Habari ndugu msomaji wa makala za uchambuzi. Ni wiki nyingine ambapo tunaendelea na utaratibu wetu wa kujifunza kwenye kitabu cha Wiki. Wiki hii tunaangazia kitabu kiitwacho The Four Purposes of Life (Makusudi manne ya Maisha) kilichoandikwa na mwandishi DAN MILLMAN. Kitabu kinazungumzia makusudi manne ya maisha, ambapo kusudi la kwanza likiwa ni kujifunza masomo ya maisha, kusudi la pili ni kutambua kazi na wito wako, kusudi la tatu ni kugundua wito wako uliofichika (kila mtu ana wito wake uliofichika) na kusudi la nne ni kukabiliana na wakati wa sasa (kuutumia vizuri muda wa sasa). Hapa chini nimekushirikisha mambo 20 niliyojifunza kutoka kwenye kitabu hichi.

 
Karibu tujifunze.
1. Kama hutajifunza masomo rahisi hua yanakuaga magumu kadri muda unavyokwenda. Kukataa kujifunza au kukataa mabadiliko hupelekea madhara makubwa baada ya muda, na sio kwa ajili ya kutuadhibu hapana ni ili kupata usikivu (attention) wetu. Lessons repeat themselves until we learn them.
2. Tunajifunza na kukua kupitia changamoto tunazokabiliana nazo, kila shida inayo zawadi zilizofichika ndani yake. Wengi tumewahi kupitia kwenye maumivu ya kimwili, kiakili na hata ya kihisia, lakini kila changamoto imeleta kipimo kikubwa cha kupima uwezo, hekima na mtazamo tulionao. Pamoja na kwamba hatuwezi kukaribisha changamoto au kukabiliana na mabadiliko yasiyotarajiwa, kupoteza vitu/ndugu au kukata tama, lakini baada ya kupitia hayo yote unapotizama nyuma baada ya muda unakuja kuthamini zawadi za shida ulizopitia. Wapo watu wanagundua uwezo wao kutokana na shida walizopitia, wapo wanaoanzisha biashara kubwa baada ya kufukuzwa kwenye ajira zao. Huwezi kukua kama njia yako imenyooka tu, kama hakuna kikwazo huwezi kukua, na pengine hutaweza kutambua ni uwezo mkubwa kiasi gani uko nao.
3. Maisha yanatupatia fursa na machaguo (choices) kadhaa, lakini tunapokea, tunafanikisha au kufurahia hizo fursa kwa kiwango kile tu tunachoamini kwamba tunastahili hizo fursa. Mfano Biblia inaposema “Ombeni nanyi mtapewa” swali linakuja Ni kitu gani hicho ambacho upo tayari kukiomba na kujitahidi kukipata? Watu huomba kile wanachoamini wanastahili, ndio maana katika kuomba wapo wanaoomba pikipiki, wapo wanaoomba gari na wapo wachache wanaoomba ndege. Kama unaamini kwamba aombaye hawezi kuchagua (anapokea tu apewacho) basi utapata fursa chache sana, tena zile fursa za kinyonge kuendana na jinsi unavyojiona unastahili. Low self-worth is a primary cause of self-sabotage.
4. Changamoto moja kubwa zaidi katika eneo la kujiboresha (self-improvement) ni kubadilisha maarifa kwenda kwenye utekelezaji, kukifanyia kazi kile tunachokifahamu ni changamoto ya wengi. Wakati baadhi yetu tunatenda pasipo kufikiri, wengi wetu zaidi tunafikiri pasipo kutenda. Unaweza kuta watu wana mawazo mazuri sana, wana mipango mizuri sana, hata unapowasikiliza unatamani kuwa kama wao, sasa njoo watizame katika utendaji unakuta ni majanga. Hata ukitizama mafanikio yao ni madogo sana ukilinganisha na wanavyofikiri. Ikabadili changamoto hii moja kubwa, ujionee utofauti ambao hujawahi kuushuhudia, kufikiri kwako kuendane na utendaji. Badili kile unachokijua kua kile unachotenda. Just thinking about doing something is the same as not doing it
SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Vijana Wanaokwenda Kuanza Maisha Ya Kujitegemea Kwa Mwaka Huu 2016.
5. Kusudi la Maisha ni Maisha yenye kusudi. Kila mtu analo kusudi lake, kwa wengi kusudi hilo hua limefichika, juhudi ya ziada inahitajika kuligundua na usipoweza kuligundua na kulitumikia kusudi lako hata upate kitu gani huwezi kupata utoshelevu wa maisha. Unaweza kukuta watu wamefanikiwa kifedha lakini bado hawana furaha, mahusiano yao na watu wengine ni mabovu. Ni kwa sababu maisha yao hayatengenezi maana yeyote zaidi ya kuingiza fedha tu. Hawajatambua kusudi lao, hata hicho wanachofanya ni kwa sababu tu kinawaingizia fedha la sivyo wasingefanya.
