Rafiki yangu mpendwa,
Kila mtu anapenda mabadiliko, lakini hakuna aliye tayari kubadilika.
Mafanikio yoyote ambayo mtu anahitaji kwenye maisha yake, yanaweza kuja kupitia mabadiliko.
Hii ina maana kwamba, ili mtu atoke pale alipo sasa na kwenda mbali zaidi, lazima abadilike.
Lakini mabadiliko yamekuwa magumu kwa wengi. Wapo wanaojaribu mabadiliko lakini yanawashinda. Wanatamani vitu vingekuwa kwa utofauti fulani lakini vinashindikana.
Kinachotokea ni wengi kuona mabadiliko ni magumu na hayawezekani. Hivyo wanakubaliana na hali ya kawaida na kuendelea na maisha ya kawaida, ambayo siyo waliyokuwa wakiyataka.
Kuna sababu kubwa moja inayofanya mabadiliko kuwa magumu sana kwa wengi. Sababu hiyo ni wengi kutaka kubadili nje kabla ya kubadili ndani.
Watu wengi wanapotaka kuleta mabadiliko, wamekuwa wanaanzia nje kabla ya kufanya mabadiliko ya ndani.
Wamekuwa wanajaribu kubadili tabia za nje, wanajaribu kubadili wengine na hata kubadili mazingira.
Wanachokifanya wengi wanaosema wanataka mabadiliko ni kutaka vitu viende kama wanavyotaka wao. Sasa haya siyo mabadiliko, na kwa hakika hayawezi kufanikiwa.
Mabadiliko ya kweli yanaanzia ndani, yanaanzia ndani ya fikra na mtazamo wa mtu.
Lazima mtu ubadili namna unavyofikiri, namna unavyochukulia vitu kabla vitu hivyo havijabadilika kwa nje.
Lazima ndani yako mwenyewe uchague kuwa bora zaidi ya ulivyokuwa, lazima uwe na msukumo ambao unakufanya utake kuchukua hatua za tofauti.
Kama hata msukumo wa mabadiliko unatoka nje yako, ni vigumu zaidi kubadilika.
Na hii ndiyo sababu kuwabadili wengine ni kazi ngumu sana, kwa sababu hakuna anayependa kubadilishwa au kulazimishwa abadilike.
Kama unataka kuibadili dunia, basi jua kuna mtu mmoja tu ambaye unapaswa umbadili na dunia nzima itafuata. Mtu huyo ni wewe mwenyewe.
Ukijibadili wewe, kwa mabadiliko yanayoanzia ndani yako, utaanza kuona vitu kwa mtazamo tofauti, utaanza kuvichukulia vitu kwa uzito tofauti na hapo utaiona dunia ikiwa tofauti.
SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Cha The Four Purposes of Life (Makusudi manne ya Maisha)
Hata wale wanaokimbia eneo moja kwenda jingine wakifikiri kwamba mambo kule yatakuwa bora zaidi, huwa wanaenda kugundua kwamba walichokikimbia eneo walilotoka ndiyo wameenda kukikuta walikoenda.
Mfano kama kuna kazi unafanya na haikulipi vizuri na huipendi, ukaondoka na kwenda kwenye kazi nyingine, mara nyingi utafika hatua na kugundua hata kazi mpya uliyoanza haikulipi kama ulivyofikiri na huipendi kama ulivyokuwa unaiangalia kwa nje.
Katika hali kama hizi, ndiyo unagundua kwamba shida siyo kazi, wala kile unachopata bali shida ni wewe mwenyewe. Ukichagua kuiangalia kazi yako kwa mtazamo mwingine, ukichagua kuweka thamani zaidi, utaanza kuipenda na utaweza kuongeza kipato chako. Na hata kama hutaongeza, basi ukiondoka kwenye kazi hiyo ukiwa tayari umeshabadilika wewe, utakuwa kwenye nafasi ya kupata kazi inayokufaa zaidi.
Kabla hujakazana na mabadiliko ya nje, hebu anza kwanza kubadilika ndani yako mwenyewe. Anza kubadili fikra zako, badili mitazamo yako na badili tabia zako. Mengine ya nje yatafuata kwa urahisi kama mabadiliko yataanzia ndani.
Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha