Ili moto uwake, unahitaji kuwa na vitu vitatu muhimu.
Cha kwanza ni nishati ambayo inachochea kuwaka kwa moto.
Cha pili ni joto, lazima joto lifikie kiwango fulani ndio nishati iweze kuwaka moto.
Na kitu cha tatu ni uwepo wa hewa ya oksijeni, hewa hii kuchochea moto kuwaka zaidi.
Hivyo ukitaka moto uendelee kuwaka weka vitu hivyo vitatu.
Na kama hutaki moto uendelee kuwaka, kama unataka kuzima moto, basi ondoa vitu hivyo vitatu, sio lazima vyote kwa pamoja. Kwa mfano ukiondoa nishati hakuna kitakachowaka tena, ukiondoa upatikanaji wa hewa ya oksijeni moto utazima.
Najua unajua lengo letu hapa sio kujadili moto, bali ni kujifunza maarifa yatakayofanya maisha yetu kuwa bora zaidi.
Moja ya changamoto tunazokutana nazo kwenye maisha ni kukutana na moto mbalimbali. Huwa tunakutana na moto kila mara kwenye maisha yetu, wakati mwingine moto tumeanzisha wenyewe au tumejikuta tayari tunahusika na moto.
Moto unaweza kuwa kutoelewana ndani ya nyumba, kazini au hata kwenye biashara. Moto unaweza kuwa hasira uliyonayo juu ya wengine, au hasira ambayo wengine wanayo juu yako. Moto unaweza kuwa matatizo mengine unayokutana nayo, ambayo kadiri siku zinavyokwenda yanazidi kupamba moto.
Unapokuwa kwenye hali ya ugomvi, kuna mambo ambayo ukiyafanya unazidi kuchochea ugomvi. Unapokuwa na hasira na mtu au mtu ana hasira na wewe, kuna mambo ambayo ukiyafanya yanachochea hasira zaidi.
Leo tutaangalia jambo moja ambalo wewe unachangia kwa kiasi kikubwa sana. Kwenye moto huo, kitu hiko ni sawa na hewa ya oksijeni. Kitu hiko ni zile hisia zako unazoweka kwenye hali hiyo. Pale unapoona kwamba umefanyiwa sivyo, pale unapoona umedhalilishwa, pale unapoona umedharauliwa. Kwa njia hii utataka kuzuia majeraha kwenye hisia zako, na hivyo kutaka kumwonesha yule mwingine kwamba hawezi kukufanyia hivyo. Utajibu mashambulizi sio kwa sababu kuna kikubwa utakachopata, ila kwa sababu tu unataka umuoneshe.
Sasa unajua ni nini kitatokea? Na yeye atataka akuoneshe, halafu wote mnachochea moto, na hali inazidi kuwa ngumu.
Badala yake wewe unaweza kuondoa hewa hii ya oksijeni, kwa kuelewa kwamba huna haja ya kupambana, kwa kuelewa kwamba huenda mwenzako amekufanyia hivyo kwa sababu ana matatizo yake binafsi. na hapo ukakaa kimya, ukaacha kuchukua hatua nyingine ya kuchochea moto, na moto ukazima wenyewe.
Kuanzia sasa utakapojikuta kwenye moto wowote, iwe ni ugomvi au kutokuelewana, hakikisha huendelei kuchochea moto huo.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba mara nyingi nimekuwa nachochea moto kwenye changamoto ninazopitia kwenye mahusiano yangu na watu wengine. Na nimekuwa nafanya hivi kuridhisha hisia zangu. Kuanzia sasa nitaacha kuchochea moto kwa kutokutaka kushindana, nitapuuza na kukaa kimya na kuendelea na yale ambayo ni muhimu zaidi kwenye maisha yangu.
NENO LA LEO.
“We’re all islands shouting lies to each other across seas of misunderstanding.”
― Rudyard Kipling
Sisi wote ni visiwa ambapo tunarushiana maneno ya uongo kupitia bahari ya kutokuelewana.
Unapokuwa kwenye hali ya kutokuelewana, kukaa kimya ni bora kuliko kuendelea kutoa maneno. Maneno hayatasaidia zaidi ya kuchochea.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.