6. Kuna tofauti kati ya kazi na wito. Kazi ni ile huduma unayofanya kwa ajili ya kuingiza kipato, ni pale unapouza muda, jitihada zako, maarifa, ujuzi na uzoefu wako ili kupata mshahara, kipato au manufaa mengine. Unaweza kuiita ajira, biashara, taaluma, n,k. Unaweza kua na sababu nyingi za kukufanya uamke asubuhi na kwenda kufanya hiyo kazi lakini kupata kipato ndio sababu ya msingi inayokusukuma kwenda kuifanya. Labda kama wewe ni tajiri.
7. Wito ni kile unachopenda, unachovutiwa nacho kwa msukumo wa kutoka ndani. Sio tu kile unachotaka kufanya, bali ni kile unachohitaji kufanya, kile kitu kinachokamata hisia na mawazo yako kisawasawa bila kujali unaweza au huwezi kuelezea ni kwa nini. Kile kitu kinachokukereketa, upo tayari kukifanya hata kama hakikupatii kipato. A calling may (or may not) earn an income or become a career.
8. Wito unaweza kua kazi au kazi inaweza kua wito. Kama tulivyoona kwamba tofauti ya msingi ya wito na kazi ni kipato au maslahi, kwamba tunafanya kazi ili tuingize kipato ila tunafanya wito wetu ili tupate kuridhisha nafsi zetu (satisfaction). Ila kama unaipenda sana kazi yako kiasi kwamba unaweza kuifanya hata kwa bure bila kupata kipato chochote, basi hiyo kazi imekua wito. Na kama wito wako umeanza kukuingizia kipato kizuri basi ujue wito wako huo umekua kazi. Kuna watu wito na kazi vimeungana kua kitu kimoja ila kuna wengi ambao wito na kazi ni vitu tofauti.
9. Kwa kua Wito wa kweli unahusisha shughuli za kuwatumikia wengine, zile shughuli za burudani binafsi (personal leisure) kama kucheza gofu, kuvua samaki, kuwinda n.k zinaangukia katika kundi la mambo apendayo mtu (hobbies), Ila tunapotumia hobbies zetu kuwafundisha au kuwashirikisha wengine hiyo hobby inakua ni wito na kazi. Wale wanaoweza kugeuza wito wao kua kazi hufanikiwa na kupata utoshelevu wa maisha zaidi ya wale wanaotumikia kazi ambazo sio wito wao. Wito wako unaweza kuufanya vizuri zaidi ya mtu mwingine ambaye anafanya tu kama shughuli ya kumpatia kipato.
10. Watu wengi wanaomaliza vyuo, wanaondoka chuoni wakiwa wana elimu ndogo sana kujihusu wao wenyewe (self-knowledge). Mfano mtu anaweza kumaliza shahada ya uhasibu, pengine yuko vizuri sana kwenye hiyo fani aliyosomea lakini hajifahamu vizuri yeye binafsi. Ukiacha ule uhasibu hafahamu yeye binafsi ana uwezo gani. Na ndio maana unaweza kuta wengi wanaomaliza vyuo wasipopata ajira, huanza kulalamika kwa kutupa lawama kwa serikali na wadau wengine kwamba wamewasahau. Mtu kamaliza chuo miaka mitatu iliyopita, yupo nyumbani tu, ukimuuliza unafanya kazi gani, anaporomosha lawama kwa serikali kwa kuchelewa kutangaza kazi za fani yake.
11. Hakuna kazi nzuri kwa kila mtu. Kazi inaweza kua nzuri kwako tu tena kwa kipindi fulani cha muda katika maisha yako. Kwa maneno mengine ni kwamba hakuna kazi inayopendwa na kila mtu, hakuna kazi inayoridhisha kila mtu, mfano katika taaluma ya udaktari utakuta kuna wengine wanaridhika na kazi hiyo na kuna wengine hawaridhiki nayo. Hivyo kila kazi unayoijua, wapo ambao wanaitamani na wapo ambao hawaitaki.
SOMA; Kama Unafikiri Ukifanya Kitu Hiki Peke Yake Ndio Umefanikiwa, Unajidanganya Mwenyewe.
12. Maisha ni jaribio, ni maabara ya kujitafuta wewe mwenyewe. Hivyo mpaka umepata wito ambao unakuridhisha haswa endelea kujitafuta, waweza kujipatia kazi fulani kwa muda huku ukiwa macho kwa fursa nyingine mpya mpaka umepata kazi au wito ambao utakua tayari kujitoa kwa dhati (commitment) kwa muda fulani.
13. Hata ujitahidi na kujaribu kiasi gani kuna watu ambao hawatakukubali wala kukupenda, ila pia wapo watu watakaokukubali na kukupenda jinsi ulivyo. Kwanini upoteze muda wako katika kuwaridhisha wale wasiokukubali? Fuata kile unachopaswa kufanya, timiza kusudi lako la kuwepo hapa duniani.
14. Ili kujua kama kazi itakufaa kuna vigezo vitatu vya kuipima.
· Je kazi hii inaniridhisha?
