Wafanyabiashara na makampuni wameshajua udhaifu wetu sisi binadamu. Na udhaifu huu unatokana na kitu ambacho kila mmoja wetu anakitaka. Kuna kitu ambacho kila mmoja wetu anakitafuta. Kwa hatua zote tunazochukua, kwa juhudi zote tunazoweka kila siku, tunataka kupata kitu kimoja muhimu sana.

Kitu hiki ni furaha. Kila mtu anataka furaha kwenye maisha yake. Hata wale ambao wanafanya makosa, wanafanya hivyo wakiamini yatawaletea furaha. Hakuna mtu ambaye atapewa kati ya furaha na mateso na akachagua mateso, labda awe na matatizo yake binafsi.

Sasa baada ya watu kulijua hili, wamekuwa wakilitumia vibaya kwako wewe. Wafanyabiashara na makampuni wamekuwa wakitumia hitaji hilo la furaha kukushawishi wewe ununue zaidi bidhaa au huduma zao. Wanachokifanya ni kuitangaza bidhaa au huduma yao kama chanzo kikuu cha furaha. Ya kwamba ukitumia tu utakuwa na furaha kubwa. Na katika matangazo hayo hutumia picha au watu ambao wanaonekana kuwa na furaha sana.

Kwa kuona wale wana furaha, basi na sisi tunashawishika kwamba tukinunua bidhaa au huduma ile tutakuwa na furaha kubwa. Tunanunua bidhaa au huduma ile, na ndani ya muda mfupi tunajisikia raha, sio furaha. Lakini baada ya muda huo mfupi kuisha, mambo yanarudi pale pale, bado hatuna furaha.

Leo nataka tukumbushane jambo muhimu sana kuhusu furaha, tunakumbushana kwa sababu tulishajadili hili mara nyingi. Hakuna kitu chochote unachoweza kununua kikakupa furaha. Kwa kifupi, furaha hainunuliwi. Kama mtu anakuambia nunua hiki utapata furaha, kimbia haraka sana, maana anachotaka kufanya ni kukutapeli.

Kama hapo ulipo sasa, kwa maisha unayoishi na kazi au biashara unayofanya, huna furaha, basi hakuna kitu chochote ambacho unaweza kununua leo na kikakupa furaha. HAKUNA. Furaha ni kitu ambacho kinaanzia ndani yako. ni kitu ambacho kinatoka ndani ya nafsi yako, bila ya kujali unamiliki nini kwenye wakati huo.

Furaha ni zao la maisha unayoishi, mchango wako kwa wengine, na kuridhika na kazi au biashara unayofanya na sio zao la nini unamiliki. Ni kweli kumiliki vitu ambavyo ni muhimu kwako kunafanya maisha yawe bora na maisha yakiwa bora unakuwa na furaha. Lakini tunarudi kwenye jambo la msingi kwamba hakuna kitu ambacho ukienda kununua sasa hivi basi utapata furaha, unaweza kupata tu raha ya muda mfupi, lakini sio furaha.

Furaha ni kazi ya ndani kwako mwenyewe, usidanganyike kuinunua.

SOMA; Sheria 65 Za Mafanikio, Furaha Na Maisha Bora Kutoka Kwa ROMAN.

TAMKO LANGU;

Najua ya kwamba hakuna kitu ambacho nikinunua leo nitakuwa na furaha zaidi. Furaha ni zao la maisha yangu na inatoka ndani yangu, sio zao la kitu au vitu ninavyomiliki. Sitakubali kuingia kwenye mitego ya kibiashara ambayo inashawishi nikinunua kitu fulani basi nitakuwa na furaha sana. Nitatengeneza furaha ya kudumu kwenye maisha yangu kwa kuyaishi maisha yangu kwa viwango vyangu mwenyewe.

NENO LA LEO.

“Happiness is not in the mere possession of money; it lies in the joy of achievement, in the thrill of creative effort.” — Franklin D. Roosevelt

Furaha haitokani tu na kuwa na fedha; furaha inatokana na yale maisha unayoishi, inatokana na ubunifu na juhudi unazoweka.

Usidanganyike kwamba kuna kitu unaweza kununua sasa na kikakuletea furaha, hakuna. Furaha ya kweli inatoka ndani yako.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.