Kila mtu anaweza kumshushia mwingine chini, ila ni mashujaa peke yake ambao wanaweza kuwainua wengine.

Kila mtu anaweza kumkatisha tamaa mwingine, kumwambia anachofanya hakitafanikiwa au atashindwa, ni wachache sana wanaoweza kutoa moyo kwa wengine.

Kila mtu anaweza kumsema mwingine vibaya, kumsengenya kwa wengine na kusambaza maneno ya uzushi. Ni wachache sana wanaoweza kuwasemea wengine vizuri na kusambaza habari zao nzuri.

Kila mtu anaweza kupata wivu pale mwenzake anapopiga hatua, na kufanikiwa zaidi, anajisikia vibaya na hata kuanza kukaa mbali naye. Ni wachache wanaoweza kufurahia mafanikio ya wenzao, na kuwaomba ushauri zaidi wanawezaje na wao kufanikiwa.

Kama umegundua kwa makini kile ambacho kinaweza kufanywa na kila mtu huwa hakiwafikishi kwenye mafanikio, kinawafanya waendelee kuwa washindwa. Lakini kile ambacho kinafanywa na wachache, ndiyo kinachopelekea mafanikio kwao na kwa wengine pia.

Maana unapokazana kumshusha mwingine chini, ni lazima na wewe ukae hapo chini ili kumzuia asipande juu. Lakini unapomwinua mwingine, ni lazima na wewe upande juu ndio uweze kumwinua zaidi.

Usifanye kile ambacho kila mtu anaweza kufanya, fanya kile ambacho ni bora sana kwao na kwa yule unayekwenda kumfanyia.

SOMA; FEDHA; Usiifanyie Kazi Fedha, Wacha Fedha Ikufanyie Kazi Wewe.

TAMKO LANGU;

Nimejua kile ambacho kila mtu anaweza kufanya, mara nyingi sio kitu bora kwa wote wanaohusika. Kuanzia sasa kwenye mahusiano yangu na wengine, nitahakikisha nafanya kile juhudi za kuwainua wengine juu zaidi kwa sababu kwa kufanya hivyo na mimi nitakwenda juu zaidi. Lakini nikifanya kile ambacho wengi wanaweza kufanya, kumshusha mtu chini, itanibidi na mimi nikae chini ili kuhakikisha mtu huyo anabaki chini.

NENO LA LEO.

“There is no exercise better for the heart than reaching down and lifting people up.”
― John Holmes

Hakuna zoezi bora kwa moyo wako kama kwenda chini na kuwainua wengine juu.

Unapowainua wengine juu na wewe pia unakwenda juu. Ila unapowashusha chini na wewe inabidi ukae chini ili kuhakikisha hawapandi.

Inua wengine juu.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.