Wewe ni wewe, na utabaki kuwa wewe, iwe una fedha au huna, una kazi au huna, biashara yako inafanya vizuri au vibaya na iwe watu wanakuheshimu au wanakudharau.

Wewe utabaki kuwa wewe, iwe una marafiki wengi au machache, una kipaji au huna, na ni maarufu au sio maarufu.

Tatizo kubwa na ambalo linapelekea watu kujiona hawafai, na hata kukata tamaa huwa linaanza pale mtu anaposhikiza utu wake kwenye kitu. Pale mtu anapojiona yeye ni muhimu pale tu anapokuwa na fedha, au pale watu wanapomheshimu, au pale ambapo ni maarufu au anapokuwa na marafiki wengi.

Hiki ni kipimo ambacho dunia imekuwa inatuaminisha ni sahihi kwa utu, lakini kama ilivyo kwenye mambo mengi, hapa dunia inakosea sana.

Utu wako haupimwi na kitu chochote kile cha nje, bali unapimwa kwa kuanzia ndani yako. wewe mwenyewe ndiye unayeamua utu wako uweje. Unaanza kujiheshimu wewe mwenyewe, iwe una kitu au huna, na wengine hawatakuwa na namna bali kukuheshimu. Unaanza kujipenda wewe mwenyewe iwe una marafiki wengi au wachache na utavutia wengi zaidi kuwa karibu na wewe.

Acha mara moja kushikiza utu wako kwenye vitu fulani, hata kama watu ndio wanataka kukuona hivyo.

Ukishikiza utu wako kwenye kazi unayoifanya, siku kazi hiyo itakapoisha au utakapofukuzwa au kupunguzwa, utapata uchungu wa kukosa kazi hiyo, lakini mbaya zaidi utapata uchungu kwamba utu wako umeharibiwa. Na hii ni mbaya sana kwani ndio itapelekea wewe kujitenga, kukata tamaa na hivyo kushindwa kuchukua hatua ya kuboresha maisha yako.

Utu wako ni zaidi ya kitu chochote ambacho watu wanakuona nacho. Utu wako ni wewe, na wewe ni muhimu kuliko kitu kingine unachojilinganisha nacho. Kwa kujua utu wako ni muhimu unakuwa huru kuchukua hatua za kuboresha maisha yako.

SOMA; Kitu Kimoja Kitakachokujengea Kujiamini Na Kujithamini.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba mimi ni mimi na utu wangu hautegemei kile ninachofanya au kile nilichonacho. Hata kama ninachofanya nitaacha, hata kama nilichonacho kitaondoka, mimi nitabaki kuwa mimi na maisha yangu ni lazima yaendelee. najua nina uwezo mkubwa ndani yangu na hivyo sihitaji kushikiza utu wangu kwenye kitu chochote.

NENO LA LEO.

“We cannot think of being acceptable to others until we have first proven acceptable to ourselves.” ― Malcolm X

Hatuwezi kufikiri kukubalika na wengine mpaka pale tutakapojikubali sisi wenyewe.

Wewe ni wewe na utu wako hautokani na chochote unachofanya au ulichonacho. Jikubali ulivyo na utakuwa huru kuishi maisha bora kwako.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.