ni Huu Hapa….
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kukosa kwangu ujasiri wa kusema na kusimamia ukweli hakunipi mimi uhalali wa kuukwepa ukweli. Ukweli utabaki kuwa ukweli hata iweje, na siku ikifika ukweli utajiweka hadharani. Nitaendelea kusimamia ukweli daima, hata kama ni mimi mwenyewe naamini hivyo katika kundi kubwa la watu.
NENO LA LEO.
In a time of universal deceit – telling the truth is a revolutionary act.
George Orwell
Katika nyakati hizi za ulimwengu wa udanganyifu, kusema ukweli ni tendo la kimapinduzi.
Sema ukweli mara zote, kuwa na ujasiri wa kusimamia ukweli hata kama kila mtu anaupinga, maana ukweli huwa haupotezwi.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.