Maisha ni ushawishi, kwenye kila siku yako unahitaji kuwashawishi watu kuchukua hatua fulani.

Kama unafanya biashara basi unahitaji kuwashawishi wateja wanunue kile unachouza, au unahitaji kuwashawishi wanaokusaidia kuweka juhudi zaidi. Pia unahitaji kuwashawishi watu kuwekeza kwenye biashara yako. ni ushawishi kila siku na kila wakati.

Kama umeajiriwa kila siku unahitaji kushawishi wengine. Unahitaji kumshawishi mwajiri wako akupe mazingira mazuri ya kazi na kipato kizuri pia. Unahitaji kushawishi mawazo yako mazuri ya uboreshaji yafanyiwe kazi. Unahitaji kuwashawishi wengine unaofanya nao kazi ili wakubaliane na wazo lako la uboreshaji kwenye kile mnachofanya.

Kwenye familia unahitaji kumshawishi mwenza wako kuchukua hatua fulani ambayo ni bora kwenye. Unahitaji kuwashawishi watoto wako kuchukua hatua ambayo ni bora kwao. Na unahitaji kuwashawishi wanaokuzunguka kuchukua hatua fulani ambayo itawanufaisha wote.

Kila mahali na kila siku ni ushawishi. Na hivyo tunaweza kusema kwamba yule mwenye uwezo mkubwa wa kushawishi ndiye atakayeweza kufikia mafanikio makubwa.

Lakini watu wengi hawana elimu ya ushawishi, hawajui mbinu za ushawishi, badala yake wamekuwa wakitumia mbinu ya kulazimisha. Kama ni mtu ambaye yupo chini yao, wanamlazimisha afanye kitu fulani na kama ni mtu yupo juu yao wanashinikiza kwa njia mbalimbali mtu afanye. Kulazimisha na kushinikiza hakujengi mahusiano mazuri, hata kama utapata unachotaka.

Njia ya uhakika, ya kukupatia unachotaka na wakati huo kujenga mahusiano mazuri ni kushawishi.

Leo nakupa njia moja ya uhakika ya kuweza kumshawishi mtu yeyote kufanya kitu, siku zijazo nitakupa njia nyingine pia.

Njia moja ya uhakika ya kumshawishi mtu kufanya kitu, ni kumpa sababu ya uhakika inayoendana na yeye na inayomsukuma kwa nini achukue hatua husika. Sababu hiyo lazima iendane na hali yake, na iwe kwamba kwa kuchukua hatua hiyo husika, maisha yake yatakuwa bora zaidi ya yalivyo sasa. Na ili uweze kutumia njia hii vyema ni lazima umjue mtu huyo vizuri, ujue ni nini anapendelea au ni nini hapendi, na kisha kuunganisha kile unachotaka afanye na faida ya kupata anachopendelea au kuondokana na asichopendelea.

Anza sasa kuwajua vizuri wale unaohusika nao, na jua kipi kinawahamasisha na kitumie pia kuwahamasisha kuchukua hatua ambayo ni muhimu kwa maisha yako. pia kuwa makini usitumie njia hii kuwanyonya watu, maana ni njia yenye nguvu sana na ukiitumia vibaya unaweza kuwanyonya watu na ikawa unawalazimisha bila ya wao kujua. Hakikisha unachotaka wafanye ni bora kwao pia.

SOMA; Sahau Kuhusu Kuongeza Faida Na Fanyia Kazi Kitu Hiki Kimoja Kwanza.

TAMKO LANGU;

Nimejifunza ya kwamba maisha ni ushawishi, chochote ninachotaka nitakipata kwa kuwashawishi wengine. Na njia bora ya kushawishi ni kumpa mtu sababu inayoendana na hali yake kwa nini achukue hatua fulani. Kuanzia sasa nitajifunza kuhusu wale wanaonizunguka ili nijue sababu zao kubwa ni nini na nitazitumia hizo kuwashawishi kuchukua hatua ambazo ni bora kwao pia.

NENO LA LEO.

Not brute force but only persuasion and faith are the kings of this world.

Thomas Carlyle

Sio nguvu ya ukatili bali ushawishi na imani pekee ndio wafalme wa dunia hii.

Chochote unachotaka kwenye maisha yako utakipata kama utaweza kuwashawishi wengine. Jifunze kuwa na ushawishi mzuri, utakuwezesha kufikia mafanikio.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.