Changamoto, vikwazo na matatizo ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Hakuna maisha yaliyonyooka tu, ambayo hayakutani na vitu hivyo.

Kuna kitu kimoja ambacho kimekuwa kinawapata watu wanaoingia kwenye matatizo. Tatizo moja ni kama linazaa matatizo mengi zaidi. Yaani mtu anaanza na tatizo moja na hatimaye anajikuta kwenye matatizo mengi zaidi. Hapa mtu anashawishika kwamba ana bahati mbaya au ana kisirani.

Sio kweli kwamba kuanza na tatizo moja halafu ukajikuta kwenye matatizo mengi ni bahati mbaya au kisirani, bali tatizo moja linakupelekea wewe kuzalisha matatizo mengi zaidi.

Unapokuwa kwenye matatizo, akili yako haifikiri sawa sawa, hii ni kwa sababu unakuwa umesongwa na hisia za tatizo ulilonalo, na hisia hizi zinakuzuia wewe kufikiri sawa sawa. Hivyo hatua yoyote unayochukua wakati ambapo upo kwenye matatizo, inakuwa sio hatua nzuri, na hiyo inapelekea matatizo mengi zaidi. Hisia unazokuwa nazo wakati wa matatizo inaweza kuwa hasira, hofu, chuki, kinyongo.

Nafikiri umewahi kuona mtu aliyefukuzwa kazi ametapeliwa au kupoteza fedha zaidi. Au mtu ambaye mahusiano yake yamevunjika anaingia kwenye mahusiano mabovu kuliko alikotoka. Haya yote yanatokana na kufanya maamuzi kwa kuongozwa na hisia. Na wakati ambao watu wameumizwa ndio wakati ambao wako hatarini kuumizwa zaidi.

Hivyo unapokuwa kwenye matatizo, kwanza acha kufanya maamuzi yoyote, tulia kwa muda kwanza. Mpaka pale utakapohakikisha hisia ulizonazo umeshazidhibiti. Kwa kutulia huku utaepuka kufanya maamuzi ambayo yatakupelekea kwenye matatizo mengi zaidi.

Unapokuwa kwenye matatizo, tulia, hakikisha hisia zako zimekwisha ndio ufanye maamuzi mengine, vinginevyo utajikuta kwenye matatizo mengi zaidi.

SOMA; Hisia mbili zinazowaongoza binadamu na jinsi ya kuzitumia kwenye biashara na ujasiriamali.

TAMKO LANGU;

Nimejua ya kwamba ninapokuwa kwenye matatizo ninakuwa na hatari ya kuingia kwenye matatizo mengi zaidi kama nitafanya maamuzi kwa kuendeshwa na hisia ninazokuwa nazo wakati huo. Kuanzia sasa nimeamua kutulia kwanza ninapokuwa kwenye matatizo, ili niweze kutuliza hisia zangu na kuweza kufikiri kwa kina ili nitakapofanya maamuzi, yawe bora kwangu.

NENO LA LEO.

Negative emotions like hatred destroy our peace of mind.

Matthieu Ricard

Hisia hasi kama chuki zinaharibu utulivu wa akili.

Usijaribu kufanya maamuzi yoyote ukiwa unaongozwa na hisia, maamuzi hayo yatakuingiza kwenye matatizo zaidi kwa sababu akili yako inakuwa haijatulia.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.