· Je ninaweza kupata kipato kizuri?
· Je inatoa huduma yenye kufaa (useful service)?
Maswali hayo matatu yanaonyesha vipengelee 3 muhimu vya kazi yenye kuleta utoshelevu katika maisha. Mawili kati ya hayo yanaweza kuonekana yanatosha kwa muda fulani, lakini kazi inahitaji kukidhi vigezo vyote vitatu, ili kupata utoshevu wa muda mrefu.
15. Unaweza kukosa uzoefu ila huwezi kukosa kipaji. Kila mtu anacho kipaji chake, na ili kiweze kuleta thamani kwako na wengine ni lazima kipiti mchakato wa kutengenezwa na kulelewa. Watu hudhani ukiwa na kipaji basi mambo yatanyooka tu, sio kweli, unaweza kufa hata hujanufaika na kipaji chako. Ni kweli kila mmoja amezaliwa na kipaji, ila kukiibua, kukitengeneza na kukilea, Mhusika mwenyewe anapaswa kutia bidii sana.
16. Ushirikiano ni mzuri zaidi ya ushindani. Kushindana ni kule kutaka kuonekana bora kuliko wengine, huku wengine wakionekana wadhaifu. Mara nyingi hali hii huleta matabaka hasa sehemu za makazini. Mnaposhirikiana, ina maana hujiangalii wewe binafsi utapata nini, bali unaangalia kama timu mtapata nini, mnaposhirikiana ni rahisi kujifunza kwa wengine maana kila mmoja ataonyesha uwezo wake pale. Ila inapotokea kwenye timu, kila mmoja anataka kushindana na wengine, ina maana vile anavyovijua na kuviweza atavificha ili wengine wasinufaike. Kushindana kwa ajili ya maslahi binafsi hua kunazorotesha mafanikio ya kundi na hata ya mtu binafsi.
SOMA; Huyu Ndiye Mwalimu Wa Kwanza Na Muhimu Sana Kwenye Malezi Ya Mtoto.
17. Sifa kubwa ya Kiongozi ni kuwa mfano. Wale unaowaongoza unawahamasisha sana kwa kuonyesha mfano. Watu wanajifunza kwenye matendo yako kuliko maneno yako hivyo unahitajika kua mfano zaidi kwenye matendo. Usipokua mfano pengine wanaweza kudhani huwajali au huna uwezo kwenye jambo hilo. Mfano mzuri ni siku Raisi Tanzania (Dr. Magufuli) alipotangaza siku ya usafi, kisha yeye akawa mfano kwenda kwenye usafi, kitendo kile kiliamsha ari ya wananchi na viongozi wa chini. Pengine asingekwenda kwenye usafi viongozi na watendaji wa chini yake wangeamrisha tu watu wafanye usafi wao wabaki majumbani au maofisini. Kuwa mfano kwa wale unaowaongoza
18. Hakuna maamuzi ya baadaye, bali maamuzi yote hufanywa wakati wa sasa. Muda wa sasa ndio ulio kwenye uthibiti wako. Kama wataka kubadili maisha yako tumia nguvu ya sasa kwa kufanya maamuzi muda wa sasa. Utofauti wa waliofanikiwa na wale wasiofanikiwa ni kwamba wale waliofanikiwa hufanya yale ya muhimu muda wa sasa, na hao wengine yale ya muhimu huyaweka pembeni ili kuyafanya baadaye. You only need to make a decision in the moment you need to make it.
19. Hakuna maamuzi yanayokua halisi kama hakuna utendaji. Wengi wetu tunayatazama maamuzi kama mchakato wa akili na kuhitimisha. Mfano mnapokuwa kwenye kikao mkawa na hitimisho la mambo yatakayofanyika baadaye, ujue yale siyo maamuzi mpaka yametendewa kazi. Maamuzi ili yawe halisi lazima pawepo na mtu wa kuyatendea kazi. Maamuzi hayapaswi kuishia kwenye akili na makaratasi, yanapaswa kusimamiwa katika utekelezaji.
20. Kuna siri mbili kuu kwa wale waliojiajiri au wajasiriamali. Siri ya kwanza ni kuwa vizuri kwenye kile unachofanya, yaani zalisha kitu bora sana (huduma au bidhaa) kwa maana usipotoa kitu bora zaidi, hakitapata usikivu wa wateja, yaani wateja hawatajisumbua kuja kwako. Wateja hupendelea zaidi ubora. Siri ya pili ni kukitangaza kwa ubora kile unachofanya au waweza kuajiri mtu ambaye anaweza kukufanyia hiyo kazi kwa ubora zaidi. Hata kama una ujuzi mzuri sana katika kuzalisha vitu bora, kama ukishindwa kukiuza kwa wateja itakuwia ngumu kusonga mbele, kumbuka biashara yako inaweza kuwahudumia tu wale watu wanaojua kwamba biashara yako ipo. Hivyo lazima kuweka pia ubora katika kujitangaza ili kuwafikia watu wengi zaidi.
Asante sana
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com